1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua za dharura zahitajika kupambana na upotevu wa chakula

Mohmed Dahman22 Agosti 2008

Mzozo wa chakula duniani ambao umechochea ghasia na maandamano katika zaidi ya nchi 30 zinazoendelea mapema mwaka huu unafanywa kuwa mbaya zaidi kutokana na sababu kuu ya upotevu na matumizi ya kupindukia ya chakula.

https://p.dw.com/p/F2kN
Cecilia Martinsen Mkurugenzi wa Miradi katika Taasisi ya Kimataifa ya Usimamizi wa Maji akizungumza katika mkutano wa Wiki ya Maji mjini Stockholm Sweden.Picha: Stockholm International Water Institute / José Figueroa

Marekani na baadhi ya nchi zilizoendelea hutupa takriban theluthi moja ya chakula chao kila mwaka hayo yamebainishwa na repoti ambayo Mohamed Dahman anaichambuwa.

_________________________________________

Repoti hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, Taasisi ya Kimataifa ya Usimamizi wa Maji na Taasisi ya Maji ya Kimataifa ya Stockholm imetowa wito wa kupunguza kwa asilimia 50 kwa kima cha chakula kinachopotezwa baada ya kuzalishwa ifikapo mwaka 2025.

Kwa vile kima kikubwa sana cha maji huwa kinahitajika kuzalisha mazao na bidhaa nyegine za chakula kupunguza huko upotevu wa chakula kutaongeza usambazaji wa maji kwa ajili ya kilimo na matumizi ya nyumbani.

Repoti hiyo ilitolewa katika mkutano wa wa kila mwaka juu ya masuala ya maji duniani huko Stockholm Sweden inasema chakula cha kutosha kinazalishwa kulisha watu wenye afya duniani.

Waandishi wa repoti hiyo wanasema nchini Marekani hadi asilimia 30 ya chakula chenye thamani ya dola bilioni 8.3 hutupwa kila mwaka.

Repoti inailinganisha hali hiyo sawa na kuwacha mfereji umwage maji ya lita trilioni 40 kwenye pipa la taka maji ya kutosha kukidhi mahitaji ya familia za watu milioni 500.

Repoti hiyo haikuainisha viwango vya upotevu kwa kuzingatia nchi na nchi lakini imesema viwango kama hivyo vimeripotiwa kuwepo barani Ulaya.

Imetaja utafiti wenye kuonyesha theluthi moja ya chakula nchini Uingereza imetupiliwa mbali huku sehemu kubwa ya chakula hicho ikiwa haikuguswa ikiwa imehifadhiwa kwenye vifurushi vyake halisi.Nchini Sweden familia zenye watoto wadogo hutupilia mbali kama asilimia 25 ya chakula walichokinunuwa na kukipeleka nyumbani.

Dr. Charlotte de Fraiture mtafiti wa Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Maji anasema karibu nusu ya maji yaliotumika kuzalisha chakula duniani yumkini nayo yakawa yamepotezwa bure.

Profesa Jan Lundqvist wa Taasisi ya Maji ya Kimataifa ya Stockholm naye anasema suala la unene ni tatizo kubwa kuliko hata utapia mlo.

Ameeleza kwamba kuna watu milioni 850 duniani kote ambao wanateseka na njaa kila siku kwa kulinganishwa na watu zaidi ya bilioni moja nukta mbili ambao uzito wa mwili wao umekuwa wa kupindukia na wanene mambo ambayo yanaweza kupelekea kukabiliwa na matatizo mbali mbali ya afya ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kisukari na moyo.

Akizungumza pembezoni mwa Mkutano huo wa Kimataifa wa Maji mjini Stockholm Lundqwist amewaambia waandishi wa habari kwamba kuboresha usambazaji wa maji na kupunguza kiwango cha upotevu wa chakula kunaweza kuwawezesha kutowa mpangilio mzuri wa malaji kwa watu maskini na chakula cha kutosha kwa idadi ya watu inayozidi kuongezeka.

Shinizo zaidi kwa maji na uzalishaji wa chakula linakuja kutokana na mahitaji ya nishati inayozalishwa kwa kutumia mazao ya chakula, kilimo chaye kuhitaji matumizi makubwa sana ya maji pamoja na kutokana na ongezeke la idadi ya watu.

Repoti inaona mienendo hiyo itachochea mizozo sehemu nyingi hususan kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika na bara la Asia.

Wataalamu wanatahadharisha kwamba venginevyo tunabadili tabia zetu maji litakuja kuwa tatizo kubwa kwa uzalishaji wa chakula.