1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamburger SV

Ramadhan Ali1 Juni 2007

Klabu ya dimba ya Hamburg ni timu pekee kati ya zote za Bundesliga isowahi kuteremshwa daraja ya pili na msimu ujao itaendeleza mila hiyo. Klabu hii iliasisiwa lini na ilitamba miaka ipi katika dimba la ulaya na nyumbani ?

https://p.dw.com/p/CHc5

Hamburg au Hamburger SV ni mojawapo ya klabu za kale za Bundesliga-Ligi ya Ujerumani na ndio klabu pekee ya asilia ilioanzisha Bundesliga isiowahi kuteremshwa daraja ya pili tangu kuanzishwa Ligi hii 1963.

Historia ya Hamburg inaturudisha nyuma sana.Klabu hii iliundwa 1887 lakini kuna wanaodai kwamba mwaka hasa wa kuasisiwa Hamburger SV ni 1919.Inatokana na klabu 3 za dimba zilizojiunga pamoja kuunda Hamburger HSV –yaani SC Germania,FC Falke na HFC.

Mafanikio ya kwanza makubwa ya klabu hii ya kaskazini mwa Ujerumani hayakukawia :kwani 1922,Hamburg ilitawazwa mabingwa wa Ujerumani ingawa katika mpambano wa marudio ya finali kati yake na Nüremberg,hakuna alieibuka mshindi.Hamburg ikakataa kuvaa taji mwaka huo.Mwaka mmoja baadae lakini ,Hamburg ikatamba tena wazi na kutoroka na kombe la ubingwa na 1928 ikavaa tena taji.Taji la 3 lilibidi kungojewa kitambo kirefu.

1960 ndipo lilipowadia kwa Hamburg kuvaa taji tena.Kitu cha kukumbukwa katika ushindi wa mwaka huo ni kwamba,Hamburg ilicheza na wachezaji wote kutoka jiji lao-hakukuwa na mgeni.Miongoni mwao alikuwa chipukizi mmoja aliekuja kutamba baadae tangu katika Bundesliga hata katika Kombe la dunia la FIFA:Uwe Seeler.

Uwe sio tu akitia mambo mengi kuliko wachezaji wengine wa Hamburg,bali hadi hii leo amekuwa mtiifu kwa klabu hii-hakuihama.Kwani, kwa zaidi ya miongo 2 jina la Uwe Seeler likienda sambamba na Hamburger SV kama Beckenbauer na Bayern Munich.Katika uwanja wa Hamburg kuna sanamu la staid huyu mwenye umri wa miaka 70 hii leo likionesha mguu wake uliochongwa kwa shaba.

Palipo sanamu hilo pamegeuka kituo cha kupeana miadi.Kwani,ikiwa mashabiki wataka kuonana uwanjani huambiana tukutane katika Mguu wa Uwe Seeler.

Ni baada ya 1975 ndipo Hamburg ilipoanza kweli kuhanikiza katika dimba la Ujerumani.Kwani mara 2 kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani DFB Pokale lilienda Hamburg na walishinda pia kombe la washindi barani Ulaya kwa kuilaza RSC Anderlecht ya Ubelgiji.

Pale staid mwengine mashuhuri wa dimba la Ujerumani Günther Netzer aliposhika wadhifa wa umeneja wa klabu hii,kocha Branko Zebec aliongoza Hamburg kuvaa taji lake la 4 la ubingwa hapo 1979.Jogoo lao lakini wakati huo lilitoka Uingereza:Kevin Keeagan.

Stadi mwengine mkubwa aliefuata nyayo za Kevin Keeagan hadi mto Elbe kujiunga na Hamburg si mwengine bali Franz Beckenbauer.Aliporudi kutoka Cosmos New York,Beckenbauer,hakurudia moja kwa moja Münich bali Hamburg.

Aliichezea klabu hiyo hadi 1982 alipohetimisha maisha yake ya kucheza dimba,lakini hakuondoka huko bila ya kwanza kuhakikisha Hamburg inatwaa ubingwa mwaka huo chini ya kocha kutoka Austria Ernst Happel.

Baada ya ubingwa wake wa 6,HSV ikatawazwa 1983 mabingwa wa kombe la Ulaya la klabu bingwa baada ya kuizabna Juventus Turin ya Itali bao 1:0 katika finali.

Ulikuwa mkwaju maridadi kabisa alieutandika Felix Magath kutoka masafa ya mita 25.Hadi hii leo, huo ndio ushindi wa mwisho mkubwa kwa klabu hii ya Hamburg.

Stadi mwengine aliejiunga na Hamburg kutoka nje baada ya Beckenbauer,akawa Anthony Yeboah-mghana alietamba katika Bundesliga 1993 na si chini ya mara 2 akiichezea Frankfurt pamoja na J.J.Okocha wa Nigeria ,aliibuka mtiaji mabao mengi kabisa katika Bundesliga.

Yeboah lakini, alishindwa kutimiza matarajio aliowekewa na Hamburg alipojiunga nayo kutoka Leeds United ya Uingereza.Haukupita muda Yeboah aliihama Hamburg akielekea Aurabuni kumalizia maisha yake ya dimba.

Stadi wao mkubwa leo ni mholanzi Rafael van der Vaart.Ni mabao yake yalioikoa Hamgburg kutobakia na rekodi yake kuwa timu pekee katika bundesliga isiowahi kuteremshwa daraja ya chini.Kwahivyo, HAMBURGER SV itaendelea hata msimu ujao kutamba katika daraja ya kwanza ikitamani tena kuvaa taji la Bundesliga.