1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya raia wa Iraq ni tete

Thelma Mwadzaya30 Julai 2007

Takriban raia milioni 8 wa Iraq wanahitaji msaada wa dharura kwasababu ya vita nchini humo.Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la misaada la Uingereza Oxfam na kamati ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Iraq.Wairaqi hao wanahitaji msaada wa maji safi,huduma za usafi,chakula na malazi.

https://p.dw.com/p/CHjx
wanawake nchini Iraq
wanawake nchini IraqPicha: DW

Ripoti hiyo inaongeza kuwa zaidi ya watu milioni 2 wengi wao wanawake na watoto wameachwa bila makao huku wengine kulazimika kuwa wakimbizi katika nchi jirani za Syria na Jordan.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Iraq inaeleza kuwa serikali ya nchini hiyo inashindwa kutoa huduma za msingi za maji,usafi,chakula na malazi kwa yapata watu milioni 8.

Kwa upande mwingine inaonya kuwa ongezeko la ghasia linaziba matatizo ya kibinadamu yanayosababishwa na vita tangu mwaka 2003.Wairaqi milioni 2 wameachwa bila makao nchini mwao huku wengine milioni 2 kutoroka nchi za jirani.

Utafiti huo unatambua kwamba vita ndio chanzo kikubwa cha matatizo ya Wairaqi ila magonjwa na utapia mlo ni vitisho vikubwa kwa wakazi hao.

Kwa mujibu wa utafiti huo asilimia 70 ya wakazi wote wa Iraq hawana maji safi ya kutosha ikilinganishwa na asilimia 50 kabla ya vita kuanza.

Takriban asilimia 30 ya watoto wana utapia mlo kiwango ambacho kimeongezeka katika kipindi cha miaka mine iliyopita.Asilimia 15 ya waIraqi hawawezi kumudu mahitaji ya chakula.

Kulingana na mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Oxfam Jeremy Hobbs serikali ya Iraq na jamii ya kimataifa zinapaswa kutia juhudi zaidi ili kutimiza mahitaji ya wakazi wa Iraq.

Shirika la Oxfam lilisitisha huduma za msaada nchini Iraq kwasababu ya usalama duni tangu vita kuanza mwaka 2003.Mashirika mengine yasiyo ya kiserikali nchini humo yanajitahidi kutoa misaada kwa raia wa Iraqi ila yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha.Baadhi yao yanaogopa kuchukua msaada kutoka mataifa yanayochangia majeshi yao nchini Iraq kwa sababu za kiusalama.Shirika la Oxfam kwa upande wake linatoa wito kwa mataifa ambayo hayajapeleka vikosi vyao kulinda amani nchini Iraq kutoa misaada zaidi.

Wengi ya wakimbizi hao wako katika nchi jirani za Jordan na Syria wakiwa wataalam wanaoacha nchi yao katika hali tete.

Serikali ya Nuri al Maliki inapaswa kugawanya jukumu la usambazaji msaada kwa mashirika ya misaada,kuimarisha sheria ili kuwezesha mashirika ya kisheria kutimiza wajibu wao aidha kuongeza maradufu kiwango cha msaada kwa kila familia hadi dola 200.

Serikali za mataifa ya kigeni zinapaswa kutoa misaada ya kiufundi na fedha ili kutekeleza sera hizo aidha kutoa huduma za msingi.