1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya wasiwasi mjini Nairobi

1 Oktoba 2012

Hali ya wasi wasi yazuka katika mji mkuu wa Kenya Nairobi kufuatia shambulio la bomu katika kanisa liliouwa mtoto mmoja na kujeruhi wengine kadhaa na kusababisha ghasia za kulipiza kisasi dhidi ya jamii ya Wasomali

https://p.dw.com/p/16I3H
NAIROBI, Sept. 30, 2012 Police guard at the site of a grenade blast at St. Polycarp Church along Juja road in Nairobi, Kenya. Sept. 30, 2012. Suspected terrorists threw a grenade inside the St. Polycarp Church in Kenya's capital Nairobi on Sunday, leaving at least one child killed and three people injured, police confirmed
Kenia Nairobi Anschlag auf KirchePicha: picture-alliance/Zuma Press

Makoti ya watoto na viatu vilivyorowa damu vilikuwa vimetapakaa kwenye sakafu ya kanisa la Anglikana la Mtakatifu Polycarp. Mkuu wa polisi wa jiji la Nairobi Moses Nyakwama ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mtoto mmoja ameuwawa na wengine watatu walijeruhiwa vibaya na kwamba wanashuku shambulio hilo limefanywa na watu wanaoliunga mkono kundi la Al Shabaab.

Amesema hiyo ni mikiki ya mfa maji ambaye hawachi kutapatapa na kwamba hivi karibuni polisi ya Kenya imewakamata watuhumiwa kadhaa kuhusiana na maguruneti. Janet Wanja aliyeshuhudia tukio hilo amesema alikuwa ndio kwanza anaingia kanisani katika kanisa hilo lilioko eneo la Pangani wakati mripuko ulipolitingisha jengo la kanisa.

Amesema "Nimesikia sauti kubwa ya mripuko na baadae vilio vya watoto, nilichanganyikiwa kwa kile nilichokishuhudia, watoto wakiwa na majeraha na damu ikiwa imetapakaa kila mahala".Wanja anauliza kwa nini wanashambulia kanisa?

Hali ilivyo baada ya mripuko kanisani
Hali ilivyo baada ya mripuko kanisaniPicha: picture-alliance/Zuma Press

Wilfred Mbithi mkuu wa operesheni za polisi mjini Nairobi amekaririwa akisema baadhi ya mashahidi wamewaambia kwamba waliwaona wanaume wawili wenye asili ya Kisomali wakikimbilia nyuma ya kanisa ambapo ndiko kulikotokea mripuko huo. Wakati ikutuhumiwa kwamba watu hao ndio waliolirusha guruneti hilo kanisani,polisi pia inachunguza uwezekano kwamba mripuko huo umesababishwa na bomu ambalo lilikuwa limetegwa kanisani humo na mapema.

Afisa wa kanisa Livingstone Muiruri amesema watoto tisa wamejeruhiwa katika mripuko huo na kwamba watoto waliokuwa wakihudhuria misa walikuwa na umri wa kati ya miaka sita na kumi. Baada ya shambulio hilo watu wenye hasira wanaofikia 100 waliwavurumishia mawe Wasomali,majengo na magari yanayomilikiwa na jamii hiyo lakini hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa katika purukushani hizo zilizotokea katika kiunga cha Pangani.

Polisi ya Kenya iliwatawanya watu hao wakati Wasomali wakikimbilia usalama wao kwa kujifungia majumbani mwao.

Pangani imepakana na mtaa wa Eastleigh uliopachikwa jina la "Mogadishu ndogo" kutokana na wakaazi wake wengi kuwa ni wakimbizi wa Somali au Wakenya wenye asili ya Somali. Baadae hapo jana polisi wawili wa Kenya waliuwawa kwa kupigwa risasi katika mji wa kaskazini wa Garissa ulioko karibu na mpaka na Somalia.

Herman Ndiemma naibu mkuu wa polisi wa mji wa Garissa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba polisi hao waliuwawa wakati walipokuwa wakielekea kwenye chuo cha ufundi ambapo walipangiwa kukilinda.Ndiema amesema wanashuku wafuasi wa kundi la Al Shabaab kuhusika na shambulio hilo na kwamba polisi imeimarisha usalama katika mji huo.

Majeshi ya Kenya nchini Somalia
Majeshi ya Kenya nchini SomaliaPicha: AP

Wakaazi wengi wa mji wa Garissa ni wale wenye asili ya Kisomali na mji huo uko kilomita 180 kutoka mpaka wa Kenya na Somalia.

Polisi nchini Kenya ilitowa onyo kwamba kuna hatari ya kufanyika mashambulizi baada ya vikosi vya Kenya kuongoza mashambulzi dhidi ya waasi wa Al Shabaab katika mji wa Kismayo nchini Somalia. Magazeti ya Kenya hapo jana yamesema polisi imegunduwa kifaa cha kutengenezea mabomu kwenye mkoba uliokuwemo kwenye basi lililokuwa limebeba abiria kutoka Garissa kwenda Nairobi hapo Ijumaa. Kwa mujibu wa magazeti hayo abiria wote 60 waliokuwemo ndani ya basi hilo wametiwa nguvuni baada ya kila mmoja kuukana mzigo huo.

Washambuliaji walifanya mashambulizi kwa kutumia bunduki na mabomu kwa makanisa mawili huko Garissa hapo mwezi wa Julai na kuuwa takriban watu 17.

Mwandishi:Mohamed Dahman/RTR

Mhariri:Yusuf Saumu