1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hofu yaanza kutanda Sudan

Nijimbere, Gregoire15 Julai 2008

Wasi wasi imeanza kujitokeza nchini Sudan na kikosi cha Umoja wa mataifa cha kulinda amani Darfur kimeanza kuwaondoa wafanyakazi wake kutoka Sudan huku maandamano ya kumuunga mkono rais al-Bashir yakifanyika.

https://p.dw.com/p/Ed3M
Rais wa Sudan Omar Hassan al-BashirPicha: AP

Maandamano hayo ya kumuunga mkono rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir yameanzia kwenye chuo kikuu hadi ofisi ya tawi la Umoja wa mataifa linalohusika na maendeleo UNDP na kwenye Ubalozi wa Uingereza mjini Khartoum. Waandamanaji wamesema na hapa ninanukuu ´´ tupo jeshi la Mtume Muhamad na tupo tayari kumwaga damu yetu kumhami rais wetu´´ .

Hapo walikuwa wakipaza sauti za kupinga hatua ya mwendeshamashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya jinai ya mjini The Hague Uholanzi Luis Moreno Ocampo ya kutaka mahakama hiyo itowe waranti wa kumkamata rais wa Sudan al-Bashir kuzijibu tuhuma za mauaji ya kuangamiza jamii, uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binaadamu katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan ambako kulingana na makisio ya Umoja wa mataifa watu laki mbili wameshauawa na wengine milioni 2 na nusu kuyahama maskani yao tangu vita kuzuka katika jimbo hilo miaka mitano iliopita.

Hatua hiyo ya kumfungulia mashtaka rais wa Sudan imezusha wasi wasi hata katika kikosi cha majeshi ya Umoja wa mataifa cha kulinda amani katika jimbo la Darfur, UNAMID ambacho kimeanza kuwaondoa wafanyakazi wake wa kawaida. UNAMID imetangaza kuwa wafanyakazi wake kiasi ya 200 wamehamishiwa nchini Uganda na Ethiopia na kwamba wengine watafuata licha ya ahadi ya serikali ya Sudan kwamba itafanya kila iwezalo kulinda usalama wa wanajeshi na wafanyakazi wengine wanaohusika na shughuli za kibinaadamu. Mashahidi wamesema basi mbili za wafanyakazi hao zimeondoka makao makuu ya UNAMID mjini Al-Fasher na mji mkuu katika jimbo la Darfur na kuelekea Entebbe Uganda.


Hata wanajeshi wa kikosi cha kijeshi cha Umoja wa mataifa cha UNAMID ambao watabaki Darfur, bado wanategemea ulinzi kutoka kwa serikali ya Sudan.

Licha ya mkataba huo kuwa hatarini, Umoja wa mataifa umesema kwamba utaendelea na shughuli zake nchini Sudan. Msemaji wa Umoja wa mataifa Brian Kelly, amesema ´´tuna wajibu wa kushiriki katika shughuli za kulinda amani nchini Sudan`´ kabla ya kuendelea kukumbusha kuwa usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa mataifa na mashirika ya huduma za kibinaadamu ni muhimu. Wadadisi wengi wa maswala ya kisiasa wanasema kuwa hatua ya kumshtaki rais wa Sudan itazidi kuiathiri hali ya mambo katika jimbo la Darfur na mashirika ya misaada kushindwa kufanya kazi ipasavyo na watakaoathiriwa zaidi daima ni wakimbizi zaidi ya milioni 2 wanaohitaji misaada ya dharura.