1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas yakabidhi vivuko ukanda wa Gaza

1 Novemba 2017

Kundi la Kiislamu la Hamas limeanza kukabidhi udhibiti wa vivuko vya mpakani mwa ukanda wa Gaza kwa rais wa Palestina anayeungwa mkono na Marekani Mahmoud Abbas.

https://p.dw.com/p/2mqZj
Gazastreifen Hamas Übergabe Grenzverwaltung an Palästinenserbehörde
Picha: Reuters/I. A. Mustafa

Haya ni katika makubaliano yaliyosimamiwa na Misri yanayolenga kumaliza mfarakano wa ndani uliodumu kwa mwongo mmoja. Hatua hiyo imeashiria utekelezwaji thabiti wa makubaliano ya maridhiano ya Oktoba 11 ambayo Wapalestina wanataraji yatapunguza vikwazo vya kiuchumi kwa Gaza na kufanya kuwepo kwa majadiliano yatakayozaa matunda katika lengo lao la kuunda taifa lao huru.

Israel na Marekani lakini wana mashaka kuhusiana na makubaliano hayo ya Palestina, kutokana na kukataa kwa Hamas kusalimisha roketi zake na zana zengine, kwa kuzingatia kwamba kundi hilo limepigana vita vitatu na Israel tangu kuchukua udhibiti wa Gaza kutoka kwa Abbas mwaka 2007.

Walioshuhudia wanasema waajiriwa kutoka mamlaka ya Palestina waliingia katika vivuko vya Erez na Kerem Shalom katika mpaka wa Israel na kivuko cha Rafah katika mpaka wa Misri, wakati ambapo wenzao wa Hamas walikusanya vifaa vyao na kuondoka kwa malori.

Jambo la kihistoria limefanyika katika eneo hilo la Gaza

Huko Rafah, picha za Abbas na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi zilipamba  milango ya ukumbi wa pasi za usafiri na bendera za Palestina na Misri zilipepea katika eneo hilo.

Gazastreifen Hamas Übergabe Grenzverwaltung an Palästinenserbehörde
Wapalestina wakivunja jengo lililojengwa na Hamas katika mlango wa ukanda wa GazaPicha: Getty Images/AFP/T. Coex

Mkuu wa idara ya ushuru katika kivuko cha Rafah anayeifanyia kazi mamlaka ya Palestina Mohamad Hinawee amesema jambo la kihistoria limefanyika katika eneo hilo, "leo hii ni siku muhimu katika historia ya Palestina, mamlaka ya kisheria imeredi tena katika vivuko," alisema Hinawee, "Serikali ya umoja imerudi na sasa sisi ni serikali moja inayoongozwa na Mahmoud Abbas. Tunaishukuru Misri pia kwa juhudi zake kubwa," aliongeza Hinawee.

Kutokana na sababu za kiusalama Israel ina sheria kali katika masuala ya kuvuka kwa watu na bidhaa katika kivuko chake katika ukanda wa Gaza, na sheria hizi zinajumuisha marufuku ya kuuza bidhaa eneo hilo.

Misri ambayo hapo awali iliwahi kulishutumu kundi la Hamas kwa kusaidia uvamizi wa makundi ya Kiislamu katika rasi ya Sinai inayopakana na Gaza, imelifunga eneo kubwa la Rafah. Hamas inakanusha madai hayo na imeongeza ulinzi katika mpaka huo.

Hamas bado ina kundi la kijeshi

Maafisa wamearifu kuwa mawaziri katika serikali ya Abbas wameanza kufanya shughuli zao katika eneo la Gaza katika wiki chache zilizopita na Jumanne, walichukua udhibiti wa akaunti za mapato za vivuko vya Rafah na Kerem Shalom.

Gazastreifen Hamas Übergabe Grenzverwaltung an Palästinenserbehörde
Waziri wa Palestina Mufeed al-Husayna akitembea katika eneo la utoaji pasi la GazaPicha: Getty Images/AFP/T. Coex

Hamas ilikuwa inatumia mapato hayo ambayo ni kodi zilizotozwa wafanyabiashara na wasafiri, kama bajeti yake ya Gaza, kuwalipa mishahara wafanyakazi wake kati ya 40,000 na 50,000 ambao ilikuwa imewaajiri tangu mwaka 2007. Mishahara hiyo sasa italipwa na mamlaka ya Palestina chini ya makubaliano ya Cairo.

Hamas pia bado ina kundi la kijeshi ambalo wachambuzi wanasema lina wapiganaji wasiopungua 25,000 waliojihami. Bado kundi hilo linasalia kuwa nguvu kubwa kwenye eneo la Gaza, ambalo lina watu milioni mbili.

Mamlaka ya Palestina itaanza udhibiti wa vivuko vya Erem na Kerem Shalom mara moja na haya ni kulingana na maafisa, waliosema kuwa eneo la Rafah litasubiri mipango mingine ya usalama, kama kuweka kikosi kutoka kwa walinzi wa rais Abbas na kutoka Misri.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga