1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ni tete katika mpaka wa Ukanda wa Gaza

27 Desemba 2010

Hali katika eneo la mpaka wa Ukanda wa Gaza inaripotiwa kuwa ya wasiwasi baada ya wapiganaji wawili wa kiislamu kuuawa walipopambana na wanajeshi wa Israel.

https://p.dw.com/p/zqBU
Ukanda wa GazaPicha: AP

Kutokana na hali hiyo,pande zote mbili zimetishia kulipizana kisasi.Wakati huohuo, Israel inashikilia kuwa kamwe haitaiomba Uturuki radhi kwasababu ya kuushambulia mwezi wa Mei msafara wa meli za msaada uliokuwa ukielekea Gaza.Yote hayo yanatokea ikiwa imetimia miaka miwili tangu Israel kuushambulia Ukanda wa Gaza unaomilikiwa na Hamas.

NO-FLASH Israel erwidert Raketenangriff
Mtaa wa Rafa uliposhambuliwa na vikosi vya Israel:Ukanda wa Gaza ni eneo la makomboraPicha: picture alliance/dpa

Usalama wa Israel

Hali hiyo ya wasiwasi imetokea baada ya wapiganaji wawili kuuawa kwenye eneo la Ukanda wa Gaza linalopakana na Israel,jambo lililowafanya wawakilishi wa pande zote mbili kurushiana maneno makali na vitisho.Akizungumza kabla ya kikao cha baraza la mawaziri,Naibu Waziri Mkuu wa Israel ,Silvan Shalom, alisisitiza kuwa endapo makombora yataendelea kuilenga nchi yake na kuwaathiri raia wasiokuwa na hatia,bila shaka watalazimika kulipiza kisasi kwa kutumia nguvu zote.Hata hivyo alieleza kuwa,''Israel ni mshirika wa ulimwengu ulio huru.Baadhi ya nyakati tunadhani kwamba mataifa mengine hayayafahamu mazigira tunamoishi.Kuna makundi kama Hamas na Hezbollah yanayotaka kuishambulia Israel.Kwahiyo lazima Israel iulinde usalama wake,''aliweka bayana.


Hatuogopi na tuko imara!

Kwa upande wao,wapiganaji wa kiislamu wa Jihad na Hamas walitishia kuwa huenda wakalipiza kisasi baada ya watu wao kuuawa wakati wa mapambano kati yao na wanajeshi wa Israel.Kauli hizo zimetolewa wakati wa maziko ya wapiganaji hao wawili.Mauaji hayo yalitokea mapema jana asubuhi pale wanajeshi wa Israel waliojihami kwa silaha nzito walipowavamia wapiganaji hao wa Kiislamu waliokuwa wakijaribu kutega mabomu kwenye eneo la mpakani la Gaza. 

Kwa mujibu wa msemaji wa kundi la wapiganaji la kiislamu la Jihad,wao wako tayari kulipiza kisasi endapo Israel itaendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza.Kauli hizo ziliungwa mkono na Hamas.Abu Obeida ni msemaji wa kitengo cha kijeshi cha Hamas na anafafanua,''kuwa adui wetu wa Kiyahudi lazima aelewe kwamba hatutatulia ikiwa mashambulio yataendelea.Kwamba wapiganaji wa Qasam wametulia haina maana kwamba hatuna nguvu.Tunaitathmini hali tu.Endapo watatuchokoza watashangaa na tutawazuwia,''alisisitiza.

Makombora na mashambulio

Hali katika Ukanda wa Gaza imezidi kuwa tete kwasababu makundi ya wapiganaji yamekuwa yakilifyatulia makombora eneo la kusini mwa Israel ambayo imelazimika kufanya mashambulio ya ndege yanayoyalenga mahandaki yanayotumiwa kusafirishia bidhaa kimagendo huko Ukanda wa Gaza.Hali hiyo ya usalama imewawia vigumu wakazi wa Ukanda wa Gaza wanaohitaji bidhaa za matumizi za dharura.

Superteaser NO FLASH Israel Mavi Marmara Gaza Flotte
Meli ya Mavi Marmara iliyoshambuliwa na Israel:Wakazi wa Gaza wanahitaji msaada wa bidhaa za matumiziPicha: AP

Wakati huohuo,Israel inashikilia kuwa kamwe haitoiomba radhi Uturuki baada ya kuushambulia msafara wake wa meli zilizokuwa zikielekea Ukanda wa Gaza mwezi wa Mei.Meli hizo zilizokuwa zimesheheni bidhaa za misaada zilishambuliwa na Israel inayodai kwamba wakazi wa Gaza hawazihitaji.

Stihizai

Akizungumza kwenye kikao cha mabalozi wa Israel mjini Jerusalem,Waziri wa mambo ya nje ,Avigdor Liebermann,alisema kuwa dai hilo la Uturuki ni sawa na stihizai.Kulingana na rasimu ya makubaliano ya kutafuta suluhu ya mzozo kati ya mataifa hayo mawili,Israel inapaswa kuitaka radhi Uturuki,kuurejesha rasmi uhusiano wao kadhalika kuwalipa fidia jamaa wa mkasa huo.Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alijitenga na kauli hizo na akasisitiza kuwa huo ulikuwa mtazamo wa binafsi.

Uhusiano kati ya Israel na Uturuki umezidi kuvurugika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tangu tukio hilo kutokea lililosababisha mauaji ya wanaharakati 9 wa Kituruki.

Kwa upande mwengine,maelfu walikusanyika bandarini mjini Istanbul hapo jana ili kuilaki meli iliyowasili iliyokuwa ikiuongoza msafara huo wa bidhaa za msaada.Kundi la kutoa misaada la Uturuki lilichukua fursa hiyo pia kutangaza kwamba meli hiyo Mavi Marmara itajaribu kufunga safari nyengine kama hiyo mwakani.   

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-RTRE/AFPE

Mhariri:Aboubakary Liongo