1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton aanza ziara ya kukuza demokrasia kwa nchi zilizokuwa umoja wa kisovieti

2 Julai 2010

Rais wa Ukraine akusudia kujiunga na Umoja wa Ulaya,kuliko kuwa mwanachama wa NATO.

https://p.dw.com/p/O9Hk
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton akisalimiana na wananchi wa Ukraine.Hiyo ilikuwa mwaka 1997 wakati akiwa mke wa Rais mstaafu Bill Clinton.Bi Hillary ameanza ziara ya kutembelea Kiev leo.Picha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton,amewasili nchini Ukraine kwa ziara maalumu itakayosaidia kustawisha demokrasia katika nchi zilizokuwa umoja wa nchi za kisovieti.

Clinton amewasili katika mji mkuu wa Kiev akitokea Washington, ambapo anatarajiwa kutoa hotuba itakayogusia pamoja na mambo mengine,suala la kukuza demokrasia na haki za binaadamu.

Ziara hiyo ya Waziri Clinton, itafuatia na ziara nyingine katika nchi nne zilizokuwa umoja wa kisovieti,katika nchi za Armenia,Azbeijan na Georgia ikiwa ni mkakati wa Marekani kurejesha uhusiano ulioyumba baina yake na Urusi.

Lakini pia imeelezwa kuwa Clinton,atakuwa na ziara kama hizo katika nchi za Poland na Caucasus.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni ya kwanza kwa Waziri Clinton kuzuru Kiev tangu mwezi februari, ulipofanyika uchaguzi uliompa ushindi Rais Victor Yanukovych dhidi ya Victor Yushchenko.

Kwa mujibu wa msaidizi wa kitengo cha mambo kinachoshughulikia mahusiano baina ya nchi za Ulaya na zile za Asia,Phil Gordon amesema kuwa, Marekani inataka kuhakikishiwa juu ya utawala wa nchi hizo za Ulaya ya kati,iwapo zitafuata mkondo wa dola la Urusi,ama lile la Marekani.

Imeelezwa kuwa Waziri Clinton anatarajiwa kufunguwa kamati ya kitengo cha uhusiano, kitakachokuwa na kazi ya kuboresha na kusimamia masuala yanayohusu maingiliano ya kibiashara,nishati,ulinzi na usalama pamoja na masuala yote yanayohusiana na utamaduni baina ya mataifa hayo.

Clinton atakuwa na mazungumzo na Rais Yanukovych na Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine,Kostyantyn Gryshchenko pamoja na wanachama wa asasi za kiraia pamoja na wakuu wa vyombo vya habari,ili kuelezea dhima ya ziara hiyo nchini humo.

Katika kuendeleza mkakati wa Marekani kujiimarisha zaidi kisiasa na uungwaji mkono na jumuiya za kimataifa,Waziri Clinton ataondoka kesho kuelekea Poland,kabla ya kuelekea Caucasus na kumalizia ziara yake kwa nchi za Azerbaijan,Armenia na Georgia kabla ya kurejea Washington siku ya jumanne.

Katika hatua nyingine,Bunge la Ukraine limepitisha muswada wa sheria utakaoliwezesha taifa hilo kuingia katika mikataba ya kibishara na nchi zilizo katika umoja wa NATO,muswada uliokuwa umeandaliwa ukizingatia msimamo wa Rais Viktor Yanukovych,ambaye tangu kuchaguliwa kwake mwezi Februari, ameazimia kuzingatia uhusiano na Urusi.

Pamoja na mambo mengine, muswada huo umeyapa kipaumbele masuala ya kitaifa yanayogusia siasa za nchi hiyo, ikiwemo kuendeleza mkakati wa mahusiano na majeshi ya kujihami ya nchi za mgharibi, NATO lakini bila kugusia suala la uanachama wa jumuiya hiyo.

Kwa upande mwingine, Rais Yanukovych amekuwa akieleza mara kwa mara juu ya msimamo wake wa kupendelea zaidi nchi hiyo kujiunga na umoja wa Ulaya, kuliko kuwa mwanachama wa NATO, huku ikielezwa kuwa siasa za nchi hiyo zimefungamana zaidi na Urusi.

Mwandishi;Ramadhan Tuwa/ AFP

Mhariri:Miraji Othman