1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE: Tsvangirai atoka hospitalini

16 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIO

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabe Morgan Tsvangirai, ametoka hospitalini hii leo. Tsvangirai amesema bado anahisi uchungu kufuatia kipigo cha polisi lakini ameapa kuendelea na mapambano yake dhidi ya utawala wa kiimla wa rais Robert Mugabe.

Kiongozi huyo wa chama cha Movement for Democtratic Change, MDC, alipokea matibabu kwa kile chama chake ilichokiita ufa kwenye fuvu la kichwa, siku mbili baada ya kutiwa mbaroni pamoja na viongozi wengine wa upinzani wakati wa mkutano wa maombi mjini Harare.

Mke wa Tsvangirai, Susan, amesema kupigwa kwa mumewe umekuwa mtihani mgumu kwake lakini ana matumaini mageuzi yatafanyika nchini Zimbabwe.

´Ulikuwa wakati mgumu wa majaribu kwangu tangu Jumapili, kwa sababu sijaona ukatili kama huo maishani mwangu. Lakini inanipa moyo na matumaini kwamba kitu kitafanyika hivi karibuni. Kutakuwa na mageuzi siku chache zijazo kwa sababu hizi ni siku za mwisho za mfa maji.´

Katika taarifa iliyochapishwa leo na gazeti la Independent, mjini London Uingereza, Morgan Tsvangirai amesema licha ya polisi kuutesa mwili wake, hatavunjika moyo bali ataendelea kupigania uhuru wa Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe amewaambia waliomkosoa kwa mateso dhidi ya Tsvangirai waende kujitia kitanzi. Amemlaumu kiongozi huyo kwa kuchochea machafuko yaliyosababisha kukamatwa kwake Jumapili iliyopita.