1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Mashariki ya kati

Hamidou, Oumilkher18 Januari 2008

Israel inaendelea kuwahujumu wanaharakati wa Hamas wanaovurumisha makombora dhidi ya maeneo yakie ya kusini.

https://p.dw.com/p/CtTv
Damu inazidi kumwagika Mashariki ya kati.Picha: AP



Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon anasema ameingiwa na hofu kutokana na kuzidi  matumizi ya nguvu katika ardhi za wapastina na nchini Irael,akiitolea mwito Israel ijizuwie na wapalastina waache mashambulio yao.



Jeshi la Israel limezidisha mashambulio yake dhidi ya Gaza mnamo siku za hivi karibuni-likijibu makombora yanayofyetuliwa na wanamgambo wa Hamas dhidi ya Israel.Wapalastina 32 wameuliwa wiki hii kufuatia mashambulio hayo.


Waziri mkuu Ehud Olmert amesema wataendelea kuwaandama magaidi wanaovurumisha makombora dhidi ya maeneo ya kusini mwa Israel.


"Katika eneo la kusini mwa Israel,vita vinaendelea na tutafanya kila liwezekanalo kuzuwia mashambulio,tutawaandamana bila ya huruma wanaharakati wa hamas,JIhad na maadui wote wengine"-amesisitiza waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.



Katika mashambulio ya jana wapalastina watano wameuliwa,wakiwemo wanawake wawili huku waziri wa ulinzi Ehud Barak akiamuru vivukio vyote kati ya Israel na Gaza vifungwe.


Amri hiyo itakayoendeleya kwa siku kadhaa inahusu pia magari yanayosafirisha bidhaa na binaadam.


Tangu miezi kadhaa sasa Israel imeiwekea vikwazo vya kiuchumi Gaza,inayotajwa kua " ardhi adui" tangu wafuasi wa Hamas waliponyakua uongozi wa eneo hilo msimu wa kiangazi uliopita.


Hata hivyo hii ni mara ya kwanza kwa amri kali kama hiyo kutangazwa dhidi ya eneo hilo wanakoishi watu zaidi ya milioni moja na laki tatu.


Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ameingiwa na wasi wasi kutokana na kuzidi matumizi ya nguvu huko Gaza na kusini mwa Israel.


Katika taarifa yake,katibu mkuu wa Umoja wa mataifa amehimiza mashambulio ya wanaharakati wa hamas dhidi ya Israel yakome na kuitaka Israel ijizuie."


Katibu mkuu Ban Ki-Moon amezikumbusha pande zote mbili wajib wao katika kujifungamanisha na  sheria za kimataifa na kutoyatia hatarini maisha ya raia wasiokua na hatia.


"Mashambulio ya Israel ni pigo kwa juhudi za amani kati ya Israel na Palastina" amesema msemaji wa kiongozi wa uitawala wa ndani wa Palastina-Nabil Abou Roudeina.


Ameitolea mwito Marekani iingilie kati haraka kuepusha hali isizidi kuharibika na kukorofisha kile alichokiita "fursa ya kihistoria ya kupatikana amani."


Kwa upande wake serikali ya Marekani imeitaka Israel ifanye kila liwezekanalo kuwaepushia madhara raia wa kawaida huko Gaza."


Serikali ya mjini Washington imeyataja hata hivyo mashambulio ya Israel dhidi ya Gaza kua "kiinga ya haki dhidi ya makombora yanayopfyetuliwa na Hamas.


Zaidi ya watu elfu sita na 85 wameuwawa kufuatia mashambulio kati ya Israel na palastina tangu mwaka 2000-wengi wao ni wapalastina.






►◄