1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas waahidi kuendelea na mapambano

Oumilkher Hamidou15 Desemba 2009

Fatah waitathmini hotuba ya Ismael Haniya kuwa dhidi ya juhudi za Misri za kuleta suluhu kati yao

https://p.dw.com/p/L2X1
Wafuasi wa Hamas waadhimisha miaka 22 tangu chama chao kilipoundwaPicha: AP

Wafuasi wa Hamas wamezitumia sherehe za kuadhimisha miaka 22 tangu chama chao kilipoundwa kufuatia wimbi la kwanza la Intifada,kuzidisha shinikizo dhidi ya chama cha ukombozi wa Palastina-PLO kinachojiandaa kurefusha mhula wa Mahmoud Abbas kama rais wa utawala wa ndani bwa Palastina.

Maelfu kwa maelfu ya wafuasi wa Hamas,chama kinachodhiti hatamu za uongozi katika eneo la Gaza,baada ya kuvitimua vikosi hasimu vya Fatah, kinachoongozwa na Mahmoud Abbas,walishiriki katika mhadhara huo ambao haujawahi kushuhudiwa tangu Israel ilipolivamia eneo hilo mwaka mmoja uliopita.

Katika mkusanyiko huo Ismael Hanijya,ambae ndie anaeongoza Hamas katika eneo la Gaza ameshadidia msimamo wa chama chake ambao ni pamoja na kupinga kuachana na mapambano kwa mtutu wa bunduki na kuundwa taifa huru la Palastina katika ardhi ya Palastina kuanzia bahari ya kati hadi ukingo wa magharibi wa mto Jordan. Ismaerl Haniya amesema:

"Tunatamka kwa niaba ya umma wa Palastina;walioko nyumbani,wanaoishi kama wakimbizi na uhamishoni ,na kwa niaba ya umma wa ulimwengu wa kiarabu na kiislam,Vuguvugu la Hamas halitaachana kamwe na muongozo wa mapambano na Jihad,hadi umma wetu utakapojipatia uhuru wake,haki ya kurejea nyumbani na mamlaka yake,Inshaa Allah."

Ismael Hanijeh ,ambae chama chake hakiwakilishwi katika kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Palastina PLO,amepinga mapema dhamiri za chama hicho, za kurefusha wadhifa wa rais Mahmoud Abbas,kama kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina.Baraza kuu la chama cha ukombozi wa Palastina linakutana hii leo kupitisha uamuzi huo.

Palästinenser Präsident Mahmoud Abbas bei einer Sitzung des PLO Zentralkomitees West Bank Ramallah
Kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud AbbasPicha: AP

Taasisi hiyo muhimu ya chama cha ukombozi wa Palastina inatazamiwa pia kuunga mkono msimamo wa rais Mahmoud Abbas wa kupinga kurejea katika meza ya majadiliano ya amani pamoja na Israel bila ya kusitishwa moja kwa moja ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi.

Mswaada wa azimio wa baraza kuu la PLO,uliolifikia shirika la habari la Reuters,unazungumzia juu ya kuachiwa Mahmoud Abbas na utawala wa ndani wa Palastina waendelee na dhamana zao mhadi uchaguzi utakapoitishwa,pengine June 28 mwakani."

Miaka 22 tangu kilipoundwa,na miaka karibu minne tangu Israel ilipovihamisha vikosi vyake toka Gaza,na mwaka mmoja tangu Tsahal walipojaribu kuuvunja nguvu utawala wa Hamas,Haniya anasema msimamo wa chama chake cha itikadi kali uko vile vile.

Chama cha Fatah kimesema katika taarifa yake hotuba ya Ismael Haniya inabainisha azma ya kuzidisha mfarakano kati ya Hamas na Fatah pamoja na msimamo wake shupavu kupinga juhudi za Misri za kufikia suluhu kati ya makundi hayo mawili.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Reuters/AFP)

Mhariri:Abdul Rahman