1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya Ugiriki katika Umoja wa Ulaya inatiliwa shaka

18 Juni 2015

Mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro wanakutana Alhamisi mjini Luxembourg kuujadili mgogoro wa fedha unaoikumba Ugiriki huku ikihofiwa huenda nchi hiyo ikalazimika kuondoka kutoka kanda ya euro.

https://p.dw.com/p/1Fiuj
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Huku mazungumzo kati ya Ugiriki na wakopeshaji wake Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha duniani IMF yakigonga mwamba wiki hii, maafisa wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wameanza kujadili wazi uwezekano wa Ugiriki kuondoka kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro.

Hapo jana, siku moja kabla ya mkutano wa nchi wanachama 19 wa kanda hiyo inayotumia sarafu ya euro kufanyika, benki kuu ya Ugiriki kwa mara ya kwanza ilionya kuwa nchi hiyo huenda ikalazimika kujiondoa kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro na hata kutoka kwa Umoja wa Ulaya iwapo itashindwa kufikia makubaliano na wakopeshaji wake.

Benki hiyo imesema kuondoka kwa Ugiriki katika kanda inayotumia sarafu ya euro kutasababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi, kupungua pakubwa kwa mishahara na kuongezeka maradufu kwa ukosefu wa ajira katika taifa hilo la kusini mwa Ulaya.

Kuondoka kwa Ugirki kwajadiliwa wazi

Na kama ishara ya kuwa uwezekano huo wa kujiondoa kwa Ugiriki katika umoja huo ni jambo ambalo linazingatiwa, mkuu wa benki kuu ya Ujerumani Jens Weidmann amesema kujiondoa kwa Ugiriki kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro kutabadili mkondo wa uthabiti wa sarafu hiyo lakini haitaiporomosha kwani kanda hiyo haiitegemei Ugiriki.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Schmidt

Licha ya onyo hilo la kuondoka kwa Ugiriki na nchi hiyo kutarajiwa kuilipa IMF euro bilioni 1.6 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu,waziri wa fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amesema hatarajii mzozo wa kuitaka Ugiriki kufanya mageuzi magumu ya kiuchumi ili ipewe mkopo zaidi wa uokozi kutatuliwa katika mazungumzo ya leo na kuongeza ni viongozi wa kisiasa ndiyo wanaoweza kufikia makubaliano hayo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana imani kuwa makubaliano na Ugiriki yanaweza kufikiwa kwani palipo na nia pana njia na kuongeza angeitaka nchi hiyo kusalia katika kanda inayotumia sarafu ya euro.

Marekani pia yatiwa wasiwasi

Mgogoro huo wa kiuchumi umeitia wasiwasi pia Marekani. Mkuu wa benki kuu ya Marekani Janet Yellen ameonya uchumi wa dunia utakumbwa na msukosuko iwapo Ugiriki na wakopeshaji wake watashindwa kufikiana.

Maelfu ya wagikriki waandamana mjini Athens kupinga masharti ya wakopeshaji
Maelfu ya wagikriki waandamana mjini Athens kupinga masharti ya wakopeshajiPicha: Reuters/Y. Behrakis

Yellen amesema kukosa makubaliano muhimu ya kiuchumi anaona kutakuwa na matatizo yatakayoikumba Ulaya na masoko ya fedha duniani

Kura za maoni zinaonyesha wengi wa wagiriki wanaunga mkono mkakati unaotumika na serikali katika kufanya mazungumzo na wakopeshaji wake. Kiasi ya watu 7,000 waliandamana hapo jana jioni katika mji mkuu wa Ugiriki Athens, kupinga masharti ya wakopeshaji ya kutaka serikali ibane zaidi matumizi.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras anatarajiwa kuhudhuria hii leo jukwaa la kiuchumi la kimataifa nchini Urusi na kufanya mazungumzo hapo kesho na Rais wa Urusi Vladimir Putin hatua ambayo wachambuzi wanasema ni ishara kuwa Tsipras anajaribu kuuonyesha umoja wa Ulaya kuwa ana mikakati mingine ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi unaoikumba nchi yake.

Mwandishi: Caro Robi/AFP/dpa/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga