1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye watafiti wagundua sumu ya Mbungó

25 Machi 2012

Mbungó hueneza magonjwa ya Nagana, ambayo yanakadiriwa kusababisha vifo vya ngómbe milioni tatu kila mwaka, hali inayoathiri vikubwa uzao wa wanyama hao. Lakini sasa kuna sumu ya kukabiliana nao.

https://p.dw.com/p/14MMw
Mbungó ni mdudu anayeeneza ugonjwa wa Nagana
Mbungó ni mdudu anayeeneza ugonjwa wa NaganaPicha: picture-alliance/dpa

Ufugaji ndio chanzo kikuu cha kuingiza kipato kwa wafugaji wa kabila la Kimasai nchini Kenya na Uganda. Wafugaji hao hujipatia chakula, kipato na usalama kutokana na fedha wanazopata baada ya kuuza mazao ya mifugo hiyo.

Lakini changamoto kubwa inayowakabili Wamasai hao ni wadudu wajulikanao kama mbung´o. Ili kukabiliana na tatizo hili, wanasayansi nchini Kenya wametengeneza sumu ya kuwaua.

Wanasayansi hao wa Kituo cha Kimataifa cha Fisiolojia na Ekolojia ya Wadudu (ICIPE) mjini Nairobi, Kenya wanamchukulia mbung´o kama mpinzani wa kutisha. Chakula kikuu cha mdudu huyu ni damu ya binadamu, wanyama wa kufugwa na wanyama pori pia.

Athari za Ugonjwa wa Nagana

Mbungó hueneza magonjwa ya Nagana, ambayo yanakadiriwa kusababisha vifo vya ngómbe milioni tatu kila mwaka, hali inayoathiri vikubwa uzao wa wanyama hao.

Aidha, wanyama waliougua ugonjwa wa Nagana, aghalabu hukosa siha njema. Kiwango cha kuzaliana cha wanyama hao hupungua, na wale wanaokamuliwa hutoa maziwa machache na pindi wanapochinjwa huwa na nyama kiasi kidogo sana.

Kijana akiswaga ngómbe kuelekea malishoni
Kijana akiswaga ngómbe kuelekea malishoniPicha: dapd

Licha ya kuwepo kwa kampeni za mara kwa mara za kutokomeza mbungó nchini Kenya, wakazi wengi wa vijijini pamoja na wanyama waliopo katika hifadhi za taifa bado wanakabiliwa na ugonjwa unaoitwa Nagana. Halikadhalika, kushindwa kuwaondoa kabisa wadudu hao kwa njia ya kemikali, kunazidi kudidimiza juhudi za kupunguza umaskini.

Hatahivyo, utafiti wa Kituo cha Kimataifa cha Fisiolojia na Ekolojia ya Wadudu nchini Kenya, unaonesha kuwa ugonjwa wa Nagana unaweza kuzuiwa kutokana na kinga inayotengeneza kutokana na viambata walivyochukua kwa mnyama aina ya Ndogoro. Watafiti hao wametengeneza kinga hiyo inayovaliwa na ngo´ombe shingoni. Kifaa hicho chepesi chenye kinga kinapunguza uwezo wa mbungó kungáta wanyama kwa asilimia 90.

Jinsi kinga hiyo inavyotumiwa

Rajinder Kumar Saini ni mwanasayansi mkuu na kiongozi wa Kitengo cha Afya ya Wanyama katika kituoni hapo, anasema,"Tumevumbua kemikali hii kwa sababu tumegundua kwamba wadudu hawa hawali viambata hivyo, kwa hivyo tulivitathmini viambata hivyo na tukagundua kemikali inayopatikana ndani yake. Tumevifanyia majaribio mara kadhaa, na viambata vitatu tulivyonavyo vina harufu kali na ndivyo vinavyowekwa shingoni mwa mnyama."

Akifafanua zaidi, Daktari Saini anasema kiwinga hicho si lazima kiwekwe katika shingo ya mnyama. Kinaweza pia kuwekwa sehemu yoyote shambani, mahali ambapo kitaweza kuwafukuzia mbali mbungó hao. Mpaka sasa, wafugaji wengi wamepokea vyema teknolojia hiyo mpya.

Rajinder Kumar Saini anasema "Kinga hii dhidi ya mbungó haiuzwi kwa bei ghali. Unaweza kuinunua tu sokoni na kuichanganya ili kuwalinda wanyama hao."

Ngómbe wenye siha njema hutoa maziwa na nyama kwa wingi
Ngómbe wenye siha njema hutoa maziwa na nyama kwa wingiPicha: AP

Kituo hicho cha Kimataifa cha Fisiolojia na Ekolojia ya Wadudu mjini Nairobi, kiko mstari wa mbele katika kuendelea na mradi huo wa utafiti, kinazalisha kinga hiyo kwa wingi. Mwezi Agosti, mwaka 2009, Umoja wa Ulaya, ambao ndio mfadhili mkuu wa mradi huo, ulikiomba kituo cha ICIPE kutafuta washirika zaidi wa kibiashara, ambao wataweza kuzalisha kwa wingi zaidi kinga hiyo.

Tangu mwaka 2009, Taasisi ya Maendeleo ya Utafiti wa Viwanda nchini Kenya, ilichukua wazo hilo na kuendeleza uzalishaji wa kinga hiyo kwa wingi zaidi.

Wakati huo huo, Kampuni moja ya nchini Uswizi imekubali kutathmini na kuvifanyia utafiti zaidi viambata hivyo ili kudhibiti wadudu wengine sehemu mbalimbali duniani.

Mwandishi: Asumpta Lattus

Mtafsiri: Ndovie, Pendo Paul

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed