1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya tahadhari ingalipo Munich

1 Januari 2016

Hali ya tahadhari bado ni kubwa katika mji wa kusini wa Munich nchini Ujerumani baada ya vituo viwili vya reli kufungwa wakati wa usiku kwa kuhofia mashambulizi ya kigaidi wakati wa mkesha mwa mwaka mpya.

https://p.dw.com/p/1HWuq
München - Terrorwarnung

Mkuu wa polisi wa Munich Hubertus Andrae akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa (01.01.2015) amesema "kwa sasa bado wanausalama wa ziada 1,000 wako kazini."

Polisi wamemwagwa katikati ya mji huo na katika viuo viwili vya treni kikiwemo kituo kikuu ambavyo ilibidi kufungwa saa za mwisho mwisho za mwaka 2015 baada ya polisi kutowa onyo la shambulio la kigaidi kwa kuzingatia dokezo la shirika la ujasusi la kigeni.

Taarifa kamili juu ya tishio hilo na watu wanaohusika bado haziko wazi lakini duru moja ya ujasusi imewataja watu waliopanga mashambulizi ni watano hadi saba na wanatokea Syria na Iraq wakiwa na mafungamano na kundi la Dola la Kiislamu.

Data zimechunguzwa

Hata hivyo Andrae amewaambia waandishi wa habari kwamba wamezichunguza data kuhusiana na majina ya watu hao lakini hadi sasa hawajuwi iwapo majina hayo ni sahihi, iwapo watu hao wako kweli na wako wapi.

Waziri wa Mambo ya ndani jimbo la Bayern Bayern Joachim Herrmann (kulia) na Mkuu wa polisi wa Munich Hubertus Andräe
Waziri wa Mambo ya ndani jimbo la Bayern Bayern Joachim Herrmann (kulia) na Mkuu wa polisi wa Munich Hubertus AndräePicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Saa moja na ushee kabla ya kuingia mwaka mpya polisi iliamuru kuondolewa kwa watu kutoka vituo hivyo viwili vya treni kutokana na uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi na kutowa tahadhari kwenye mtandao wa Twitter kwa lugha mbali mbali.

Huduma za usafiri katika vituo hivyo zikasitishwa mara moja na wananchi walitakiwa kuepuka mikusanyiko mikubwa baadae vituo hivyo vikafunguliwa tena lakini polisi ikatowa wito kwa wananchi kuwa macho.

Polisi wengine wakiwa wamevalia mavazi ya kuzuwiya fujo waliwekwa kwenye milango ya vituo hivyo na wasafiri waliokuwa wakitaka kuingia kwenye vituo hivyo walirudishwa.

Hofu ingalipo

Maafisa usalama wa Ujerumani wanaamini kwamba watu kadhaa wameingia Ujerumani kati ya mwezi wa Oktoba na Novemba wakisafiri kwa kutumia paspoti za Syria nambari za pasi hizo zikiwa sawa na zile zinazomilikiwa na Kundi la Dola la Kiislamu.

Kituo kikuu cha reli Munich.
Kituo kikuu cha reli Munich.Picha: Reuters

Mmiliki mmoja wa mkahawa mjini humo ameliambia shirika la habari la dpa kwamba "uwezekano wa kufanyika shambulio umezidi kuongezeka kwa sababi hivi sasa Ujerumani imejihusisha katika vita." akimaanisha uamuzi wa Ujerumani wa hivi karibuni kutowa vikosi vyake na msaada mwengine wa kijeshi kwa muungano unaopambana na Kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria.Ameongeza kusema ni "suala la mahala gani kutafanyika shambulio hilo."

Miji mikuu ya Ulaya imekuwa katika hali kubwa ya tahadhari tokea mwezi wa Novemba wakati wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu walipouwa watu 130 katika mashambulio ya risasi na kujitowa muhanga mjini Paris na kuzusha hofu kwamba wanaweza kufanya mashambulizi mengine wakati wa shamra shamra za Krismasi na Mwaka Mpya.

Barani kote Ulaya sherehe za hadharani ziliendelea kufanyika kama zilivyopangwa lakini chini ya ulinzi mkali wa maelfu ya polisi na vikosi vya usalama.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : Yusra Buwayhid