1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Westerwelle afunga ndoa.

Halima Nyanza20 Septemba 2010

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amefunga ndoa na mpenzi wake wa kiume wa siku nyingi Michael Mronz. Harusi hiyo ilifanyika hapa Bonn, mji alikozaliwa mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/PGoV
Gudo Westerwelle akiwa na mumewe Michael Mronz.Picha: AP

Katika ripoti iliyotolewa na gazeti la Bild la hapa Ujerumani na kuthibitishwa na msemaji wa chama cha FDP, kinachoongozwa na mwanadiplomasia huyo, Guido Westerwelle mwenye umri wa miaka 48 na mpenzi wake mfanyabiashara Michael Mronz mwenye miaka 43, walihalalisha rasmi uhusiano wao huo, katika ndoa yao iliyofungwa na meya wa mji wa Bonn Juergen Nimptsch.

Ni watu wa karibu kutoka katika familia hizo mbili na marafiki ndio waliialikwa kuhudhuria hafla hiyo.

Westerwelle , ni mwenyekiti wa chama cha Liberal Free Democrats -FDP- na pia ni Kansela msaidizi katika serikali ya mrengo wa kati kulia inayoongozwa na Kansela Angela Merkel,

Waziri wa mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na mpenzi wake huyo Michael Mronz meneja wa michezo, wamefunga ndoa siku ya Ijumaa baada ya kuwa na uhusiano tangu mwaka 2003 walipokutana katika mji wa Aachen, hapa Ujerumani.

Kabla ya kuhalalisha rasmi mahusiano yao hayo, Michael Mronz alikuwa akiongozana na  na Westerwelle katika ziara zake nje kama waziri wa mambo ya nje, lakini alisitisha kufanya hivyo mara kwa mara baada ya viongozi wa upinzani kuhoji juu ya uwezekano wa kuwapo kwa maslahi binafsi, huku viongozi waandamizi wa chama cha upinzani cha Social Democrats SPD, wakiuliza kuwa Michael Mronz atatumia safari hiyo kwa ajili ya kufanikisha biashara zake.

Sheria ya Ujerumani kuhusiana na kuoana kwa watu wa jinsia moja ililegezwa na serikali ya mrengo wa kati kushoto iliyokuwa ikiongozwa na SPD na kijani.

Chama cha kijani kilipendekeza kuruhusiwa kwa wapenzi wa jinsia moja kuweza kuoana.

Wakati huohuo, Chama tawala nchini Ujeruimani cha Free Democrats FDP, ambacho kinaunda serikali ya muungano, kimekanusha taarifa kwamba kiongozi wa chama hicho Guido Westerwelle anafikiria kujitoa katika uongozi wa chama hicho.

Taarifa hizo zinakuja wakati kura ya maoni iliyopigwa hivi karibuni ikionesha kwamba msaidizi huyo wa Kansela Angela Merkel, uungwaji mkono wake ukishuka kwa asilimia nne baada ya kushika asilimia 15 katika uchaguzi wa shirikisho la Ujerumani uliofaynika mwezi Septemba mwaka uliopita.

Gazeti moja hapa nchini lilimnukuu Waziri huyo ambaye ni Waziri wa kwanza nchini Ujerumani kutangaza hadharani kwamba ni shoga, wakati wa ziara yake ya mapumziko katika mji wa kitalii wa Mallorca akisema kwamba alifikiria kung'atuka katika uongozi wa chama hicho.

Wakosoaji wamekuwa wakisema kwamba Westerwelle ameshindwa kutekeleza majukumu yake mwanadiplomasia mkuu wa Ujerumani na mara kwa mara kujiingiza  katika mabishano ya siasa za ndani jambo ambalo limezorotesha shughuli za serikali ya mseto.

Mwandishi: Halima Nyanza/Reuters, afp, dpa)

Mhariri:Abdul-Rahman