1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE:Sheria za uchaguzi kubadilishwa

19 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBOb

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimefikia makubaliano na serikali ili kutimizwa kwa sheria itakayowezesha uchaguzi wa rais na wabunge kufanyika pamoja katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.Katika hatua ambayo haikutarajiwa wanachama wa ngazi za juu wa chama cha Movement for Democratic Change MDC wanasema kuwa hawatapinga mabadiliko ya katiba yatakayobadili sheria za uchaguzi,kuongezwa kwa idadi ya wabunge aidha kusogeza mbele uchaguzi wa wabunge kwa miaka miwili.Kwa mujibu wa Welshman Ncube mwanachama wa ngazi za juu katika kundi lililojitenga katika chama cha MDC hatua hiyo huenda ikaondoa mivutano kati ya serikali na vyama vya upinzani.Mivutano hiyo ilisababisha majeshi ya usalama kushambulia viongozi wa chama hicho mapema mwaka huu.

Kulingana na Waziri wa Sheria wa Zimbabwe Patrick Chinamasa tukio hilo ni la kihistoria.Chama cha MDC kwa upande wake kilikataa mabadiliko hayo awali na kuyaelezea kama juhudi za Rais Mugabe na chama chake cha ZANU-PF kulazimisha matokeo ya uchaguzi yanayoegemea upande wao.Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini amekuwa akisimamia juhudi za upatanishi kati ya serikali na upinzani huku uchaguzi ukiwadia.Kiongozi huyo aliyekabidhiwa jukumu hilo na Jumuiya ya maendeleo ya SADC anaripotiwa kukutana mjini Pretoria na maafisa wa ngazi za juu wa chama cha MDC wiki jana.

Tangazo hilo linatolewa huku mjadala kuhusu mabadiliko ya katiba ukifikia awamu ya pili.Kulingana na waziri wa Sheria wa Zimbabwe Patrick Chinamasa,endapo sheria hiyo itapitishwa idadi ya wabunge itaongezwa kutoka 150 hadi 210 aidha kuwezesha bunge kuteua kiongozi endapo nafasi ya rais inakuwa wazi kabla muhula kumalizika.Rais Mugabe amekuwa madarakani tangu mwaka ’80 wakati Zimbabwe ilipopata uhuru wake na anawania muhula wa saba.