1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali si shwari Madagascar.

Halima Nyanza/Reuters13 Machi 2009

Wanajeshi walioasi nchini Madagascar leo wamesambaza vifaru tayari kwa mapigano katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo na kuarifu kuwa watavitumia kupambana na mamluki yoyote.

https://p.dw.com/p/HBEr
Moja wapo ya hasara zilizokumba jamii, kutokana na mvutano wa kugombea madaraka kati ya Rais wa Madagascar, Marc Ravalomanana na mpinzani wake Andry Rajoelina.Picha: picture alliance / landov

Wanajeshi nchini humo wameasi kutoka katika jeshi la serikali la nchi hiyo kwa kusema kuwa wanataka kurudisha hali ya utulivu katika nchi hiyo ambayo kwa sasa imekumbwa na machafuko ya liyosababisha na mvutano kati ya Rais wa nchi hiyo Marc Ravalomanana na Mpinzani wake Andry Rajoelina.

kizungumzia hali hiyo, msemaji wa wanajeshi hao walioasi, Kanali Noel Rakotonandrasa, amefahamisha kuwa vifaru hivyo vya jeshi vimetawanywa katika sehemu ya siri na sio mitaani.


Ameongezea kusema kuwa hatua hiyo ni ya tahadhari na kwamba watawakamata mamluki wowote watakao kwenda huko.


Wengi katika upande wa upinzani wamekuwa na hofu kuwa Rais wa nchi hiyo ataleta mamluki ili kuweza kumsaidia kulinda nafasi yake madarakani.


Hata hivyo, wanajeshi hao walioasi wamekana taarifa kwamba wamekuwa wakipewa amri kutoka kwa kiongozi wa upinzani.


Msemaji huyo wa wanajeshi walioasi, amekanusha pia taarifa kwamba vikosi hivyo vya wanajeshi vimesambazwa karibu na makazi ya Rais wa nchi hiyo, na kuongeza kwamba hawana nia ya kumshambulia kiongozi huyo.


Aidha amekataa kusema ni vifaru vingapi vilivyotawanywa.


Machafuko hayo yanayotokea sasa nchini Madagascar yameelezwa kuwa ni mabaya kabisa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka kadhaa, ambapo mpaka sasa haieleweki wazi nani anadhibiti serikali na Jeshi.


Hali ya kugombea madaraka kati ya Rais Marc Ravolamanana na mpinzani wake, Andry Rajoelina, imekuwa ikiongezeka wiki hii, ikiwemo kufukuzwa kazi kwa mkuu wa Jeshi ambaye alitishia kufanya mapinduzi iwapo viongozi hao wa kisiasa watashindwa kumaliza machafuko yanayotokea nchini humo.


Jumatano wiki hii, kiongozi wa wanajeshi walioasi katika jeshi la nchi hiyo alijitangaza kuwa mkuu wa majeshi na kumuondoa madarakani Jenerali mkuu, ambaye aliwapa viongizi haio wanaopingana saa 72, mpaka leo wawe wametafuta suluhu ama jeshi litaingilia kati.


Hali hiyo ya ghasia inaelezwa kuathiri sana biashara ya utalii ambayo inaingizia nchi hiyo kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.


Jana Rais wa nchi hiyo Marc Ravalomanana alitaka majeshi ya nchi hiyo kutekeleza majukumu yao na kuwalinda raia.


Akihutubia baraza la Mawaziri, Rais Ravalomanana aliahidi kufanya juhudi za kurudisha tena amani na usalama nchini humo.


Mazungumzo yaliyopangwa na Umoja wa Mataifa kati ya pande hizo mbili zinazopingana yameahirishwa.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataiafa, Ban Ki Moon, amezitaka pande hizo mbili, kutatua tofauti zao kwa amani na kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Marekani imewaonya watu wake walioko nchini Madagascar kuzingatia kuondoka nchini humo kutokana na hali ya usalama iliyopo.


Umoja wa Ulaya nao umeonya kuwa suluhu yoyote inakayofanywa kinyume na katiba katika kusuluhisha mzozo huo wa kisiasa, itapelekea kusimamishwa kwa misaada inayotolewa kwa nchi hiyo.



Mwandishi: HalimaNyanza/Reuters

Mhariri: Othman Miraji