1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali yarudi kuwa shwari Lubero, Kongo

7 Januari 2016

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, unasema hali imerejea kuwa shwari kwenye eneo la Lubero, Kivu ya Kaskazini ambako waasi wa FDLR wa Rwanda wameripotiwa kuuwa watu 14 alfajiri ya leo.

https://p.dw.com/p/1HZsj
Kongo, Soldaten der FARDC
Picha: AFP/Getty Images/A. Wandimoyi

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa MONUSCO, Charles Bambara, kikosi cha uingiliaji kati cha Umoja wa Mataifa kimewasili leo katika kijiji cha Miriki, ambacho kimeripotiwa kushambuliwa na wapiganaji wa FDLR kutoka Rwanda, wanaojificha katika misitu ya maeneo hayo. Bambara amesema kikosi hicho kwa ushirikiano na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kimewahakikishia wakazi wa kijiji hicho usalama wao, na kwamba kwa sasa hali imerejea kuwa ya kawaida.

Mbali na watu 14 waliouawa na ambao miili yao imepatikana, watu wengine 8 wamejeruhiwa katika shambulio hilo, na wengine wawili wameripotiwa kuchukuliwa mateka na waasi wa FDLR.

Waasi hao kutoka Rwanda walikuwa walengwa wa operesheni ya Umoja wa Mataifa baada ya nyingine iliyolisambaratisha kundi lililojulikana kama M23, lakini juhudi za pamoja kati ya MONUSCO na jeshi la Kongo dhidi yao zilisitishwa mwezi Januari mwaka jana, kutokana na tofauti zilizoibuka kati ya pande hizo. Hata hivyo, msemaji wa MONUSCO, anasema sasa tofauti hizo zimetatuliwa na operesheni za pamoja zitaanza muda wowote, na amethibitisha kwamba bado FDLR ni kitisho katika maeneo ya Lubero.

''Bado kuna wanamgambo wa FDLR mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ni vigumu kujua kwa uhakika idadi yao na kufuatilia mienendo yao kwa sababu hilo ni eneo lenye pori kubwa, lakini ni ukweli kwamba katika eneo la Lubero yalikotokea mashambulizi ya leo, wapo wapiganaji wa FDLR' amesema msemaji wa MONUSCO, Charles Bambara

Msemaji wa jeshi la Kongo Mak Hazukay ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wapiganaji wa FDLR walijipenyeza nyuma ya ngome za jeshi hilo na kuweza kuwashambulia raia wakitumia visu na mapanga. Mkuu wa kijiji cha Mariki kilichoshambuliwa Gervais Paluku Murandia amesema wake zake wawili na binti yake mkubwa ni miongoni mwa waliouawa.

Mtetezo mmoja wa haki za binadamu katika eneo lililoathirika Soulaymane Mokili, amesema ameona mwenyewe baadhi ya maiti za waliouawa, zikiwa na majeraha ya visu na risasi.

Beni Demokratische Republik Kongo Blauhelmsoldaten 23.10.2014
Picha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

'Shambulio limefanywa mapema asubuhi, naweza kusema lilikuwa shambulio la kushtukiza dhidi ya raia wasio na hatia. Naweza kuhakikisha kwamba operesheni ya pamoja kati ya MONUSCO na jeshi la Kongo inaendelea kujaribu kuwasaka wahalifu hao waliowashambulia raia. Tunajaribu kuwatafuta ili kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria, ' amesema Bambara

Hii sio mara ya kwanza kwa waasi hao wa FDLR kulishambulia eneo la Lubero. Mwezi Oktoba mwaka jana waliwauwa watu watatu kwa kuwachoma visu katika eneo hilo linalokaliwa na watu wa jamii ya wanande.

Duru kutoka eneo hilo zinahusisha mashambulizi hayo na hatua ya viongozi wa wanande kuwakatalia wahutu wa Kongo kurudi katika makazi yao ndani ya eneo hilo, ambao wanawatuhumu kutaka kuliteka eneo lao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre/Interview

Mhariri: Mohammed Khelef