1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kijeshi za Marekani hatarini eneo la Sahel

Josephat Charo
17 Machi 2024

Marekani imehangaika Jumapili kutathmini mustakhbali wa opereshei zake dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel kufuatia Niger kusema inafuta ushirikiano wa kijeshi wa miaka mingi na serikali ya mjini Washington.

https://p.dw.com/p/4dpCD
Mkuu wa baraza la mpito la Niger CNSP, Abdramane Amadou
Mkuu wa baraza la mpito la Niger CNSP, Abdramane AmadouPicha: AFP via Getty Images

Utawala wa kijeshi nchini Niger imefuta mkataba wa ushirikiano wake wa kijeshi na Marekani mara moja. Tangazo hilo lililotolewa na msemaji wa baraza la taifa la kuilinda nchi CNSP Kanali Amadou Abdramane, lilitangaza Jumamosi (16.03.2024) jioni na lilitolewa siku moja baada ya ziara ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani kuitembelea nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wakati wa ziara yake, ujumbe huo ulijaribu kukutana na mkuu wa utawala wa kijeshi Abdourahamane Tchiani lakini haukufanikiwa. Mjumbe mkuu wa Marekani Molly Phhe alirejea katika mji mkuu wa Niger, Niamey, wiki hii kukutana na maafisa wa vyeo vya juu wa serikali, akiwa ameandama na Jenerali wa jeshi la Marekani Michael Langley, Mkuu wa kamandi ya Marekani barani Afrika.

Soma pia: Niger yavunja makubaliano ya kijeshi na Ufaransa

Molly aliwahi kuitembelea Niger Desemba mwaka uliopita, huku kaimu naibu waziri wa mambo ya nje Victoria Nuland akisafiri pamoja naye kuizuru Niger mwezi Agosti.

"Tunafahamu juu ya kauli ya baraza la taifa la kuilinda nchi CNSP Niger, ambayo inafuatia mazungumzo ya wazi katika ngazi za juu," alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller katika mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter. "Tunawasiliana na CNSP na tutatoa maelezo zaidi kama ilivyothibitishwa," aliongeza kusema. 

Wanajeshi wa Burkina Faso na Ufaransa wa Operation Barkhane
Operesheni dhidi ya wapiganaji waasi wenye mafungano na kundi la Dola la Kiislamu na mtandao wa al Qaeda katika eneo la Sahel ziko mashakani.Picha: Philippe De Poulpiquet/MAXPPP/dpa/picture alliance

Operesheni dhidi ya ugaidi hatarini

Abdramane alisema waliamua kufuta mkataba unaohusiana na wafanyakazi wa wizara ya ulinzi ya Marekani na wafanyakazi wa kiraia, kwa kuwa waligundua tabia ya dharau na vitisho vya hatua za kisasi kutoka kwa ujumbe huo ulioongozwa na naibu waziri wa mambo ya nje anayeshughulikia masuala ya Afrika, Molly Phee.

Marekani imekuwa na uwepo wake nchini Niger kwa miaka kadhaa katika juhudi za kudhibiti kitisho cha wanamgambo wa kiislamu katika eneo la Sahel. Kufuatia mapinduzi ya kijeshi Julai mwaka uliopita, serikali ya mpito iliyojiteua yenyewe imekuwa ikiyapa kisogo mataifa kadhaa washirika wa zamani, ikiwemo tume ya Umoja wa Ulaya ya kuwajenga uwezo raia, UECAP.

Nchi jirani kama vile Mali na Burkina Faso, pia zimekataa uwepo wa Marekani na Ulaya wakipendelea msaada kutoka kwa Urusi. Utawala wa jeshi ulitwaa madaraka Julai mwaka jana baada ya kumpindua rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia Mohammed Bazoum.

Mpaka wakati Bazoum alipopinduliwa, Niger ilionekana kama ngome ya mwisho ya demorasia katika eneo lililozongwa na mapinduzi na ilikuwa mshirika aliyependwa wa Marekani na mataifa ya Ulaya yaliyopania kuwadhibiti wapiganaji waasi wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.

(dpa, ape)