1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas na Fatah waanza kukutana huko Misri

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP26 Februari 2009

Vyama vya Hamas na Fatah vimeanza mkutano wao katika mji mkuu wa Misri Cairo, chini ya upatanishi wa Misri katika mpango wa kumaliza uhasama wao , ili kuweza mazingira ya kuundwa kwa serikali ya umoja

https://p.dw.com/p/H1aC
Wafuasi wa Fatah katika moja ya maandamano ya kupinga ghasia GazaPicha: AP

Mapema vyama hivyo vilikubaliana kutatua suala la majaaliwa ya wafungwa wa pande zote mbili, suala ambalo limekuwa kikwazo cha wao kufikia muafaka, pamoja na kuacha kutoleana kauli kali.


Wajumbe wa vyama hivyo viwili vya Hamas na Fatah wanakutana katika ofisi za mkuu wa shirika la ujasusi la Misri, Omar Sueiman, ambaye anasimamia upatanishi huo.

Matarajio ni makubwa kwamba huenda makundi hayo yakafikia maelewano na kutimiza masharti yaliyowekwa na jumuiya ya kimataifa kabla ya kupatiwa msaada wa mabilioni ya dola wakati wa mkutano wa kuchangisha fedha za kuijenga upya Gaza baada ya kuathiriwa na vita.


Mapema kabla ya kuanza kwa mkutano huo hii leo, maafisa wa ngazi ya juu wa vyama hivyo walikubaliana, kimsingi, masuala kadhaa, ambapo katika taarifa yao ya pamoja walisema kuwa wafungwa wa pande zote mbili wataachiwa huru wakati wa kuanza kwa majadiliano yao hii leo.


Afisa wa juu wa kundi la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza, Mahamoud Zahar, amesema kuwa wanachama wa kundi hilo wapatao 80 waliyokuwa wanashikiliwa katika magereza ya Fatah inayodhibiti Ukingo wa Magharibi wameachiwa , na kwamba kuna wanachama wengine 300 wa kundi hilo bado wanashikiliwa huko Ukingo wa Maggharibi.


Kwa upande wake Hamas imesema kuwa imeondoa amri ya kuwazuia majumbani wanachama kadhaa wa Fatah huko katika Ukanda wa Gaza.


Hamas na Fatah vimekuwa na uhasama kwa muda mrefu lakini uhasama huo ulifikia hatua mbaya June 2007 pale Hamas ilipochukua udhibiti wa eneo la Ukanda wa Gaza kwa kuwafurusha wapiganaji wa Fatah katika mapigano yaliyosababisha vifo vya raia wengi.


Misri ilianza juhudi za kuvipatanisha vyama hivyo Novemba mwaka jana, lakini Hamas ilijiondoa katika dakika za mwisho ikidai kuwa Fatah ilikuwa ikiendelea kuwakamata wanachama wake huko Ukingo wa Magharibi.


Hatua ya kuvipatanisha vyama hivyo na kuwepo kwa serikali ya Umoja ya Wapalestina imekuwa ikionekana kuwa ni hatua muhimu katika kufikiwa kwa amani ya Mashariki ya Kati.


Waziri Mkuu wa Sweden, Fredrik Reinfeldt, ambaye nchi yake itachukua kiti cha urais wa Umoja wa Ulaya Julai mwaka huu, ameelezea anaunga mkono hatua ya kupatanishwa makundi hayo ya Kipalestina, akisema kuwa ni muhimu katika mpango wa amani ya eneo la Mashariki ya Kati.


Alisema hayo mjini Stockholm baada ya kukutana na Rais wa mamlaka ya Palestina anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa, Mahamoud Abbas.


Mjini London kundi linalojumuisha wapatanishi wa zamani wa amani katika mizozo mbalimbali duniani, limeitaka jumuiya ya kimataifa kulishirikisha kundi la Hamas moja kwa moja katika mpango wa amani ya Mashariki ya Kati, likisema hiyo ndiyo njia pekee ya kufikia malengo hayo.


Kundi hilo linajumuisha Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Israel, Shlomo Ben-Ami, mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati, Alvaro de Soto, aliyekuwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Bosnia, Paddy Ashdown, na Waziri wa zamani wa Nje wa Australia ambaye alikuwa mpatanishi katika mzozo wa Cambodia, Gareth Evans.


Katika waraka wao wapatanishi hao wa zamani wa amani wameelezea matumaini yao kwa serikali mpya huko Marekani ya Rais Barack Obama kwamba itaongoza njia ya kuwepo kwa mkakati mpya wa kutafuta amani Mashariki ya Kati kwa msingi wa kukubaliana na hali halisi na siyo kwa mtizamo wa kiitikadi.

Marekani na Umoja wa Ulaya zimekataa kushirikiana na Hamas katika kutafuta amani ya eneo hilo, zikilitaka kwanza kundi hilo kutimiza masharti kadhaa moja likiwa ni kukubali haki ya kuwepo kwa taifa la Israel.