1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamburg katika hatari ya kushushwa daraja

20 Aprili 2015

Klabu inayoshikilia mkia katika msimamo wa Bundesliga Hamburg ina mechi tano pekee zilizosalia ili kuepuka kushushwa daraja, baada ya kichapo cha goli moja kwa sifuri dhidi ya Werder Bremen

https://p.dw.com/p/1FBDw
Fußball Bundesliga SV Werder Bremen vs. Hamburger SV
Picha: picture-alliance/dpa/C. Jaspersen

Hamburg sasa wameshindwa mechi zao tano za mwisho, huku wakipata tu pointi mbili katika mechi tisa. Ulikuwa mchuano wa kwanza wa kocha mpya Bruno Labbadia tangu alipotwikwa jukumu la kuokoa jahazi kama kocha wa nne wa Hamburg msimu huu. Alikuwa na haya ya kusema baada ya mpambano huo

Ikiwa timu pekee ambayo haijawahi kushushwa daraja kutoka Bundesliga, Hamburg ilinusurika kutimuliwa msimu uliopita baada ya kushinda mechi ya mchujo. Wakati huo huo, viongozi Bayern Munich wanakaribia kutwaa taji la tatu la Bundesliga baada ya ushindi uliowatoa jasho wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Hoffenheim, lakini Mlinda mlango Manuel Neuer anasema ulikuwa ushindi muhimu

Bayern huenda wakaanza sherehe za ubingwa wikendi ijayo baada ya nambari mbili Wolfsburg kuhitaji goli la kusawazisha katika dakika za mwisho mwisho lililofungwa na Kevin De Bruyne ili kutoka sare ya goli moja kwa moja na Schalke.

Baada ya sare ya kutofungana goli kati ya Borussia Moenchengladbach na Eintracht Frankfurt, Bayer Leverkusen iliichukua nafasi ya tatu ambayo ni tiketi ya moja kwa moja ya kucheza kandanda la Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuirarua Hanover magoli manne kwa sifuri.

Bundesliga Borussia Dortmund gegen SC Paderborn
Borussia walimpa kwaheri Kocha Jurgen Klopp kwa kupata ushindi wa nyumbaniPicha: Baron/Bongarts/Getty Images

Kwingineko, Borussia Dortmund walipata ushindi wa magoli matatu kwa sifuri katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Paderborn na kusonga hadi nafasi ya tisa. Ulikuwa mchuano wao wa kwanza tangu Jurgen Klopp alipotangaza kuwa ataondoka mwishoni mwa msimu.

Na wakati Wanaborussia wakimwambia kwaheri Klopp, pia wanajiandaa kumkaribisha mrithi wake. Thomas Tuchel ndiye aliyepewa jukumu na mabingwa hao mara nane wa Bundesliga, kuvaa viatu vya Klopp kuanzia Julai mosi. Lakini Tuchel ambaye amesaini mkataba wa miaka mitatu katika uwanja wa Signal Iduna Park, yuko tayari kuifufua klabu hiyo?

Kama tu Klopp, Tuchel mwenye umri wa miaka 41 alianzia kazi ya ukufunzi katika klabu ya Mainz lakini akaiweka klabu hiyo katika kiwango cha juu.

Japokuwa Bayern Munich na Borussia Dortmund zinatambulika kwa mchezo wa mashambulizi ya kasi katika miaka ya karibuni, Tuchel anadai kuwa mwanzilishi wa mfumo huo katika msimu wa kwanza wa Mainz katika Bundesliga.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu