1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyekuwa Kansela wa Ujerumani Schmidt afariki dunia

Mohamed Abdulrahman/Jeanette Seiffert10 Novemba 2015

Helmut Schmidt anatajwa kuwa ndiye mwanasiasa maarufu zaidi katika historia ya karibuni ya Ujerumani kuliko wote waliowahi kuchaguliwa na akiheshimiwa sana kwa kukisimamia anachokiamini.

https://p.dw.com/p/1H3SU
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Hayati Helmut Schmidt.
Kansela wa zamani wa Ujerumani, Hayati Helmut Schmidt.Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Akihojiwa katikati mwa mahojiano ya televisheni kuhusu deni la Ulaya na jinsi Kansela Angela Merkel Merkel alivyokuwa akiushughulikia mgogoro huo, Schmidt alijibu kwa maneno haya: "Nitapaswa kusita kwa muda mrefu kabla sijajibu kidiplomasia."

Ilikuwa ni nadra sana kwa Schmidt kubabaisha mambo lakini pia hakuwa mtu wa kumeza maneno, kwani daima alizungumza alichokiamini. Aliwahi pia kutoa matamshi makali na hasa baada ya kupumzika harakati za kisiasa, kwa mfano palipohusika na masuala kama nafasi ya Ujerumani katika bara dogo la Ulaya na sera ya Umoja wa Ulaya kuelekea Ukraine. Yote hayo katika kile alichosema ni "siasa za kitoto". Akiulizwa kama Barack Obama ni rais wa kipekee, alijibu: "sikubaliani hata kidogo na hilo".

Mara kwa mara Schmidt alikosoa juu ya maendeleo ya Umoja wa Ulaya, mchanganyiko wa tamaduni nchini Ujerumani na kutumwa kwa wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan na takriban wakati wote aliungwa mkono na umma.

Mapambano dhidi ya Jeshi Jekundu

Wajerumani wengi wanamkumbuka Helmut Schmidt jinsi alivyojizatiti kupambana na kundi la kigaidi la Jeshi Jekundu (RAF) mwaka 1977. Ugaidi wa kundi hilo ulikuwa ni pamoja na kutekwa nyara rais wa Jumuiya ya Wanaviwanda wa Ujerumani, Hans Martin Schleyer, na kutekwa nyara ndege ya abiria ya Lufthansa na kulazimishwa kutuwa uwanja wa ndege wa Mogadishu nchini Somalia.

Madhumuni ya vitendo vyote viwili vya kigaidi yalikuwa ni kutaka kuachiwa huru wanachama wa kundi hilo waliokuwa gerezani, lakini Schmidt hakutaka maridhiano ya aina yoyote katika kukabiliana na kadhia hizo.

Aliweza kudhihirisha uwezo wa dola kuwalinda raia wake dhidi ya vitisho na baadaye akafafanua juu ya msimamo aliochukuwa. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kupata imani ya wananchi kuhusiana na jukumu la serikali kuwalinda. Ulikuwa uamuzi ulioyaweka madaraka yake hatarini.

Historia kisiasa

Maisha ya kisiasa ya Schmidt yalianza baada ya kujiunga na chama cha SPD mwaka mmoja baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hata alipokuwa waziri wa ndani katika serikali ya mkoa wa Hamburg, alipata sifa ya kuwa mtu mwenye maarifa ya kutatua matatizo.

Mwaka 1964 akateuliwa kuwa mwenyekiti wa wabunge wa chama chake na baada ya kuundwa serikali ya mseto ya Shirikisho kati ya SPD na FDP 1969, kansela wakati huo Willy Brandt akamteuwa kuwa waziri wa ulinzi.

Brandt alijiuzulu 1974 kutokana na kashfa ya Guillaume - afisa katika ofisi yake aliyekuwa jasusi wa Ujerumani Mashariki, na Schmidt akawa mrithi wake, akiwa kansela wa tano wa Ujerumani.

Alipata ridhaa ya umma na kuchaguliwa 1976 na 1980, lakini ilipofika 1982 serikali yake ya mseto na FDP ikakumbwa na msukosuko na FDP kujitoa. Uchaguzi uliofuata Schmidt, hakufanikiwa kuunda serikali. FDP iliamua kushirikiana na CDU/CSU.

Migogoro ya kisiasa

Miaka iliofuata ilikuwa ya mivutano ndani ya SPD, huku Schmidt akichukuliwa kama mtu aliyepinga maamuzi ya mikutano mikuu ya chama. Kubwa zaidi lilikuwa ni utekelezaji wa kile kilichoitwa uamuzi wa ncha mbili kuhusiana na utegaji wa makombora ya Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi (NATO) barani Ulaya. Schmidt alipendelea utegaji zaidi wa makombora ya Marekani katika ardhi ya Ujerumani. Schmidt aliuona upinzani ndani ya chama chake kuwa ni "kutouona ukweli wa mambo ulivyo".

Alipojiondoa kwenye siasa, Schmidt alikuwa mhariri mshirika wa gazeti maarufu la kila wiki, "Die Zeit", pamoja na kutoa mihadhara mbali mbali juu ya masuala ya kisiasa na kiuchumi duniani.

Mwandishi: Mohammed Abdul-rahman/Jeanette Seiffert
Mhariri: Saumu Yusuf