1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua za kufunga mikaja na nani awe rais wa shirikisho?

Oumilkher Hamidou7 Juni 2010

Serikali kuu ya Ujerumani inapanga kutangaza hatua za kupunguza matumizi -hakuna sekta itakayosalimika na mchoro mwekundu

https://p.dw.com/p/NjtP
Baraza la mawaziri la serikali kuu ya UjerumaniPicha: picture alliance / dpa

Hatua za kupunguza matumizi, nani achaguliwe kuwa rais wa shirikisho -la Ujerumani na misaada ya maendeleo kwa Bara la Afrika ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazateni hii leo.

Tuanze lakini moja kwa moja na hatua za kupunguza matumizi ya serekali.Gazeti la "NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG " linaandika:

Ama kweli wakati unabadilika: Hapajapita muda tangu serikali ilipoahidi kuwapunguzia kodi za mapato wenye kumiliki hoteli, hivi sasa azma hiyo imepigwa mchoro mwekundu. Enzi za kuvuta wakati na kuchelewesha mambo zimeshapita. La muhimu zaidi kwa sasa ni kuepusha mambo yasizidi kuharibika. Ingawa kupunguza matumizi katika sekta ya jamii haiangaliwi tena kuwa ni miko, seuze tena bajeti ya huduma za jamii ni kubwa mno- lakini hatua hiyo isije ikatafsiriwa kana kwamba serikali inachukua hatua za upande mmoja .Wajasiri mali,benki,wenye kulipwa mishahara mikubwa mikubwa,wenye kumiliki rasli mali na wawekezaji,nao pia wanalazimika kuchangia ili kuepusha mwanya uzidi kukua kati ya maskini na matajiri:

Gazeti la "Badische Zeitung" la mjini Freiburg linahisi kuna sekta ambazo zitasalimika na mchoro mwekundu.Gazeti linaendelea kuandika:

Katika sekta ya elimu na utafiti,mchoro mwekundu hautopita.Kimsingi jambo hilo ni la maana kwa mustakbal wa Ujerumani-lakini wasiwe na uhuru wa kutumia watakavyo.Kila Euro moja inayotolewa haimaanishi kwamba italeta tija eti kwa sababu imetengwa kwa ajili ya elimu. Idara za uchunguzi wa matumizi zinabidi ziwe macho zaidi kuhakikisha mabilioni ya fedha yanayotolewa kwa ajili ya kugharimia miradi maalum, misaada ya fedha kwa wanafunzi na miradi ya uchunguzi zinatumika ipasavyo.Kwa sababu hiyo ndio njia pekee itakayohakikisha mustakbal mwema kwa jamii nzima.

Baada ya serikali ya muungano wa CDU/CSU na waliberali wa FDP kumtangaza waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony, Christian Wulf, kuwa mgombea wao wa wadhifa wa rais wa shirikisho, upande wa upinzani wa SPD na walinzi wa mazingira, Die Grüne, umejitokeza na mgombea wao pia. Gazeti la "Nordbayerische Kurier" la mjini Bayreuth linaandika:

Sigmar Gabriel amezicheza kwa werevu karata zake alipomtangaza Joachim Gauck, mtu asiyeelemea upande wowote kupigania wadhifa wa rais wa shirikisho. SPD wanatambua fika, wengi tuu miongoni mwa wanachama 1244 wa baraza kuu la shirikisho wanampendelea zaidi Gauck badala ya Wulf. Litakua pigo kubwa kwa kansela Angela Merkel kama waziri mkuu wa jimbo la Lower Sachsony atadhoofika kabla ya kuingia mashindanoni au hata kushindwa. Kansela hakuwa na wakati wa kushusha pumzi wala kutafakari kufuatia uamuzi wa Horst Köhler wa kujiuzulu ghafla kama rais wa shirikisho. SPD lakini wame chomoa turufu kwa kumteuwa Joachim Gauck atetee wadhifa wa rais wa shirikisho.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou/DPA

Imepitiwa na: Miraji Othman