1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Saudi Arabia yawaruhusu wanawake kuendesha gari

Mohammed Khelef
27 Septemba 2017

Baada ya miaka kadhaa ya kupigania haki ya kuendesha gari na kuzuiliwa, hatimaye wanawake kwenye Ufalme wa Saudi Arabia wameondoshewa rasmi marufuku hiyo na Mfalme Salman na mwakani wataanza kuingia barabarani kisheria.

https://p.dw.com/p/2knGp
Saudi Arabien Frau in einem Auto in Road
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Jamali

FE: Frauen MMT/04/05/06.10.2017 Women in Saudi Arabia - MP3-Stereo

Wakati wanawake katika nchi nyengine za kiislamu wana uhuru wa kuendesha magari bila ya kipingamizi, amri ya kuwapiga marufuku nchini Saudi Arabia imekuweko kwa miaka mingi.

Kwa hakika; si sheria ya Kiislamu wala sheria ya Saudi Arabia inayohusika na usafiri barabarani inayopiga marufuku wanawake kuendesha gari, lakini walikuwa tu wakinyimwa leseni na hata kukamatwa pale wanapokutikana wakifanya hivyo.

Balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani, Mwanamfalme Khaled bin Salman, alisema kuwaruhusu wanawake kuendesha gari ni hatua moja kubwa mbele na kwamba jamii sasa iko tayari kwa hilo.

"Huu ni wakati muwafaka wa kufanya hivyo," mtoto huyo wa Mfalme Salman aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington.

Tangazo  hilo lilitolewa kama Kanuni ya Ufalme ambayo ilitangazwa Jumanne na shirika la habari la taifa na televisheni ya taifa.

Adhabu kali kwa wanawake

Aziza Youssef, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mfalme Saud na mmojawapo wa wanaharakati wakosoaji kuhusu haki za wanawake, alisema hii ni hatua nzuri  kwa haki za wanawake, miongoni mwa  haki chungu nzima wanazozipigania.

Saudi Arabien - Kronprinz Mohammed bin Salman bei Militärübung
Mfalme Salman (kushoto) na mrithi wake, Mohammed bin Salman, anayetajwa kuwa na nguvu za kushawishi mageuzi ya sasa.Picha: picture-alliance/abaca/Balkis Press

"Hadi sasa kuna mifano chungu nzima ambapo wanawake wanaadhibiwa kwa sababu tu ya kuendesha gari," alisema mwanaharakati huyo. 

Mnamo mwaka 1990, wanawake 50 walikamatwa kwa kuendesha gari na wakanyang'anywa hati zao za kusafiria na pia kufukuzwa kazi.

Zaidi ya miaka 20 baadaye, hapo mwaka 2011 mwanamke mmoja alihukumiwa kupigwa bakora 10 kwa kuendesha gari, ingawa baadae Mfalme Abdullah aliibatilisha hukumu hiyo.

Mnamo mwaka 2014, wanawake wawili wa Kisaudi walitiwa nguvuni kwa zaidi ya miezi miwili kwa kukiuka amri hiyo, wakati mmoja wao alipojaribu kuvuuka mpaka wa Saudi Arabia kwa kutumia leseni ya taifa jirani la Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu.

Wasaudia washangiria ushindi

Amri hii mpya kuwaruhusu wanawake kuendesha gari nchini Saudi Arabia imepongezwa na Rais Donald Trump wa Marekani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gueterres. Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Gueterres alisema: "Hii ni hatua muhimu, katika njia sahihi."

Baadhi ya kanda za vidio kwenye mtandao wa YouTube zimezionesha familia na madereva wa kiume wakiashiria alama ya ushindi kwa wanawake na wakisema kuwa wakati wa mabadiliko umewadia.

Saudi-Arabien Frauen im Stadion in Riad
Katika matukio ya nadra sana, wanawake nchini Saudi Arabia waliruhusika kwa mara ya kwanza kuhudhuria sherehe za kitaifa kwenye uwanja wa michezo mnamo tarehe 23 Septemba 2013.Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Mwanaharakati wa haki za wanawake, Madeha al Ajroush alielezea furaha yake huku akiwa na shauku kubwa.

"Nimefurahi sana na nina shauku. Sikuweza kuamini kwani kwa miaka 27 tumekuwa tukilisubiri hili, hatimaye limekuja. Ninakosa hata la kusema isipokuwa nimefurahi sana sana."

Hata hivyo wanawake hawatoruhusiwa kuanza kuendesha gari mara moja, badala yake kamati maalum itaundwa kuangalia jinsi amri hii mpya itakavyotekelezwa.

Pamoja na mabadiliko haya, kwa sehemu kubwa wanawake nchini Saudi Arabia bado wanategemea kibali chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mwanamme katika familia kama vile wanapotaka kupata hati ya kusafiria, kwenda nje ya nchi au kuolewa.

Mwishoni mwa juma, Mfalme Salman na mwanawe mdogo wa kiume na mrithi wake, Mohammed bin Salman, mwenye umri wa miaka 32,waliwaruhusu wanawake kuingia kwenye uwanja mkuu  wa michezo mjini Riyadh kwa ajili ya sherehe za kila mwaka za taifa hilo, uwanja ambao umekuwa ni kwa wanaume pekee.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/AP
Mhariri: Josephat Charo