1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamburg yaparamia kileleni mwa Bundesliga

31 Agosti 2009

Paolo Guerrero aikomea pekee mabao 2 katika lango la Cologne.

https://p.dw.com/p/JMZZ
Kocha wa Hamburg (Labbadia)Picha: AP

Katika Bundesliga-wingi wa Holland, Arjen Robben alipiga hodi mara 2 katika lango la mabingwa VFL Wolfsburg na kukaribishwa ndani na hivyo kuivua Bayern Munich na balaa jengine.

-Paolo Guerrero kutoka Peru nae amelifumania lango la FC Cologne mara 2 jana na kuitundika Hamburg kileleni mwa Bundesliga.

-Katika premier League,mabingwa Manchester United walitoka nyuma na kuiambia Arsenal "kutangulia si kufika".

-Huko Itali, mabingwa Inter Milan wamewateketeza mahasimu wao wa mtaani AC milan kwa mabao 4:0 wakati Cristiano Ronaldo ametia bao la penalty akivaa kwa mara ya kwanza jazi ya Real Madrid.

Ligi mashuhuri barani ulaya:

Katika Bundesliga, wingi wa Holland Arjen Robben akiichezea mara ya kwanza Bayern Munich, alilifumania lango la mabingwa Wolfsburg mara 2 kuchangia ushindi wa Munich wa mabao 3-0 dhidi ya mabingwa Wolfsburg.

Robben aliitwa uwanjani katika kipindi cha pili cha michezo ili kujaza pengo la Hamit Altintop wakati Munich ikiongoza kwa bao 1:0.Katika dakika ya 68 ya mchezo, Robben alipopokea pasi maridadi kutoka kwa mfaransa Franck Ribbery na kutia bao lake la kwanza kwa Bayern Munich. Dakika 12 baadae,Ribbery akamtunukia tena dimba na Robben akaupiga msumari wa 3 na wa mwisho katika jeneza la mabingwa Wolfsburg.Huo ukawa ushindi wa kwanza kabisa wa B.Munich msimu huu.Kocha wa Munich, mdachi Van Gaal akivuta pumzi kwa ushindi huo alisema:

"Naamini ushindi wetu ulistahiki na sasa tunaweza kuangalia zaidi mbele."

Katika changamoto ya jana usiku, mperu Paolo Guerrero nae alimuigiza mdachi Robben kwa mabao yake 2 katika lango la FC Cologne yaliochangia ushindi wa Hamburg wa mabao 3:1 ulioinasisha Cologne mkiani .

Mmorocco Adil Cihi alifyatua mkwaju mkali na maridadi kutoka mita 30 ulionasa katika wavu wa lango la Hamburg.Bao hilo lakini, halikutosha kuivua Cologne na balaa la pigo jengine kali katika Bundesliga.

Schalke ilikiona klichomtoa kanga manyoya mbele ya chipukizi Freiburg,kwani bao 1 la mkorea wa kusini Cha lilitosha kuwatundua kileleni mwa Ligi. Shukurani kwa mabao ya stefan Kiessling,Bayer Leverkusen nayo imebakia kileleni mwa bundesliga bega kwa bega na Hamburg.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza: mabingwa Manchester united walitoka nyuma na kuilaza Arsenal mabao 2-1 na sasa Manu imepanda hadi nafasi ya 4 ya ngazi ya Ligi.Lilikuwa bao walilotia wenyewe Arsenal lililowaponza. Mrusi Andriy Arshavin, alilifumania kwanza lango la Manchester kabla ya mkwaju wa penalty wa Wayne Rooney kufuta bao hilo.Lakini bao la kichwa katika lango la timu yake ya Arsenal,lilihakikisha ushindi wa Manchester united.Chelsea ilikandika Burnley mabao 3-0 wakati Tottenham Hotspur imeizaba Birmingham City 2-1.

Katika serie A, Ligi ya itali, mabingwa Inter Milan wamewakomoa mahasimu wao wa mtaani AC Milan kwa kuwachapa mabao 4 bila jibu.Juventus yadhihirika ndio itakayotoa tena changamoto kwa Inter msimu huu,kwani iliilaza Roma mabao 3-1.Mbrazil Diego aliehama Bundesliga,ndie alipachika pekee mabao 2.Fiorentina ilipiga kumbo Palermo kwa bao 1-0.

Ama katika La Liga-Ligi ya Spain,mchezaji wa mwaka wa dimba Cristiano Ronaldo akiichezea Real Madrid kwa mara ya kwanza alitia bao la ushindi la mkwaju wa penalty kufanya mabao 3-2 dhidi ya Deportivo La Coruna.Jana Valencia iliikomea Sevilla mabao 2:0. Malaga iliikumta Atletico Madrid kwa mabao 3:0.

Muandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Mhariri: M.Abdul Rahman