1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

031109 Brüssel EU-Vertrag

4 Novemba 2009

Hatimaye Rais Vaclav Klaus wa Jamhuri ya Czech amekuwa kiongozi wa mwisho barani Ulaya kutia saini kuuridhia mkataba mpya wa Ulaya uliopewa jina la mkataba wa Lisbon.

https://p.dw.com/p/KO4N
bendera ya Umoja wa UlayaPicha: EU

Hatua hiyo inafuatia mahakama ya Czech kutupilia mbali kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wabunge waliyodai kuwa mkataba huo unakwenda kinyume na katiba ya nchi hiyo.

Viongozi kadhaa wamepongeza hatua hiyo akiwemo, Waziri mpya wa Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle aliyeko ziarani nchini Ubelgiji katika makao makuu ya umoja huo wa Ulaya.

Viongozi na wanasiasa mbalimbali wameipongeza hatua hiyo ambayo ilikuwa ni kikwazo cha mwisho kwa mkataba huo kuanza kutumika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ambaye yuko katika ziara ya kujitambulisha, akizungumza mjini Brussels, alisema kuwa, kila kitu hivi sasa kinaweza kwenda haraka, na kwamba inategemewa mkataba huo kuanza kutumika tarehe mosi mwezi ujayo kwani sasa imeridhiwa na nchi zote wanachama.

Guido Westerwelle, FDP, Außenminister und Vizekanzler Flash-Galerie
Waziri wa Nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: picture alliance/dpa

´´Mkataba wa Lisbon siyo tu una faida kwa mataifa wanachama ya Umoja wa Ulaya, lakini pia kwa bara lote la Ulaya´´

Naye Kansela Angela Merkel ambaye yuko ziarani nchini Marekani amesema kuwa  Umoja wa Ulaya sasa utakuwa imara zaidi  na kwamba jana ilikuwa siku muhimu sana ambayo ni mwisho wa mchakato uliyochukua miaka kadhaa ya kutekelezwa kwa mabadiliko ya mkataba huo wa Lisbon.

Rais Nicolaus Sarkozy wa Ufaransa alisema kuwa Umoja wa Ulaya sasa utaweza kuwa na  taasisi mpya ambazo zitafanyakazi kwa mahitaji ya karne ya 21.

Mkataba huo umetayarishwa ili kuweza kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kazi za umoja huo, ambao umepanuka mara mbili zaidi tokea yalipoanza kujiunga  mataifa ya zamani ya kikoministi ikiwemo Jamuhuri ya Czech iliyojiunga mwaka 2004.

Gordon Brown G8 Gipfel in Italien
Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon BrownPicha: picture alliance / empics

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown, ambaye chapuo lake kwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi nchi hiyo Tony Blair kutaka kuchaguliwa kuwa mkuu mpya wa umoja huo, lilishindwa, baada ya wakuu wa nchi za umoja huo kuonesha kutokubaliana naye, alisema sasa umoja huo uko katika nafasi ya kushughulia masuala muhimu.

 ´´Na ni matumaini yangu kuwa Ulaya itaweza kuweka pembeni miaka kadhaa ya majadiliano ya kikatiba na sasa tunaweza kusonga mbele na kushughulikia masuala muhimu ambayo umoja wa Ulaya unakabiliana nayo ambayo ni jinsi ya kupata ajira za kazi, jinsi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi ya kuimarisha usalama kwa wananchi wa Ulaya´´

Rais Barack Obama wa Marekani naye pia hakuwa nyuma kuipongeza hatua hiyo akisema kuwa itaimarisha zaidi ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Akizungumza baada ya kukutana na mkuu wa kamisheni ya Umoja huo wa Ulaya Jose Manuel Barroso, mkuu wa sera za nje wa umoja huo Javier Solana pamoja na Waziri Mkuu wa Sweden ambayo ndiyo inayoshikilia kiti cha urais wa umoja huo,Fredrik Reinfeldt mjini Washington, Rais Obama, alisema mkataba huo utafungua njia kwa pande hizo mbili kuzidisha ushirikiano wao  siyo tu katika masuala ya kiuchumi, bali katika masuala ya usalama.

Mjini London, kiongozi wa chama cha upinzani cha Consevatives, David Cameron amebadilisha msimamo wake wa kuupinga mkataba huo kama chama chake kitashinda katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Msemaji wa sera za nje wa chama hicho William Hague amesema kuwa kutokana na mkataba huo hivi sasa kuwa sheria  barani Ulaya, kura ya maoni haiwezi kuitishwa dhidi yake.

Cameron ambaye anategemewa na wengi kushinda katika uchaguzi wa mwakani alisema kuwa chama chake kingeitisha kura ya maoni dhidi ya mkataba huo wa Lisbon.Lakini sasa amefuta dhamira na kutangaza kuunga mkono.

Waziri Mkuu wa Sweden Fredrik Reinfeldt amesema ataitisha mkutano maalum wa wa wakuu wa nchi wanachama siku chache zijazo kujadiliana masuala muhimu, yakiwemo kuwachagua wakuu wapya wa  umoja huo.

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Herman van Rompuy anapigiwa upatu kuweza kuchukua nafasi mpya ya urais wa umoja huo.

Mwandishi:Susanne Henn/AFPE

Mtafsiri:Aboubakary Liongo

Mhariri. Sekione  Kitojo.

Audio in DaletWeb:

ENDE