1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heiligendamm: Russia yakataa kucheleweshwa kura kuhusu hatma ya Kosovo

9 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBtW

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amesema Russia haijakubali kucheleweshwa kwa miezi sita upigaji kura kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa jimbo la Kosovo la Serbia.

Nicolas Sarkozy amesema hatua za kuridhisha hazikupigwa kuhusu suala hilo kwenye mkutano wa mataifa manane yaliyostawi kiviwanda, G8, nchini Ujerumani.

Rais wa Ufaransa alipendekeza upigaji kura ucheleweshwe ili kutoa muda wa kuafikiana na akasema Russia inapaswa kutambua kwamba Kosovo ina uwezekano mkubwa wa kuwa huru.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likizingatia mpango wa mjumbe wa Umoja huo, Maarti Ahtisaari, wa kuipatia uhuru Kosovo kwa usimamizi wa kimataifa.

Kosovo, Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani zinaunga mkono mpango huo wakati ambapo Russia na Serbia zinaupinga.

Viongozi wa Kosovo wenye asili ya Albania wametishia watajitangazia uhuru kutoka Serbia iwapo Russia itatumia kura yake ya turufu kupinga uhuru wa Kosovo.