1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hatari yatangazwa Charlotte kufuatia maandamano

Yusra Buwayhid22 Septemba 2016

Kumezuka maandamano ya watu walio na hasira katika maeneo ya mji wa Charlotte nchini Marekani, baada ya polisi kumpiga risasi mwanaume mmoja mweusi, huku kukiwa na maelezo yanayotofautiana juu ya tukio hilo.

https://p.dw.com/p/1K6P6
USA Polizei erschießt Afro-Amerikaner in North Carolina - Proteste
Picha: Reuters/J. Miczek

Mkesha wa maombi uliokuwa wa amani, ghafla uligeuka kuwa maandamo ya watu waliokuwa na hasira, na baadae ukawa usiku wa vurugu kubwa baada ya mtu huyo kupigwa risasi na kuachwa na majeraha mabaya sana, huku waandamanaji wakiwavamia polisi waliokuwa wakijaribu kuwatawanya.

Kumekuwa na maelezo yanayotafautiana juu ya tukio hilo. Mkuu wa polisi wa mji wa Charlotte , Kerr Putney, awali aliripoti kuwa mtu mmoja aliyepigwa risasi wakati wa maandamano hayo ameuawa, lakini maafisa wa mji baadae waliandika katika ukurasa wao wa Twitter kwamba mtu huyo amepelekwa hospitali na yupo katika hali mbaya saa.

Maafisa hao pia wamesema mtu huyo alipigwa risasi na raia mwenzake na si polisi. Aidha, afisa mmoja wa polisi ameripotiwa kuwa anapata matibabu hospitali baada ya kupata majeraha wakati wa maandamano hayo ya jana usiku.

Mmoja wa waandamanaji Braxton Winston amerekodiwa akizungumza kwa hasira huku akiwa amezungukwa na waandamanaji wenzake akimtaka Mkuu wa polisi atoke nje ya jengo aje azungumza nao.

“Daima mnatuambia yale tusioruhusiwa kufanya. Haturuhusiwi kupiga magoti. Haturuhusiwi kuandamana. Haturuhusiwi kusimama. Hatuna ruhusa ya kuimba. Kitu gani tunachoruhusiwa kufanya. Chifu Kerr Putney, toka nje uje utueleze kile tunachoruhusiwa kufanya, ” amesema Braxton Winston.

Gavana wa jimbo la North Carolina, Pat McCrory ametangaza hali ya hatari jana usiku katika mji mkubwa wa jimbo hilo wa Charlotte, na baadae kuita kikosi cha ulinzi wa taifa baada ya Mkuu wa polisi wa Charlotte kusema wanahitaji msaada.

Waandamanaji waharibu majengo ya biashara

USA Polizei erschießt Afro-Amerikaner in North Carolina - Proteste
Polisi wakikabiliana na waandamanaji mjini Charlotte, MarekaniPicha: Reuters/Charlotte Magazine/Adam Rhew

Jana usiku, mamia ya waandamanaji waliokuwa wakipiga mayowe "Maisha ya watu weusi yana thamani" pamoja na "mikono juu, usifyatuwe risasi" walitawanyika baada ya polisi kuanza kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.

Lakini makundi kadhaa ya waandamanaji yalibaki, na kushambulia raia, wakiwamo maripota, walivunja vioo vya madirisha ya mahoteli, majengo ya maofisi, migahawa huku wakiwasha moto mdogo katika maeneo tofauti.

Vurugu ziliibuka watu walipoanza kuuliza masuali mengi kuhusu tukio la Jumanne la kifo cha Keith Lamont Scott, menye umri wa miaka 43 aliyepigwa risasi karibu na jengo analoishi. Polisi wamekataa kutoa mkanda wa video wa ushahidi wa tukio hilo lakini wamesema Scott alikuwa amebeba bunduki na alikataa mara kadhaa kufuata amri za polisi za kuweka silaha chini. Hata hivyo, familia ya Scott pamoja na majirani zake wanasema hakuwa amebeba bunduki bali kilikuwa ni kitabu.

Vurugu za Charlotte zimewastaajabisha wengi, mji huo unaojulikana kwa biashara za mabenki Kusini mwa Marekani, hauna kawaida ya kutokea vurugu zinazohusiana na ubaguzi wa rangi wa polisi. Mji wa Charlotte una idadi ya watu wapatao 830,000 na asilimia 35 miongoni mwao ni watu weusi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape

Mhariri: Daniel Gakuba