1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hertha Berlin yakamata nafasi ya tatu

Bruce Amani
28 Novemba 2016

Hertha Berlin wamekamata nafasi ya tatu katika ligi kuu hiyo ya kandanda hapa Ujerumani, baada ya kuwalaza Mainz 2-1. Timu zote hata hivyo zilimaliza mechi na wachezaji kumi kila upande

https://p.dw.com/p/2TNwg
Deutschland Hertha BSC v 1. FSV Mainz 05
Picha: Getty Images/Bongarts/B. Streubel

baada ya Vedad Ibisevic ambaye alifunga magoli yote ya Hertha kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutimuliwa uwanjani hatima iliyompata pia Jean-Philippe Gbamin wa Mainz

Awali, Schalke iliendeleza kampeni yao nzuri ya kupanda juu katika ligi, baada ya kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Darmstadt. Matokeo hayo yanaiacha Schalke katika nafasi ya nane na hawajashindwa katika mechi 11 za mwisho katika mashindano yote kufikia sasa. Markus Weinzierl ni mkufunzi wa Schalke "Nadhani tuliweza kushinda leo lakini timu ilikabiliwa na shinikizo kubwa sana. Lakini ikajitahidi na kusawazisha na kisha katika kipindi cha pili tukashinda mchuano".

Siku ya Jumamosi, Bayern Munich ilisajili ushindi wa 2-1 dhidi ya Bayer Leverkusen na beki Mats Hummels aliyeifungua Bayern bao la ushindi alikiri kuwa bado ipo kazi ya kufanywa "Tulikuwa na matatizo mengi hasa mwishoni, kwa sababu hatukushambulia hata mara moja, walituweka chini ya shinikizo na tumeona kuwa bado hatujiamini kwa asilimia 100".

Dortmund walizidiwa nguvu na Frankfurt
Dortmund walizidiwa nguvu na FrankfurtPicha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Ushindi huo ulipunguza kwa pointi tatu pengo kati ya Bayern na vinara wa ligi RB Leipzig ambao walijiimarisha kileleni kwa kuwakandamiza Freiburg 4-1 siku ya Ijumaa matokeo ambayo yalimpa tabasamu kubwa kocha wao Ralph Hasenhüttl. "Ulikuwa mchezo mzuri sana kwetu kwa hakika. Nadhani tulicheza vizuri tangu mwanzoni na tumeonyesha pia kuwa tulitaka kushinda. Baada ya kusawazisha tukaanza kushambulia na kisha tukatapa bao la pili na tatu. Hiyo inaonyesha aina ya mchezo wetu na mwishowe tulistahili kupata ushindi huo".

Borussia Dortmund waliangukia pua baada ya kulazwa 2-1 na Eintracht Frankfurt ambao walisonga katika nafasi ya nne pointi 24 sawa na Hertha katika nafasi ya tatu. Nico Kovac ni kocha wa Einttracht "Timu imeshinda na sio kwamba BVB wametuzawadia ushindi huu leo. Tulilazimika kuufanyia kazi kwa dakika 90, lakini wakati mwingine tumelazimika kukabiliwa na hali ngumu kama hiyo, na ninajivunia timu hii. Naipongeza kwa ilichokifanya".

Dortmund wameteremka hadi nafasi ya saba na pointi 21 nyuma ya Hoffenheim na Cologne ambazo ziko na pointi 22 kila mmoja.

Borussia Moenchengladbach walitekwa kwa sare ya 1-1 na Hoffenheim, maana kuwa hawajashinda mchuano wowote kati ya saba za mwisho. Wolfsburg wana pengo la pointi mbili juu ya eneo la kushushwa daraja baada ya kutoka sare ya 0-0 na Ingolstadt. Katika matokeo mengine Hamburg ilitoka sare ya 2-2 dhifi ya majirani zao Werder Bremen wakati Cologne ilishindwa kufunga katika sare ya 0-0 na Augsburg.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu