1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatari kwa mkutano wa G8?

Maja Dreyer10 Mei 2007

Ni mwezi mmoja tu umebaki hadi kufanyika mkutano wa kilele wa nchi zinazostawi kiviwanda duniani, kwa ufupi G8, hapa nchini Ujerumani. Katika juhudi zao za kuhakikisha usalama wa mkutano huo, polisi ya Ujerumani jana ilivamia nyumba wanapokutana makundi ya msimamo mkali ya mrengo wa kushoto katika miji kadhaa ya humu nchini.

https://p.dw.com/p/CHSz
Watu kadhaa wamekamatwa kwenye uvamuzi huo wa polisi
Watu kadhaa wamekamatwa kwenye uvamuzi huo wa polisiPicha: AP
Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali, makundi kadhaa yanatumuhiwa kuvuruga mkutano wa G8 kwa njia ya kigaidi. Matukio haya ni masuala muhimu katika uchambuzi wa magazeti ya humu nchini, maoni yakiwa ni tofauti lakini. La kwanza ni la gazeti la “Schweriner Volkszeitung”:

“Kwa kuchukua hatua hiyo, polisi imeonyesha wazi kuwa inatathmini hatari ya kufanyika mashambulio kuwa kubwa na pia kwamba haitakubali mashambukio kutokea. Maadamano ya wapinzani wa utandawazi tangu miaka mingi yanaisindikiza mikutano ya kilele ya nchi zinazoongoza kiviwanda. Kandoni mwa wale waandamanaji wanaotumia njia ya amani kuwakumbusha viongozi wa nchi za G8 mahitaji ya nchi maskini, bahati mbaya kuna pia wale waandamanaji wanaotumia nguvu. Wale wanaopigania usawa duniani wanapaswa kujitenganisha na wahalifu wanaotumia maandamano hayo kushambulia ovyoovyo.”

Gazeti la “Tagesspiegel” lakini lina wasiwasi juu ya uvamizi huo wa polisi na matokeo yake. Linaandika:

“Uvamizi huo ulilengwa kuwaonya wale wanaharakati wanaotumia nguvu na kuwatishia. Lakini kuna mashaka ikiwa lengo hili litafikiwa. Huenda tishio hilo litafikia pahali tofauti. Yaani sasa uwezekeno ni mkubwa kuwa wale wanaharakati wanaoandamana kwa amani watakaa nyumbani kutokana na kuhofia ghasia.”

Gazeti la Braunschweiger Zeitung lakini lina msimamo ulio wazi kabisa:

“Ni muhimu kwa viongozi wa nchi zinazoongoza kiviwanda duniani kukaa kwenye meza moja na kuzungumza. Kwa hivyo inabidi kuzuia mahali pa mkutano Heiligendamm pasiwe mahali pa vita. Kuna kundi dogo la wahalifu ambao wanaenda maandamanoni tu kuanzisha fujo. Heiligendamm bila shaka upo kwenye ratiba yao ya safari. Wana malengo yoyote ya kisiasa.”

Hatimaye tuelekee Ufaransa kwa suala la pili. Rais mteule wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, baada ya ushindi wake katika uchaguzi, amefanya likizo fupi kwenye boti nzuri ya rafiki wake mkuu wa kampuni kubwa. Ni jambo lililozusha kasoro nchini mwake, na pia humu Ujerumani wahariri wanamkosoa Sarkozy. Hilo hapa gazeti la “Financial Times Deutschland”:

“Hadi kwenye mwisho wa kampeni ya uchaguzi, Sarkozy alijionyesha kama ni mtu wa kawaida ambaye alianza chini na kupanda juu. Alitangaza ataendesha mtindo mpya wa kisiasa pamoja na kuunganisha Ufaransa badala ya kuigawa. Lakini siku tatu tu baada ya kuchaguliwa anafanya kinyume chake. Kwa kufanya likizo hii ya anasa anaendelea kama alivyofanya awali. Bila ya shaka yoyote alieleza kuwa hajali ikiwa watu wanakasirika. Hii basi ni tabia ya kiburi ya mfalme mpya Sarkozy.”