1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ni tete nchini Afghanistan

14 Oktoba 2009

<p>Hali nchini Afghanistan inaendelea kuwa tete, ambapo kamanda mkuu wa vikosi vya Marekani nchini humo Stanley McCrystal, ameelezea juu ya tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwa serikali ya Afghanistan.</p>

https://p.dw.com/p/K5sh
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akabiliwa na kazi nzito ya kutafuta imani ya wananchiPicha: PA/dpa

Duru za Washington zimemkariri McCrystal akionya kuwa, mapigano dhidi ya kikundi cha Taliban yamo hatarini.

Maelezo hayo yametolewa katika ripoti ambayo hata hivyo bado haijachapishwa, ambapo kamanda huyo wa kimarekani amesema, hata kama maelefu ya nyongeza ya wanajeshi wa kimarekani yatapelekwa nchini Afghanistan, bado operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya kikundi cha Taliban iliyodumu kwa miaka minane, itashindwa kufanikiwa.

Rais wa Marekani Barack Obama, wiki hii anafanya mzunguko mwingine wa mikutano na washauri wake wakuu, kujaribu kutafuta hatua inayofuata nchini Afghanista na Pakistan.

Kamanda McCrystal ameomba nyongeza ya wanajeshi wengine 40,000 nchini Afghanistan.

Uingereza kwa kwa upande wake, imetangaza leo kupeleka nyongeza ya wanajeshi 500 wa ziada nchini Afghanistan, na hivyo kufanya idadi ya jumla ya wanajeshi wake nchini humo kufikia 9,500.

Katika taarifa yake kwa bunge, Waziri Mkuu Gordon Brown, anatarajiwa kuwahimiza wanachama wengine wa NATO barani Ulaya kuchukua hatua kama yake ya kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Afghanistan.

Gordon Brown besucht die britischen Soldaten
Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown, katikati, ataka kuwahimiza wanachama wa NATO waongeze wanajeshi nchini AfghanistanPicha: AP

Hatua hiyo inakuja baada ya mashauriano makubwa juu ya mbinu

za Marekani na Uingrereza, juu ya vita vya Afghanistan.

Uamuzi huo wa kupeleka wanajeshi zaidi wa kiingereza nchini Afghanistan, unagongana na kura za maoni zilizoendeshwa leo, ambapo zaidi ya robo tatu ya watu waliopiga kura hizo, wametaka majeshi ya waingereza yaondolewe Afghanistan.

Kwa mujibu wa kura hizo zilizochapishwa na gazeti la Times, asilimia 36 ya kura zinataka majeshi hayo yarudi nyumbani, tofauti na asilimia 29 ya kura kama hizo zilizoendeshwa wiki nne zilizopita.

Nyongeza hiyo ya wanajeshi itapelekwa katika jimbo la kusini la Helmand, ambapo kiasi cha wanajeshi 221 wa Uingereza tayari wamepoteza maisha katika jimbo hilo.

Wakati huo huo, ikiwa karibu miezi miwili tangu kumalizika kwa uchaguzi nchini Afghanistan, na bado hakuna matokeo rasmi, rais Hamid Karzai sasa anakabiliwa na kibarua kizito cha kutafuta imani ya wananchi juu ya timu yake ya uongozi ambayo inazongwa na tuhuma za kufanya hila wakati wa uchaguzi.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yakiwa yanatarajiwa kutolewa baadaye wiki hii, yanaweza bado yakamlazimisha Karzai kurudiana tena na mpinzani wake mkubwa Abdullah Abdullah, katika awamu nyingine ya uchaguzi, kama jopo linaloshugulikia malalamiko ya uchaguzi, litaona kuwa hakufikisha asilimia 50 ya kura hizo.

Wakati hayo yakijiri, rais Hamid Karzai amelalamika nchi yake kuendelea kushambuliwa na wanamgambo wa Taliban, akidai kuwa wamekuwa wakiendesha mashambulizi kutokea nchini Pakistan:

"Maelfu ya wapiganaji wa Taliban kutokea Pakistani wanakuja kutuua.

Je sisi tufanye nini? Lazima tujilinde, na lazima tuwashinde wataliban kule kwenye ngome yao."

Historia ya nchi ya Afghanistan imekuwa yenye utata na mizozo mingi, iliyokumbwa na uvamizi wa kigeni pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miongo mitatu sasa.

Mwandishi:Lazaro Matalange/RTE/DPA

Mhariri:Abdul-Rahman.