1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya uwekezaji nchini Rwanda yatikisika kabla ya uchaguzi.

5 Agosti 2010

Ingawa Rwanda inakosolewa kwa uongozi usiokuwa wa kidemokrasia, inasifiwa sana kwa uwajibikaji wake.

https://p.dw.com/p/Ockp
Rais Kagame anayesifiwa na mataifa ya magharibi kwa kuinua uchumi wa taifa hilo tangu mauaji ya halaiki ya 1994.Picha: picture-alliance/dpa

Hali ya uwekezaji nchini Rwanda muda huu kabla ya uchaguzi mkuu unaonekana kutikisika kwa kiasi fulani. Suala kuu linaojitokeza ni ikiwa Rais wa taifa hilo, Paul Kagame anaweza kukabiliana na pingamizi zilizopo bila ya kusababisha athari kubwa ya ufadhili na kiuchumi na ikiwa mchango wake unaweza kusababisha hatari ya uwekezaji wa muda mrefu.

Rais Kagame amekuwa akisifiwa na nchi za magharibi na wafadhili kwa kulijenga taifa hilo baada ya mauaji ya halaiki ya mwaka wa 1994. Bw Kagame pia anapanga mkakati wa kuliondoa taifa hilo lenye idadi ya raia milioni 10 kutotegemea tu kilimo hasa upanzi wa chai na kahawa na kulibadilisha liwe kitovu cha mawasiliano na teknolojia.

Thomas Vis afisa wa ngazi juu katika benki ya dunia, amesema nia ya uwekezaji nchini Rwanda bado inaongezeka hasa katika sekta ya miundo mbinu na kilimo.

Hata hivyo wakosoaji na mashirika ya kutetea haki yanasema rais huyo anaendelea kuwa mbabe na yanauliza masuali kuhusu kuuawa kwa mwanasiasa wa upinzani, kufyatuliwa risasi kwa jenerali muasi anayeishi Afrika kusini, kuuawa kwa mwandishi habari na kukamatwa kwa vigogo wa upinzani. Serikali ya Rwanda imekanusha kuhusika kwake.

Wachunguzi wengine wanasema Rais huyo amekuwa akichukua hatua kutokana na changamoto kutoka kwa viongozi wakuu ingawa wachache wanashuku kwamba atashinda katika uchaguzi mkuu wa tarehe tisa kwa urahisi. Vyama kadhaa vya upinzani vimeshindwa kushiriki.

Licha ya hayo, wawekezaji waliodhani kwamba rais Kagame atabakia madarakani sasa wanashangaa zaidi kuhusu hali ya siku zijazo.

Mataifa mengi yakiwemo yale ya magharibi yanapendelea aendelee kuongoza. Laura Morrison, mtafiti wa masuala ya udhibiti wa hatari, anasema haieleweki kabisa ni nani anayeweza kuchukua nafasi yake ikiwa ataondolewa na wawekezaji wengi wana imani sana naye.

Flash-Galerie Ruanda Versöhnung Bild 5
Sehemu ya mji mkuu wa Rwanda, Kigali. Taifa hilo lina idadi ya raia milioni 10.Picha: James Nzibavuga

Rwanda sio taifa la pekee la Kiafrika ambalo limekuwa likisifiwa na magharibi na ambalo linaonekana kuanza kuegemea upande wa uongozi wa kiimla. Wachunguzi wengine wamekuwa wakizitaja Uganda na Ethiopia kama mifano mingine.

Thomas Cargill, kiongozi wa kitengo cha masualamya Afrika katika shirika la utafiti ya Chartham, alisema haiwezekani kupuuza hatua zilizopigwa kuhusiana na utawala barani Afrika katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita. Alisema kwamba imani ya uwekezaji imeongezeka na kuwa kinachoendela sasa sio tu kuhusiana na uongozi wa kiimla bali kuna ujasiri zaidi katika mataifa ya Kiafrika wa kuiambia magharibi kwamba Afrika inaweza kutekeleza mipango yao kwa njia yao.

Rwanda imekuwa ikisifiwa pia kwa kupiga hatua katika vita dhidi ya rushwa na kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ilipigiwa kura na benki ya dunia kama taifa lililoimarika kibiashara kote duniani. Na ingawa inatajwa na wachunguzi kwamba nchi hiyo haina demokrasia thabiti, ina uwajibikaji wa hali ya juu.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters

Mhariri, Sekione Kitojo