1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya maafa ya kiutu yainyemelea Fallujah

1 Juni 2016

Hali ya kiutu mjini Fallujah imeporomoka haraka tangu majeshi ya serikali kuanzisha operesheni maalum ya kuukomboa mji huo wa magharibi kutoka kwa wanamgambo wa Dola la Kiislamu siku kumi zilizopita.

https://p.dw.com/p/1Iy5O
Irak Falludscha Kämpfe IS
Mashambulizi ya jeshi la serikali dhidi ya mji wa FallujahPicha: Getty Images/AFP/A. Rubaye

Wakati huo huo Umoja wa mataifa umetoa tahadhari jana kuhusiana na hatima ya familia 300 hadi 400 za Wairaki waliokusanywa na wapiganaji wa jihadi wa Dola la Kiislamu , huenda kwa matumizi kama ngao ya binadamu katika mapigano katika mji huo.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamepata "ripoti za kuaminika kwamba familia hizo zinapelekwa katika kituo katika mji huo unaodhibitiwa na kundi la Daesh na kwamba hawaruhusiwi kuondoka katika maeneo hayo," naibu mwakilishi wa Umoja wa mataifa nchini Iraq Lise Grande, amesema akitumia neno hilo la Kiarabu akiwa na maana ya Dola la Kiislamu.

Irak Militäroperation gegen IS Falludscha
magari yenye silaha yakielekea FallujahPicha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

"Hii itakuwa na maana kwamba Daesh wanaweza kuwatumia watu hawa , ama wanapanga kuwatumia kama aina fulani ya ngao ya binadamu," amewaambia waandishi habari.

"Watu hao wako katika hatari kubwa iwapo kutakuwa na mapambano ya kijeshi." Majeshi ya Iraq yalianzisha mashambulizi wiki moja iliyopita kwa nia ya kuukomboa mji wa Fallujah , ambao umekuwa ngome kuu ya kundi la IS baada ya kuukamata Januari mwaka 2014.

Umoja wa Mataifa watoa onyo

Umoja wa mataifa umeieleza serikali ya Iraq kuhusu hali hiyo, mbayo imepunguza kasi ya operesheni yake kujaribu kuzilinda familia zilizokwama katika mji huo.Kamanda wa kikosi cha kwanza cha jeshi la Iraq maalum kwa mapambano dhidi ya magaidi Luteni Kanali Muhand al-Tamimi amesema mapambano bado yanaendelea.

Irak Falludscha Kämpfe IS
Wanajeshi wa jeshi la serikali wakifurahia kukombolewa kwa vijiji karibu na FallujahPicha: Getty Images/AFP/A. Rubaye

"Vikosi vya kupambana na magaidi vimeendelea kusonga mbele kuelekea malengo yaliyopangwa kuukomboa mji wote wa Fallujah kutoka kundi la Dola la Kiislamu. Mungu akijalia vikosi vyetu vina nia ya kuukomboa kabisa mji wote."

Serikali ina tambua haja ya kuwalinda raia wakati wa mashambulizi, Grande amesema. Ni raia 5,000 kati ya 50,000 ambao wamekwama katika mji huo wamefanikiwa kukimbia , wengi wao walitembea kwa masaa kadhaa na walishambuliwa wakati wakikimbia, Grande amesema.

Familia zilizokimbia kutoka vijiji vya karibu zimelifahamisha baraza la wakimbizi la Norwey NRC kwamba mji wa Fallujah , unashambuliwa kutoka katika pande tatu tofauti, na kusababisha kuwa na njia chache salama za kukimbia.

Irak Falludscha Kämpfe IS
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Mohammed

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF limetoa onyo kali kwa majeshi ya Iraq na wanamgambo wa Dola la Kiislamu kuwalinda watoto wakati wa mapambano ya kuukomboa mji wa Fallujah. UNICEF imesema leo kwamba ina wasi wasi kuhusu watoto wanaokadiriwa kufikia 20,000 waliokwama katika mji huo, wakati wachache wamefanikiwa kukimbia kutoka mji huo tangu mashambulizi yalipoanza.

Kwa mujibu wa shirika hilo, Iraq inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kiutu , ambapo watu wanaokadiriwa kufikia milioni 10 wanahitaji msaada na kiasi ya wengine milioni 3.4 wametawanyika katika nchi hiyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Mtullya Abdu