1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Mashariki ya kati

Hamidou, Oumilkher11 Machi 2008

Uamuzi wa seerikali ya Israel wa kujenga makaazi zaidi ya wahamiaji wa kiyahudi wakosolewa na Marekani

https://p.dw.com/p/DMUM
Matumizi ya nguvu yapamba moto GazaPicha: AP


Israel imekubali kutoishambulia Gaza ikiwa hujuma za makombora ya wapalastina dhidi ya ardhi yake zitasita.Habari hizo zimethibitishwa hii leo na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa serikali ya Israel.


Israel imeihakikishia msimamo huo Misri inayosimamia juhudi za upatanishi kati yake na wapalastina kwa lengo la kufikia makubaliano ya kusitisha matumizi ya nguvu.Afisa wa ngazi ya juu wa wizara ya ulinzi ya Israel amesema tunanukuu:Israel imefikia makubaliano pamoja na Misri ambapo inaahidi kujizuwia kushambulia Gaza kwa wakati wote ambao makombora ya Kassam hayatafyetuliwa dhidi ya ardhi yake."Mwisho wa kumnukuu afisa huyo wa wizara ya ulinzi ya Israel ambae hakutaka jina lake litajwe.


Majadiliano ya kusaka makubaliano ya kuweka chini silaha yanafanyika kutokana na juhudi za Misri,katika wakati ambapo Israel inapinga kuzungumza na Hamas inayowalinganisha na kundi la magaidi nae kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina mahmoud Abbas akiwa amevunja maingiliano yote pamoja na kundi hilo la itikadi kali,tangu walipotwaa madaraka huko Gaza mwezi June mwaka jana.


Wakati huo huo mpango wa Israel wa kujenga makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za wapalastina umekosolewa na Marekani.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice akizungumuza na waziri mwenzake wa Israel Tzipi Livni mjini Washington,ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa na kuheshimiwa utaratibu mpya wa amani ya mashariki ya kati.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amesema kuheshimiwa makubaliano mepya ya amani ni sehemu ya utaratibu wa Annapolis,akimaanisha mazungumzo yaliyoanzishwa November iliyopita mjini Annapolis karibu na Washington kati ya wa-Israel na wapalastina.


Wakati wa mazungumzo hayo Israel iliahidi kusitisha ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi katika ardhi za wapalastina ili kuepukana na balaa la kukorofisha mazungumzo na hasa kuhusu mipaka ya taifa la siku za mbele la wapalastina.


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice hakuikosoa moja kwa moja Israel kwa kuamua jumapili iliyopita kujenga nyumba mia kadhaa za wahamiaji wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi.Alikua lakini msemaji wake Sean McCormack aliyesema tangazo la serikali ya Israel halisaidii kuimarisha utaratibu wa amani.


Mpatanishi wa Palastina katika mazungumzo ya amani pamoja na Israel Saeb Erakat anasema:


"Tunalaani uamuzi wa serikali ya Israel wa kujenga mamia ya nyumba karibu na Jerusalem.Tunaamini hilo ni jaribio la kutaka kufuja utaratibu wa amani na kukorofisha mazungumzo kuhusu Jerusalem hata kabla hayajaanza.Ni sawa na kutaka kuyawekea vizingiti mazungumzo hayo."


Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice anafuatilizia sana mazungumzo kati ya Israel na wapalastina na anajihusisha moja kwa moja na juhudi za kusitisha mataumizi ya nguvu kati ya pande hizi mbili.


►◄