1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Heshima na uhuru ni haki ya kila binadamu

P.Martin11 Desemba 2006

Misingi ya uhuru,usawa na amani duniani ni kutambua heshima na haki ya kila binadamu isiyoachanishika.

https://p.dw.com/p/CHlw

Hilo ni azimio la Katiba ya Umoja wa Mataifa iliyotangazwa mwaka 1948 kuhusika na haki za binadamu.

Katiba ya Umoja wa Mataifa ni matokeo ya yale yaliyoshuhudiwa kwenda kinyume na haki za binadamu.Azma ya misingi hiyo ni kuwawezesha binadamu kuishi pamoja duniani,lakini yadhihirika kuwa misingi hiyo imesahauliwa na kwa mara nyingine tena haki za kuwa na uhuru zipo hatarini.

Kwa mfano,waziri wa mambo ya nje wa Urussi Sergei Lavrov anapolituhumu Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya,kuwa linajishughulisha sana kuheshimu haki za binadamu,hiyo labda ingeweza kuchukuliwa kama ni ishara nzuri.Hiyo huonyesha kuwa kwa kiwango fulani hutoneshwa pale ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo na hata huko Kazakstan unaporipotiwa rasmi.

Lakini tangu mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001,hisia kama hizo zimepunguka sana katika uwanja wa kisiasa.Hata katika nchi zenye sheria za kidemokrasia kama vile Marekani,hatua za kulinda usalama zilizopitishwa baada ya mashambulio hayo,zimeathiri haki za uhuru na hivyo kusababisha migogoro kadhaa kati ya mahakama na serikali.

Kwa mfano,sheria inayozuia mateso inapokiukwa,huo ni ukiukaji mkubwa kabisa wa haki za binadamu. Kwa hivyo sasa tume ya Baker iliyoundwa nchini Marekani kuchunguza sera za nchi hiyo huko Irak hatimae ikiamua kutumia diplomasia kupiga vita ugaidi,badala ya kutumia nguvu za kijeshi na kukiuka haki za binadamu kwa mpangilio,hiyo basi ni ishara nzuri.

Binadamu wataweza kuishi pamoja ikiwa,bila ya kujali kama ni vita dhidi ya ugaidi, Ukimwi,umasikini au kuzuia matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake,suluhu lililo bora litagombewa na sio kupigia debe matumizi mabaya ya nguvu.Na hapo ni serikali tu itakayoweza kusaidia,kwa kuonyesha mfano mzuri na vile vile daima kuwa na msimamo ulio wazi kuhusu haki za binadamu.Kwani ni serikali iliyo na uwezo wa kuhakikisha heshima na uhuru wa kila mmoja na hivyo kutoa nafasi ya kuwa na utulivu wa nchi.

Kwa jumla,azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mikataba inayohusika na azimio hilo hutoa fursa ya kuongoza majadiliano na maendeleo ili kuwawezesha binadamu kuishi pamoja katika jamii sehemu mbali mbali za dunia.Ukiukaji wa azimio hilo humaanisha kuwa binadamu wananyanganywa msingi muhimu na ulio bora kabisa katika enzi hii.