1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hans-Dietrich Genscher afariki dunia

Fischer, Heimo1 Aprili 2016

Mwenyekiti wa heshima wa chama cha waliberali, FDP Hans Dietrich Genscher amefariki mjini Bonn akiwa na umri wa miaka 89. Kwa muda wa miaka mingi Genscher pia alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1INtN
Hans-Dietrich Genscher anderer Ausschnitt
Picha: picture-alliance/dpa/S.Hoppe

Tumekuja kwenu ili kuwapa taarifa kwamba mnaruhusiwa kusafiri nchi za nje." Ni kauli hiyo hasa itakayomfanya mwanasiasa Genscher aendelee kukumbukwa. Aliitoa kauli hiyo mjini Prague katika majira ya kiangazi mnamo mwaka wa 1989.

Alikuwa amesimama kwenye roshani alipoyasema hayo yaliyoleta furaha kubwa kwa raia wa iliyokuwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Ujerumani- waliokimbilia kwenye ubalozi wa Ujerumani magharibi na kuendelea kukaa kwenye ubalozi huo kwa siku kadhaa.

"Ulikuwa wasaa wa kusisimua kuliko mwingine wowote katika wadhifa wangu wote wa kisiasa. Niliweza kuwaelewa watu kwa sababu mimi mwenyewe niliondoka Ujerumani Mashariki nilipokuwa katika umri kama wao. Walikuwa na wasi wasi, lakini nilipowaambia kwamba njia ilikuwa wazi kwa ajili yao,walipiga shangwe ambazo sikuweza kuzifikiria, na huo ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho (wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Ujerumani"), alikumbuka Genscher.

Hans-Dietrich Genscher wakati akitangaza mjini Prague, kuwafungulia milango raia wa Ujerumani Mashariki kuingia Magharibi.
Hans-Dietrich Genscher wakati akitangaza mjini Prague, kuwafungulia milango raia wa Ujerumani Mashariki kuingia Magharibi.Picha: picture-alliance/dpa/R. Kemmether

Nyadhifa alizozitumikia

Katika maisha yake Hans Dietrich Genscher alizitumikia nyadhifa mbalimbali za kisiasa, lakini jina lake liliambatana sana na wadhifa wa waziri wa mambo ya nje. Tayari mnamo mwaka wa 1974 watu wengi walimwita Genscher wakili mahiri wa kuleta urari baina ya magharibi na mashariki. Kutokana na mkutano juu ya usalama na ushirikiano barani Ulaya, Genscher alihamasika kuziundua sera yake juu ya kuondoa mvutano baina ya mashariki na magharibi mnamo miaka ya 80.

Genscher aliutekeleza mpango maalumu wa ziara za kidiplomasia. Baada ya majeshi ya Urusi kuivamia Afghanistan mnamo mwaka wa 1979 Genscher alichukua msimamo mkali dhidi ya Urusi lakini wakati wote aliuacha wazi mlango wa mazungumzo. Alisimama kidete katika siasa ya kuondoa mvutano baina ya magharibi na mashariki lakini kwa uvumilivu.

Kutokana na dalili za mabadiliko ya kisiasa kujitokeza nchini Urusi, Genscher aliweza kuona fursa kwa manufaa ya nchi mbili za kijerumani na kwa ajili hiyo alitoa mwito kwa viongozi wa Ujerumani Mashariki kubadilika kimawazo. Ndoto ya Genscher ilikuwa ya kweli baada ya nchi mbili za kijerumani kuunga tena.

Hans-Dietrich Genscher ni nani hasa?

Hans Dietrich Genscher alizaliwa mnamo mwaka wa 1927 karibu na mji wa Halle katika Ujerumani Mashariki. Baada ya nchi mbili za Ujerumani kuungana tena Genscher alirejea mara kwa mara katika mji wake wa uzawa .

Genscher alikuwa mwasheria aliekuwa mwingi wa fahari alipotunukiwa shahada ya heshima ya uzamifu na chuo kikuu cha Leipzig. Baada ya masomo ya sekondari mnamo mwaka wa 1946 Genscher alisomea sheria kwenye chuo hicho na kwenye chuo cha mjini Halle. Wakati akiwa mwanachama wa chama cha waliberali, mwanasiasa huyo alishuhudia mwanzo wa utawala wa kikomunisti katika Ujerumani Mashariki.

Mnamo mwaka wa 1952 Genscher aliondoka Ujerumani Mashariki na kwenda Bremen ambako alikuwa wakili. Alijiunga na chama cha waliberali cha FDP katika jimbo hilo la Bremen. Na haraka sana alianza kupanda ngazi. Mnamo mwaka wa 1965 aliingia katika bunge la Ujerumani na alikuwamo katika bunge hilo hadi mnamo mwaka wa 1998.

Hans-Dietrich Genscher na mke wake Barbara.
Hans-Dietrich Genscher na mke wake Barbara.Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Mauaji ya wanamichezo wa Israel

Wakati akiwa waziri wa mambo ya ndani Genscher alikabiliwa na mtihani mgumu wa kwanza. Mnamo mwaka wa 1972 magaidi wa kiarabu waliwateka nyara wanamichezo wa Israel mjini Munic. Katika juhudi za kujaribu kuwakomboa wanamichezo hao walikufa.

Genscher alitaka kujiuzulu, lakini Kansela wa wakati huo kutoa chama cha Social Demokratik Willy Brandt alimkatalia. Lakini muda tu kutoka hapo Hans Dietrich Genscher aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje na pia alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama chake cha FDP.

Alikiongoza chama hicho kwa muda wa miaka 11. Lakini uongozi wa serikali ya Ujerumani ulibadilika wakati huo.

Uongozi wa Social Demokratik ulifikia mwisho na chama cha CDU kiliingia madarakani-Helmut Schmidt aliondoka na Helmut Kohl aliingia. Kuunda mseto na CDU ulikuwa uamuzi mgumu kwa Genscher, na alithibitisha mara kwa mara katika mahojiano kwamba ilimwuia vigumu kuutamatisha mseto na Social Demokratik yaani na Helmut Schmidt.

Ndugu wa chama hawakupendelea mseto na CDU na chama cha FDP kiliingia katika mgogoro mkubwa. Genscher amefariki Ijumaa mjini Bonn.

Mwandishi: Lohmüller ,Monika/Seiffert

Mfasiri:Mtullya abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga