1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hasara kubwa ya maisha kufuatia zilzala iliyopiga Uturuki

24 Oktoba 2011

Zilzala iliyopiga jana katika jimbo la mashariki la Uturuki-Van, linalopakana na Iraq imeangamiza maisha ya zaidi ya watu 239 na zaidi ya elfu moja kujeruhiwa. Mtu mmoja ameokolewa yu hai hii leo.

https://p.dw.com/p/12xdk
Waokozi wanajitahidi kufukua kuwatafuta waliosalimikaPicha: picture-alliance/dpa

Watu zaidi ya mia moja wamefariki katika mji wa Van, kitovu cha jimbo lenye jina kama hilo na wengine zaidi ya 117 katika mkoa wa Ercis-eneo lililoteketea vibaya sana kutokana na tetemeko hilo la ardhi, amesema waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki, Idris Naim Sahin, aliyezungumzia juu ya zaidi ya watu 1,200 waliojereuhiwa.

Katika mkoa wa Ercis maripota wanazungumzia juu ya hasara kubwa kabisa iliyopiga katika eneo hilo lenye wakaazi karibu laki moja na ambako majumba kadhaa yameporomoka. Wakaazi kadhaa wa eneo hilo wameyapa kisogo maskani yao.

Katika miji ya Van na Ercis iliyoko karibu na kitovu cha tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na nguvu za 7.2 katika kipimo cha Richter, waokoaji wakibeba sepetu wanasaidia kuwafukua watu waliofunikwa maporomoko ya majumba.

Wamefanya kazi usiku kucha licha ya baridi kali na mwangaza wa tochi huku waliosalimika wakijikusanya ndani ya mahema au hata nje.

Erdbeben Türkei Flash-Galerie
Waziri mkuu Erdogan (wa pili kulia) na mawaziri wakePicha: picture-alliance/dpa

Watumishi wa shirika la Uturuki la Hilal Nyekundu linajitahidi kujenga mahema katika baadhi ya maeneo ya mji huo na kugawa vyakula.

Katibu mkuu wa shirika la hilali nyekundu la Uturuki, na ambae pia ndiye anayesimamia shughuli za uokozi, Ahmet Lutfi, anasema:

" Kuna mahema ya kutosha yanayoletwa katika eneo hili, mablanketi na majiko pia. Shehena za mwanzo zimeshafika. Mahema yameshaanza kujengwa. Ercis ndio kitovu cha tetemeko hili la ardhi. Juhudi zetu zinatuwama Ercis na vijiji vya karibu na hapa."

Waziri mkuu, Recep Tayyeb Erdogan, na mawaziri wake kadhaa walilitembelea eneo hilo la maafa jana usiku na kuahidi kila la kufanywa litafanywa kuwasaidia wahanga wa zilzala hiyo.

Waokoaji karibu ya 1,300 wakifuatana na mbwa kutoka kila pembe ya Uturuki wanamiminika, saa 20 baada ya tetemeko hilo kupiga, kujaribu kuwafukua waliosalimika. Vikosi vya wanajeshi, helikopta na ndege ya mizigo vimepelekwa katika eneo hilo la maafa.

Wenyeji nao hawajapakata mikono wanaondowa vifusi kwa mikono na kuuliza kama watu wako chini ya vifusi hivyo.

Türkei Erdbeben
Wahanga wa tetemeko la ardhi la UturukiPicha: dapd

Watu wasiopungua wanne wameokolewa kwa namna hiyo. Yalcin Akay ameokolewa toka magofu ya ghorofa ya sita baada ya kupiga simu kwa polisi na kuwaeleza yuko wapi.

Kishindo cha zilzala kilipiga pia Van, mji wenye utajiri mkubwa wa utamaduni ulioko karibu na ziwa na kuzungukwa na milima ya theluji.

Nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani na Israel, licha ya mgogoro wa kidiplomasia uliopo pamoja na Ankara, wamejitolea kusaidia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri:Josephat Charo