1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimae kinu cha nyuklia cha Yongbyon kufungwa

29 Juni 2007

Maafisa wa shirika la kimataifa linalodhibiti nishati ya nyuklia wamefikia maelewano na Korea Kaskazini kuhusu kufungwa kwa kinu cha nyuklia cha Yongbyon.

https://p.dw.com/p/CHBs
Kim Yong Nam kiongozi wa Korea Kaskazini
Kim Yong Nam kiongozi wa Korea KaskaziniPicha: AP

Mkuu wa ujumbe huo wa shirika la umoja wa mataifa linalodhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia amesema kwamba ujmbe wake umeridhishwa kufuatia ziara waliyoifanya katika kinu cha nyuklia cha kaskazini mwa Yongbyon ambacho serikali ya Korea Kaskazini iliahidi kusimamisha kabisa kazi zake katika makubaliano yaliyofikiwa na pande sita mwezi Februari.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la IAEA Olli Heinonen amenukuliwa na vyombo vya habari mjini Pyongyang kwamba ziara hiyo ni ya kwanza kufanywa na maafisa wa shirika lake tangu mwezi Desemba mwaka 2002 walipotimuliwa na serikali ya Pyongyang.

Korea Kaskazini baadae ilijiondoa kutoka kwenye mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia na kutangaza kuwa inadhibiti mabomu ya atomiki na hapo mwaka jana Pyoyngyang ilifanya jaribio lake la kombora la kinyuklia lililoushangaza ulimwengu mzima.

Mkurugenzi huyo wa shirika la kimataifa linalodhibiti matumizi ya nyuklia bwana Heinonen amesema leo kwamba maafisa wake wamefanikiwa kuzuru sehemu zote zilizotakikana ikiwemo sehemu inayotumika kuzalisha madini ya Plutonium ambayo mabaki yake yanaweza kutumiwa kutengeneza viwango mbalimbali vya silaha.

Baada ya mazungumzo ya leo bwana Heinonen amefahamisha kwamba maafisa wake na Korea Kaskazini wamefikia maelewano ya kufungwa kabisa kwa kinu hicho cha Yongbyon lakini wakati huo huo amedokeza kuwa muda hasa wa kutekeleza ufungaji huo utaamuliwa na washiriki wa pande sita kuhusu mpango wa nyuklia wa Pyongyang.

Eneo zima la kituo cha Yongbyon lina zaidi majengo mia moja ambamo pia mna kinu chenye megawati tano, eneo hilo ndilo kitovu cha mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini ulioanza miaka ya 80.

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini Song Min-soon ambae yuko mjini Washington kwa mazungumzo na maafisa wa Marekani amesema kwamba uwezekano upo wa kuanzishwa mapema mazungumzo ya pande sita kati ya Korea Kaskazini na washirika watano wa mpango wa nyuklia wa nchi hiyo sambamba na shughuli za kukifunga kinu cha Yongbyon.