1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha vita vya wenyewe kwa wenyewe

7 Agosti 2015

Kujeruhiwa vibaya sana mwanaharakati wa haki za binaadam Burundi, wakimbizi wa Calais na jinsi nishati mbadala inavyowavutia wakaazi wa mashambani Kenya ni miongoni mwa mada kuhusu bara la Afrika magazetini wiki hii.

https://p.dw.com/p/1GBVy
Mwanaharakati wa haki za binaadam Pierre-Claver MbonimpaPicha: Getty Images/AFP/A. Vinceno

Tuanzie lakini Burundi ambako ripoti kuhusu hali tete na hata mauwaji zinaendelea kusikika.Gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin linazungumzia kuhusu shambulio dhidi ya mwanaharakati wa haki za binaadam Pierre Claver Mbonimpa aliyejeruhiwa vibaya sana kufuatia njama ya kutaka kumuuwa.Die Tageszeitung linaelezea jinsi mwanaharakati huyo, ambae kwa miaka kadhaa sasa amekuwa akipambana na kuandamwa wapinzani na kuwashughulikia pia wahanga wa vituko vya polisi nchini Burundi alivyopigwa risasi akiwa ndani ya gari yake jumatatu usiku alipokuwa njiani kwenda kukutana na ujumbe wa Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Burundi-Bujumbura.Hali yake ni mbaya sana na gazeti hilo la mjini Berlin, die Tageszeitung linanukuu ripoti zinazosema Pierre Claver Mbonimpa ameruhusiwa hatimae kuwenda nchi za nje kufanyiwa matibabu. Pierre Claver Mbonimpa,linaandika gazeti la die Tageszeitung ameunda shirika la kupigania haki za binaadam na haki za wafungwa mwaka 2001 .Kadri miaka inavyoendelea ndipo na yeye anapozidi kupata sifa ya kuwa mwanaharakati asiyeelemea upande wowote anayekosoa vitisho na mateso yanayofanaywa na serikali na vyombo vyake vya sheria.Gazeti linazungumzia mahojiano aliyokuwa nayo na gazeti hili la Taz muda mfupi kabla ya uchaguzi unaozozaniwa wa rais wa julai 26 iliyopita.Katika mahojiano hayo Mbonimpa aliwatuhumu wanamgambo wa tawi la vijana la chama tawala Imbonerakure,kuwatisha wananchi na kuzusha kitisho cha kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Shambulio dhidi ya mwanaharakati wa haki za binaadam Mbonimpa ni kisasi cha kuuliwa kiongozi wa zamani wa idara ya upelelezi,msimamizi wa wanamgambo wa Imbonerakure, Adolphe Nshimirimana-linaandika gazeti la die Tageszeitung.

Hali inatisha Burundi

Hali nchini Burundi imechambuliwa pia na gazeti la Neues Deutschland ."Vita vya wenyewe kwa wenyewe ni njia mojawapo" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalozungumzia madai ya upande wa upinzani ya kugawana madaraka,la sivyo kuna kitisho cha kuripuka mapigano.Kitisho hicho bado kipo kwasababu pia rais Pierre Nkurunziza mpaka sasa bado hayuko tayari kuunga mkono madai hayo ya upande wa upinzani.Kitisho cha vita kiwepo au kisiwepo,hali ya kiuchumi ya Burundi inaelekea kuporomoka linaandika gazeti la Neues Deutschland.Pekee mwezi wa juni mwaka huu ughali wa maisha uliongezeka kwa asili 7.7.Mustakbal wa Burundi kwa hivyo bado si bayana.Shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka,linakadiria warundi 2500 wanavuka mpaka kila siku na kukimbilia Tanzania.Wengine wanakimbilia Rwanda na katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.Wimbi la wakimbizi ni kubwa mno kwa namna ambayo uwezo wa mapokezi katika kambi zilizoko Nyarugusu karibu na mpaka umepindukia kwa asili mia 250 .

Ukosefu wa tamaa miongoni mwa wakimbizi wa Calais

Suala la wakimbizi limejadiliwa pia na Frankfurter Allegemeine.Lakini ripoti ya gazeti hilo miongoni mwa magazeti mashuhuri ya humu nchini inagusia zaidi wakimbizi wa kiafrika wanaozurura katika mji wa kaskazini wa Ufaransa Calais wakisubiri nafasi ya kuparamia malori na kuingia kichini chini nchini Uengereza.Kila siku wakimbizi hao wanajaribu bahati yao lakini bila ya mafanikio linasema Frankfurter Allgemeine linalowanukuu wakimbizi hao wakisema;hawana njia nyengine.

Wanavijiji kujivunia nishati mbadala Kenya

Ripoti yetu ya mwisho inahusiana na matumaini ya kuenea umeme nchini Kenya.Sheria mpya kuhusu mabadiliko ya tabia nchi zitasaidia kuharakisha matumizi ya teknolojia isiyochafua sana mazingira na kuhimiza nishati mbadala-hicho ndicho kichwa cha maneno cha ripoti nyengine ya gazeti la Neues Deutschland kuhusu bara la Afrika wiki hii.Gazeti hilo linahisi mitambo midogo midogo ya nishati ya juwa( au kawi ya juwa kama nchini Kenya wanavyosema itawavutia zaidi wakaazi wa mashambani.Ili kuhimiza matumizi ya mitambo isiyochafua mazingira, kodi pia zinabidi zipunguzwe.

Mwandishi:Hamidou Oummil;BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri: Iddi Ssessanga