1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hilary Clinton abwaga manyanga

Miraji Othman10 Juni 2008

Hilary Clinton anajitoa na anamuunga mkono Obama

https://p.dw.com/p/EGms
Seneta wa Mkoa wa New York, Marekani, Bibi Hilary ClintonPicha: AP

Kila jambo lina mwisho, lakini sio watu wengi waliotegemea mwisho kama huo aliokumbana nao Seneta Hilary Clinton wa Mkoa wa New York, Marekani.

" Nasimamisha sasa kampeni yangu ya uchaguzi na nataka kumpongeza Barack Obama kwa ushindi wake mkubwa na namna alivoendesha mchuano huu. Mimi nasimama nyuma yake na ninamuahidi kumuunga mkono kimalifu."

Maneno hayo aliyatamka jumamosi iliopita huko Washington, akiwa mtulivu, tena mbele ya maelfu ya washabiki wake. Ndoto yake ya kutaka kuwa rais wa kwanza wa kike wa Marekani aiweke pembeni, angalau kwa sasa. Kwa hivyo, sasa njia ni wazi kwa Barack Obama, seneta wa mkoa wa Illinois, kuwa mtetezi wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika kuwania urais wa Marekani. Siku nne kabla, alikuwa ameshapata idadi inayotakiwa ya kura kuweza kuidhinishwa na mkutano mkuu wa Chama cha Democratic kuwa mtetezi. Lakini Hilary Clinton alipokuwa anakiri kushindwa, usoni mwake kulikuweko wazi alama za kuvunjika moyo. Bibi huyo, tangu alipoanza kampeni yake miezi 17 iliopita, aliwekewa matumaini makubwa na watu kwamba atachomoza kuwashinda madume wa Chama cha Democratic waliokuwa wanachuana naye. Lakini licha ya kushindwa, Hilary Clinton amekiruka kivuli chake, na ile kauli mbiu aliokuwa akiitumia: Naam , tunaweza, sasa imekuwa sio tena ndoto, hasa kwa wanawake. Alitaka kuweka mfano, kuwa rais wa kwanza wa kike wa Marekani, lakini alishindwa chupu chupu.

Kutokana na mbinyo wa wakuu wa Chama cha Democratic waliomshauri bora abwage manyanga ili kukinusuru chama kisiwe na mgawanyiko katika mkutano mkuu wa kutafuta mgombea, Hilary Clinton hajawa na chaguo lengine.

Hata hivyo, licha ya kushindwa kuwa mtetezi wa urais, lakini amefikia mengi. Kampeni yake imedhihirisha kwamba yawezekana kwa Marekani kuwa na amiri jeshi mkuu aliye mwanamke. Katika nchi nzima ya Marekani, wanawake waliingiwa na ari pamoja na fahari kutokana na yeye kujibwaga katika mchuano mkali kama huo. Ujasiri wake ulikuwa kilele cha lile vuguvugu liloanza katika miongo iliopita ya kutaka usawa wa kijinsia.

Mwanamke mmoja alisema hivi:

"Haya ni matokeo ya kihistoria, kwamba kwa mara ya kwanza, mwanamke amefikia umbali huu aliofikia Hilary, licha ya kwamba mwishowe ameshindwa. Mimi ni mshabiki wa Obama, lakini nina fahari kwa Hilary Clinton kwa kile alichofikia kwa niaba ya sisi wanawake."

Kwamba Hilary Clinton hajafaulu haijatokana kwamba yeye ni mwanamke, ila tu kuna makosa fulani alifanya katika kampeni yake; hata hivyo, amefungua njia kwa wanawake wengine wanaotaka kuwania wadhifa wa urais na nyadhifa nyingine muhimu. Sasa kwamba yeye amefikia alipofikia, itakuwa rahisi kwa wanawake wengine kuendeleza.

Pamoja na Barack Obama, Hilary Clinton ameweza kuwavutia wanawake milioni 35 kushiriki katika chaguzi hizo za michuano; kiwango kikubwa kabisa kuwahi kufikiwa. Kwamba alibakia anashindana hadi mwisho yaonesha vipi mikoa yote 50 ya Marekani yalivovutiwa na mwanamke huyo.

Akiwaashiria wanawake waliomuunga mkono kwa wingi na kile wanachoweza kufikia, yeye akiwa ni mfano, Hilary Clinton alisema:

"Moyo wangu utavunjika ikiwa, kutokana na kujitoa kwangu katika kampeni, wengine watavunjika moyo kufikia malengo yao. Kwa hivyo, wekeni malengo yenu juu, fanyeni kazi kwa bidii na jishughulisheni na kile ambacho mnakiamini.Pale mnapojikwaa au kuanguka, simameni tena na msiwache kusonga mbele; msiwasikilize wale wanaokwambieni msalimu amri."

Amewapa hisia raia kwamba kila kura yao moja ina umuhimu na inatiliwa kweli maanani.

Hilary Clinton katika kampeni alisimamia mambo yaliokuwa yanamgusa sana yeye na raia wengi, kwa mfano, alipigania bima kwa raia wengi wasioweza kujilipia gharama za matibabu, elimu kwa wote na umaskini upigwe vita.

Aliwaambia hivi wafuasi wake pale alipobwaga manyanga:

"Kwa miaka 40 nimekuwa katika siasa, katika wakati huo kumekuweko chaguzi kumi za urais, lakini ni mara tatu tu ndipo Chama cha Democratic kimeshinda. Nafasi nyingi tumezipoteza tukiwa sasa katika mwaka wa saba wa kipindi cha George Bush, katika upande wa siasa za kigeni, mazingira, uchumi, afya au elimu. Tusiwachie nafasi hii tulikuwa nayo sasa ikatuponyoka. Tumefikia mbali na tumepata mengi."

Kwa vyovyote Barack Obama ili aweze kushinda katika uchaguzi wa urais hapo Novemba mwaka huu,atahitaji aungwe mkono na Hilary Clinton na apate kura za wafuasi wake . Ushindi alioupata mke huyo wa rais wa zamani Bill Clinton katika majimbo ya New Hampshire, California, Ohio na Pennsylvania, Kentucky na Puerto Rico unaweza ukatumiwa kumzawadia Barack Obama kura ambazo alizikosa, hasa zile za wafanya kazi wa viwandani, watu wasiokuwa na elimu sana watu wenye asili ya nchi za Amerika ya Kusini, wazee na wanawake, hasa wanawake vikongwe.

Hata mwenyewe Barack Obama alikiri kwamba kutokana na mchuano alioupata kutoka kwa Hilary Clinton ndio maana akawa mtetezi aliye bora, tena, la muhimu, kuwa tayari kupambana na mtetezi wa urais wa Chama cha Republican , John McCain.

Sasa kibarua kiko kwa Barack Obama, kama atamchaguwa Bibi Clinton kuwa mgombea wake mwenza, na bibi huyo hajajivunga: amesema hapiganii kuwa na nafasi hiyo, lakini akitukiwa haifikiriwi kama ataikataa. Amewaambia wafuasi wake milioni 18 waliompigia kura katika chaguzi za mchujo kumuunga mkono Barack Obama kwa nguvu zote, lakini maneno yake hayo sio wazi kabisa, ni ya tahadhari. Hajataka kuuudhi uongozi wa chama chake, kwani kwa vyovyote huenda akakihitaji chama hicho katika siku za mbele. Atajiweka kidogo mbali na Barack Obama akingoja labda mshindi huyo huenda akafanya makosa mnamo miaka minne ambapo atakuwa rais. Hapo bibi huyo atakuwa na mdomo mpana wa kusema: Mnaona , Sijakwambieni? Na mwishowe isikatalike, huenda baada ya miaka minne kutoka sasa, yaani mwaka 2012, Hilary Clinton akajaribu tena.

Kibarua kingine alichokuwa nacho Barack Obama ni kumshinda mtetezi wa urais kwa tiketi ya Chama cha Republican, John McCain ambaye alimuelezea hivi:

"Obama maisha anatoa sura nzuri mwanzoni, lakini hajawahi kufikia maamuzi makubwa, kinyume na mimi."

Malumbano hayatakoma hadi Novemba, kwani mwenyewe Barack Obama aliwaambia wafuasi wake kama hivi:

Insert: Obama...

"Leo tunaadhimisha mwisho wa safari ya kihistoria kwa kuanza safari nyingine ya kihistoria."

Tuombe tu Mungu amfikishe salama katika safari hiyo...