1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou5 Machi 2009

Risasi zinafyetuliwa upya ,muda mfupi baada ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani kumaliza ziara yake

https://p.dw.com/p/H6GE
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alipokutana na rais Shimon Peres wa IsraelPicha: AP



Madege ya kivita ya Israel yamehujumu Gaza hii leo na kuwauwa wanaharakati wanne wa kipalastina,saa chache tuu baada ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton kumaliza ziara yake ya mashariki ya kati yenye lengo la kuufufua autaratibu wa amani.


Shambulio la angani dhidi ya kambi ya wakimbizi ya Maghazi,katika eneo la kati la Gaza,limegharimu maisha ya wanaharakati watatu na kuwajeruhi wengine wawili hii leo.


Msemaji wa jeshi amesema shambulio hilo limelengwa kundi lililofyetua kombora dhidi ya kikosi cha wanajeshi wa Israel waliokua upande wa pili wa mpaka.


Jana usiku,hujuma za madege ya kivita ya Israel ziligharimu maisha ya mkuu wa tawi la kijeshi la Jihad aliyekua njiani karibu na kambi ya wakimbizi ya Jabaliya.


Kundi hilo la itikadi kali liliahidi litalipiza kisasi na hii leo wanaharakati wake wakafyetua makombora matatu dhidi ya Israel.Hakuna hasara iliyopatikana.


Mashambulio haya yameripuka saa chache baada ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton kumaliza ziara yake ya kwanza Mashariki ya kati.


"Marekani inadhamiria kubuni hali itakayopelekea kuundwa dola ya Palastina".Alisema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani baada ya mazungumzo pamoja na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas huko Ramallah.


Aliitolea mwito Israel iruhusu misaada zaidi iingie Gaza iliyoteketezwa kwa vita viliovyoanzishwa na Israel tangu December 27 mwaka jana."Tunataka misaada ya kiutu iingie Gaza kwa viwango vya kutosha ili kuwapunguzia usumbufu wakaazi wa Gaza."Alisistiza bibi Hillary Clinton aliyekosoa mipango ya Israel ya kuruhusu majumba ya waisrael yajengwe katika sehemu ya mashariki ya mji wa Jerusalem.



Mjini Washington kwenyewe,mwenyekiti wa kamisheni ya mambo ya nchi za nje ya baraza la senet,John Kerry,aliyekua ziarani hivi karibuni mashariki ya kati,amesema rais Bashar Al Assad amemhakikishia ,nchi yake Syria iko tayari kuanza mazungumza ya amani pamoja na Israel.


Na Uengereza inasema  itakua tayari kuzungumza ana kwa ana na tawi la kisiasa la Hisbollah baada ya kujiunga na serikali ya umoja wa taifa nchini Libnan.