1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kilimo duniani yatia moyo

Josephat Nyiro Charo15 Juni 2010

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, pamoja na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, hii leo yametoa ripoti ya pamoja ya mwaka kuhusu hali ya kilimo duniani

https://p.dw.com/p/NrWy
Jacques Diouf, mkurugenzi wa shirika la kilimo na chakula la Umoja wa MataifaPicha: AP

Katibu mkuu wa shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, Angel Gurria, amesema leo mjini Roma Italia kwamba hali ya sasa ya kilimo duniani inaonyesha kwamba bei ya bidhaa nyingi za kilimo zitaongezeka katika muongo ujao. Hata hivyo kiongozi huyo amesisitiza kwamba serikali zinaweza kusaidia kwa kuhakikisha kwamba taasisi, sera na teknolojia zinakuwepo ili kuwasaidia wakulima kuwekeza katika kuongeza ukuzaji wa mazao.

Katika ripoti hiyo bei za bidhaa za kilimo zinatarajiwa kuongeza katika kipindi cha miaka 10 ijayo, ubashiri ambao huenda ukawa ni habari njema kwa wakulima, ikiwa utaainishwa na sera zifaazo.

Mkurugenzi wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, bwana Jacques Diouf, amesema sio swala la idadi ya wakaazi bali ni swala la teknolojia, uwekezaji na sera. Ameongeza kusema huku asilimia 2 pekee ya idadi ya wakaazi katika nchi zilizoendelea wakiwa wanakuza mazao yao wenyewe na kutosheleza mahitaji yao ya chakula, katika nchi zinazoendelea kiasi cha asilimia kati ya 60 na 80 ya wakaazi wanahitajika kukuza mazao kwa ajili ya chakula, na kiwango kinachopatikana kinakuwa hakitoshi kuwalisha watu wote.

Bwana Diouf ameyasema hayo mini Roma wakati wa kutolewa rasmi ripoti kuhusu hali ya kilimo duniani inayosema kuongezeka kwa ukuzaji wa chakula katika nchi ambazo hazijaendelea sana duniani, bado ni kwa mwendo wa kinyonga katika kukabiliana na ongezeko la idadi ya wakaazi.

Doiuf ameitaja China, Brazil, India, Urusi na Ukraine kama matifa ambako ukuzaji wa chakula umeongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko nchi nyingine duniani. Amezipongeza nchi hizo kwa kuwa na sera nzuri zinazohitajika kuongeza ukuzaji wa chakula na kusisitiza kwamba kuna ishara ya matumaini makubwa kuhusu ukuzaji wa chakula katika siku za usoni.

Katika ripoti ya shirika la FAO na OECD, uzalishaji wa bidhaa za kilimo unatarajiwa kuongezeka katika muongo ujao ikilinganishwa na muongo uliopita. Uzalishaji wa chakula unaendelea kwa kasi ya kutia moyo kama inavyotakiwa huku ukuzaji wa chakula duniani kote ukitarajiwa kufikia asilimia 70 kufikia mwaka 2050. Hata hivyo uhakika wa kupatikana chakula bado ni suala la kutia wasiwasi, ikikumbukwa kwamba mnamo mwaka 2008 kulifanyika mandamano katika nchi mbalimbali duniani kupinga kupanda kwa bei za chakula na nishati.

Ripoti ya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD, inahimiza ukuzaji wa mazao na kuboresha kilimo. Inasema mfumo mzuri wa kibiashara utakaofanya kazi bila vikwazo na unaoongozwa na sheria zinazofaa, utasaidia kuhakikisha kuna ushindani wa haki wa kibiashara na kuhakikisha pia kwamba chakula kinasafirishwa kutoka maeneo ya kilimo hadi maeneo ambayo bado yako nyuma maswala ya kilimo.

Ripoti hiyo inasema nchi zinazoinukia kiuchumi zitaongoza katika shughuli za kilimo duniani, matumizi ya chakula na biashara. China imetajwa kuwa nchi inayobadili mkondo wa dunia wa ukuzaji wa mazao ya kilimo.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraji