1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Helikopta mbili za Uganda zapatikana

14 Agosti 2012

Mabaki ya helikopta mbili za kijeshi za Uganda yamepatikana katika msitu wa Mlima Kenya. Helikopta hizo zilianguka katika eneo hilo zilipokuwa njiani kuelekea Somalia.

https://p.dw.com/p/15pGE
Mabaki ya helikopta iliyoanguka
Mabaki ya helikopta iliyoangukaPicha: Reuters

"Helikopta zimepatikana lakini zimeungua kabisa," alieleza afisa mmoja wa jeshi la Kenya. "Hatufahamu hatma ya waliokuwa kwenye helikopta hizo." Msemaji wa jeshi la Kenya, Bogita Ongeri, amethibitihsa kupatikana kwa mabaki ya helikopta hizo. Juhudi za uokozi bado zinaendelea. Mpaka sasa hakuna taarifa zozote juu ya watu kumi waliosemekana kuwa ndani ya helikopta hizo za kijeshi.

Helikopta nyingine ya jeshi la Uganda, ilianguka Jumapili katika misitu ya Mlima Kenya lakini wanajeshi saba wa Uganda waliokuwa ndani ya helikopta hiyo waliweza kuokolewa. Helikopta zote tatu ni za aina ya Mi-24 na zimetengenezwa Urusi. Zilikuwa zikielekea Somalia kuungana na majeshi ya Umoja wa Afrika katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab. Helikopta nyingine ambayo ni aina ya Mi-17 ilianza safari Jumapili kuelekea Somalia na kutua salama mjini Garissa, Kenya, ambapo iliongeza mafuta kabla ya kuendelea na safari.

Clinton aipongeza Uganda kwa juhudi za kulinda amani

Wiki iliyopita, Uganda ilitangaza kwamba itatuma helikopta za kivita nchini Somalia kukiimarisha kikosi cha wanajeshi 17,000 cha Umoja wa Afrika kilichoko nchini humo kupambana na waasi wa Al-Shabaab wenye mafungamano na Al-Qaeda.

Hillary Clinton katika ziara yake ya Afrika
Hillary Clinton katika ziara yake ya AfrikaPicha: AP

Akiwa ziarani nchini Uganda juma lililopita sehemu ya ziara yake ya siku 11 barani Afrika, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton, aliipongeza nchi hiyo kwa mchango wake katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Umoja wa Afrika kushambulia Kismayu

Mbali na Uganda nchi nyengine zinazoshiriki katika kikosi hicho ni Burundi, huku Kenya na Djibuti zikisemekana pia kujiunga. Kenya iliingia vitani dhidi ya waasi wa Al-Shabaab ndani ya Somalia mwaka jana baada ya mashambulizi kadhaa ya kiagaidi nchini Kenya ambapo inaaminiwa yalifanywa na waasi hao.

Mkutano mkuu wa Umoja wa Afrika
Mkutano mkuu wa Umoja wa AfrikaPicha: dapd

Kikosi cha Umoja wa Afrika kinapanga masahambulizi makubwa katika mji wa kusini wa Kismayu, ambao ni ngome kuu ya Al-Shabaab, kabla ya Agosti 20. tarehe hiyo ndipo muda wa serikali ya sasa ya mpito utakapomalizika rasmi. Tayari bunge limepitisha katiba mpya ya muda na hatua hiyo itafuatwa na uchaguzi wa rais pamoja na kuundwa serikali mpya, itakayochukua nafasi ya utawala utakaoamalizika muda wake.

(Kusikiliza mahojiano baina ya Bruce Amani na msemaji wa Jeshi la Kenya, Bogita Ongeri, bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini.)

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman