1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali yazidi kuwa mbaya Syria huku wajumbe wa jumuiya ya Kiarabu wakitarajiwa nchini humo leo

21 Desemba 2011

Mapigano makali yanaendelea katika mkoa wa kaskazini mwa Syria Idlib, huku wanaharakati wakisema takriban watu 111 wameuwawa muda mfupi tu kabla ya mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu wa kumaliza miezi tisa ya umwagaji damu.

https://p.dw.com/p/13Wx0
Waandamanji katika mji wa Homs, nchini Syria.
Waandamanji katika mji wa Homs, nchini Syria.Picha: Sham News Network/dapd

Shirika la kutetea haki za binaadamu lenye makao yake nchini Uingereza la Syrian Observatory for Human Rights, limetoa takwimu hizo mpya za vifo kupitia taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP, siku moja tu baada ya kuripoti vifo vya raia 37 pamoja na takriban wanajeshi 100 walioiasi serikali katika mkoa huo wa Idlib.

Ghasia hizo ni mojawapo ya machafuko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu mashambulizi ya kijeshi katika mji wa kati wa Hama kuwauwa watu 139 mwishoni mwa mwezi Julai.

Ripoti hiyo inajiri kabla ya kuwasili nchini humo kwa kundi maalum la maafisa wa nchi za Kiarabu ili kuandaa mazingira ya maafisa wanaotathmini utekelezaji wa mkataba wa jumuiya ya Kiarabu, wenye lengo la kukomesha umwagaji damu.

Idlib, ambao ni mkoa wa kaskazini mwa Syria unaopakana na Uturuki, umeshuhudia makabiliano makali katika siku za hivi karibuni. Kundi la uchunguzi wa visa vya ukiukaji wa haki za binadam lilisema wanajeshi walio watiifu kwa rais Bashar Al Assad waliwamininia risasi wanajeshi walioiasi serikali katika kambi yao siku ya jumatau, na kuwauwa 60 kati yao, na likasema waasi wameharibu magari 17 ya kijeshi tangu jumapili.

Katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu Nabil Elaraby ameliambia shirika la habari la Reuters mjini Cairo kuwa kundi la maafisa wa jumuiya hiyo litawasili Syria hii leo huku wachunguzi wengine 150 wakitarajiwa kuwasili nchini humo mwishoni mwa mwezi huu. Amesema huo ni ujumbe mpya na kwamba italingana na utekelezaji wa nia njema.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria Walid Al Mualimm ameelezea matumaini yake kuhusu ujumbne huo wa Jumuiya ya Kiarabu. Kabla ya kusaini mwafaka siku ya jumatatu wa kuwakubalia wachunguzi watakaotathmini utekelezaji wa mpango wa jumuiya ya Kiarabu wa kumaliza ghasia hizo, kuondoka kwa wanajeshi mitaani, kuwachiliwa huru wafungwa pamoja na kuwepo kwa mazungumzo na upinzani.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-Moallem
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-MoallemPicha: dapd

Wanaharakati wa demokrasia nchini Syria wana wasiwasi kuhusu kujitolea kwa Assad katika mpango huo, ambao ikiwa utatekelezwa, unaweza kuwapa nguvu waandamanaji wanaotaka kumalizika kwa utawala wake wa miaka 11.

Umoja wa mataifa umesema zaidi ya watu 5,000 wameuwawa nchini Syria tangu maandamano ya kumpinga rais Assad yalipoanza mwezi Machi, baada ya kuchochewa na wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu. Wiki chache zilizopita serikali ya Syria ilisema wanachama wake 1,100 wa vikosi vya usalama waliuwawa na makundi yaliyojihami ya kigaidi.

Syria ilikubali mpango wa amani ulioundwa na nchi za Kiarabu, mapema mwezi jana, lakini ghasia zikaendelea hali iliyozifanya nchi za kiarabu kutangaza vikwazo vya kifedha na marufuku ya kusafiri dhidi ya maafisa wa Syria.

Marekani na Umoja wa Ulaya zimeiwekea Syria vikwazo ambavyo sambamba na ghasia zinazoshuhudiwa nchini humo, vimeufanya uchumi kuzorota kwa kiwango kikubwa.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed