1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas latoa wito wa kupinga Israel na kutaka mageuzi

Amina Abubakar7 Desemba 2017

Kundi lenye nguvu Palestina la Hamas limetoa wito wa kuanzishwa harakati za kupinga na kutaka mageuzi dhidi ya Israel baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wa Israel

https://p.dw.com/p/2ovCF
Gaza - Reaktion auf Jerusalem-Status von Hamas Chef Ismail Haniyeh
Picha: Reuters/M. Salem

Kundi lenye nguvu Palestina la msimamo mkali la Hamas limetoa wito wa kuanzishwa harakati za kupinga na kutaka mageuzi dhidi ya Israel baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wa Israel huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likitarajiwa kukutana hapo kesho katika kikao cha dharura kuzungumzia uamuzi wa Rais Trump. 

"Tunapaswa kuitisha kilio cha ghadabu kupambana na maadui wayahudi” alisema kiongozi wa kundi la Hamas linaloudhibiti ukanda wa Gaza Ismail Haniyeh, katika hotuba yake hii leo baada ya tangazo la rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel. Amesema sera ya wayahudi iliyoungwa mkono na Marekani haiwezi kukabiliwa isipokuwa kwa harakati za mapambano ya Intifada kuanzia hapo kesho huku akiongeza kuwa tamko la Trump ni tamko la Vita. 

"Nathibitisha kwamba Jerusalem imeungana, sio Mashariki wala Magharibi na itabakia kuwa mji mkuu wa Palestina, Palestina yote," alisema Haniyeh.

Rais Donald Trump wa Marekani na makamu wake Mike Pence
Rais Donald Trump wa Marekani na makamu wake Mike PencePicha: Reuters/K. Lamarque

Hamas: Wapalestina wana haki ya kutumia njia yoyote ya kuelezea hasira zao

Kiongozi mwengine wa kundi la Hamas Ismael Radwan, amesema Wapalestina wana haki ya kutumia njia yoyote ya kuelezea hasira zao dhidi ya uamuzi wa Trump. Ismael ameongeza kuwa "Watu wa Palestina wanasiasa pamoja na makundi yote ya vuguvugu la kitaifa wanapinga uamuzi wa Donald Trump tunasema uamuzi huo ni uchokozi dhidi ya watu wetu taifa letu na maeneo yetu matakatifu ya kuabudu."

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Nentanyahu amesema nchi nyingi zitafuata mkondo wa Marekani kwa kuitambua jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kwamba mawasiliano tayari yameanza kufanyika.

Akizungumza katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Israel Netanyahu hakuzitaja nchi zozote lakini akadokeza kuwa nchi zinazofuata mkondo wa Marekani huenda zikahamisha balozi zake kutoka Telaviv hadi mjini Jerusalem hata kabla ya Marekani kufanya hivyo ambapo serikali ya rais Trump imesema hilo huenda likachukua miaka kadhaa. 

Viongozi watoa hisia zao

Huku hayo yakiarifiwa viongozi wa dunia wameendelea kutoa hisia zao na kuonyesha ghadhabu juu ya uamuzi wa rais Donald trump kuitambua Jerusalem kama mji Mkuu wa Israel. rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameikaripia Marekani kwa kusema kwamba hatua yake italiweka eneo la Mashariki ya kati katika mduara wa moto.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/R. Zvulun

Akizungumza katika hotuba yake kabla ya kuelekea ziarani nchini Ugiriki Rais Erdogan amesema: "Hakuna nchi duniani kando na Marekani na Israel iliyochukua hatua dhidi ya azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1980. ni nchi hizo mbili tu zilizopinga. ni vigumu kuelewa ni nani bwana Trump anayetaka kumridhisha kwa kufufua hili tena."

Uturuki inatarajia kuitisha mkutano wa viongozi wa jumuiya ya nchi za kiislamu OIC siku ya Jumatano wiki Ijayo kujadili uamuzi wa Trump. Uturuki ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

Kauli ya Saudi Arabia

Kwengineko msemaji wa serikali ya Saudi Arabia amesema nchi yake haiungi mkono uamuzi huo kwa sababu hali ya mjini Jerusalem haipaswi kuamuliwa na mataifa mawili pekee. Rais wa Lebanon amesema mustakabali wa Jerusalem hauwezi kuamuliwa na raisi au taifa moja. Indonesia pia imetoa sauti yake na kumtaka Trump kubatilisha uamuzi wake.

Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema matarajio ya pande zote zinapaswa kuzingatiwa kwa mazungumzo ili kupata muafaka wa hali ya Jerusalem, huku Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akisema hawakubaliani hata kidogo na uamuzi wa Marekani wa kuhamisha ubalozi wake mjini Jerusalem na kuutambua mji huo kama mji mkuu wa Israel.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters/AP/dpa

Mhariri Yusuf Saumu