1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Historia yaandikwa upya Kenya!

27 Agosti 2010

Rais Mwai Kibaki wa Kenya leo amesaini katiba mpya kuwa sheria, wiki kadhaa baada ya katiba hiyo kuungwa mkono na Wakenya kwenye kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/OxbP
Rais wa Kenya Mwai KibakiPicha: AP Photo

 Umati mkubwa wa watu ulikusanyika katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi kushuhudia rais Kibaki akitia saini katiba hiyo, ambayo ni sehemu ya mchakato wa mageuzi unaolenga kuepusha kutokea tena machafuko ya baada ya uchaguzi wa Disemba mwaka 2007 nchini Kenya.

Rais Bashir ndani ya sherehe

Viongozi mbalimbali barani Afrika akiwemo rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, wamejumuika na maelfu ya Wakenya kushuhudia kusainiwa kwa katiba hiyo mpya. Hii ni mara ya pili kwa rais Bashir kujiweka katika hatari ya kukamatwa kwa kuitembelea nchi iliyosaini mkataba wa Roma, uliounda mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya kivita, ICC, iliyotoa waranti Bashir akamatwe kujibu mashtaka ya uhalifu wa maovu dhidi binadamu na mauaji ya halaiki katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.

Kenia Odinga Antrittsrede als Premier freies Bildformat
Waziri Mkuu Raila Odinga na Rais Mwai Kibaki pindi baada ya kuunda serikali ya Umoja wa KitaifaPicha: AP

Ni siku ambayo Wakenya wameisubiri kwa zaidi ya miongo miwili- wengi walikuwa wamepoteza matumaini kwamba watashuhudia Kenya mpya, Kenya itakayokuwa na katiba mpya. Bustani ya Uhuru park jijini Nairobi imeweka historia si moja wala mbili, na leo itakuwa inaweka historia nyingine pale Rais Mwai Kibaki atapoitia saini katiba mpya- na kisha kula kiapo cha uaminifu kwa katiba hiyo na kwa taifa la Kenya. Kilele cha sherehe ni pale Rais Kibaki atakapotoa hotuba yake.

Kula viapo upya

Wengine watakaokula kiapo upya ni Waziri Mkuu Raila Odinga  Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka, Spika wa bunge la Kenya, Kenneth Marende na Jaji Mkuu Evan Gicheru. Hata hivyo afisa wa kwanza kula kiapo kipya itakuwa Jaji Mkuu Evan Gicheru ambaye jukumu lake litakuwa kumuapisha rais.

Rais huyo wa Kenya baadaye atashuhudia kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Mkamu wa Rais na Spika wa bunge. Katika sherehe hizo ambazo zinatajwa kuwa mwanzo wa Kenya mpya- marais wanane wa Afrika watakuwepo katika bustani ya Uhuru kushuhudia siku hii muhimu kwa Wakenya. Rais wa zamani wa Ghana, John Kuffour aliwasili jana nchini Kenya kwa sherehe hiyo. Kuffour alikuwa kiongozi wa kwanza kujaribu kuleta upatanishi wakati Kenya ilikumbwa na mzozo baada ya uchaguzi mkuu uliozua rabsha nchini humo.

Kenia Wahlen Unruhen in Nairobi Großdemonstration
Ghasia zilizotokea Kibera,Nairobi baada ya uchaguzi mkuu wa 2007Picha: AP

Wengine waliohudhuria ni Rais wa Zanzibar Abed Karume na Rais wa Comoro Ahmed Abdallah Sambi. Wageni wengine mashuhuri ni Koffi Annan katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa ambaye alikuwa mpatanishi mkuu wa mzozo nchini Kenya. Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa na Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, pia wapo.

Präsident Omar Hassan al Bashir, Sudan
Rais wa Sudan Omar Hassan al BashirPicha: AP Photo

Mbwembwe zilizofanyika katika bustani ya Uhuru ni pamoja na heshima ya kupigwa kwa mizinga 21, nyimbo na ngoma na kupandishwa kwa bendera kubwa katika bustani hiyo. Mawaziri baadaye wataapishwa katika Ikulu ya Nairobi, huku wabunge wakila viapo upya bungeni kesho jumamosi. Majaji, mahakimu, mwanasheria mkuu na Mkurugenzi wa mashataka pia wataapishwa upya. Kamishna wa polisi, Mkuu wa majeshi pamoja na makatibu wa wizara pia wataapishwa. Kilele cha sherehe hiyo ni karamu itakayoandaliwa na Rais Kibaki na mkewe mama Lucy baadaye.