1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoffenheim imeparamia kileleni tena.

24 Novemba 2008

Hoffenheim imeilaza FC Cologne 3:1 kutwaa tena usukani wa Ligi:

https://p.dw.com/p/G1Cr
Youssef Mohamad wa Cologne azima hujuma za Hoffenheim.Picha: AP

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, chipukizi waliopanda msimu huu daraja ya kwanza Hoffenheim, wameshika tena uongozi wa Ligi wakifuatwa nyuma na Bayer Leverkusen na mabingwa Bayern Munich.

Kombe la Challenge Cup kwa Afrika Mashariki na Kati kuingiza mara hii Saudi Arabia na Zambia na timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa safari nyengine ya Ujerumani mwaka mpya .Katika medani ya riadha mjamiaca Usain bolt na Mrusi Yelena Isinbayeva na mfalme na malkia wanariadha wa mwaka.

Hoffenheim imezusha tena maajabu katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani pale ilipofaulu pia kutamba dhidi ya timu pekee ilioilaza mara 2 msimu uliopita katika daraja ya pili-FC Cologne.Katika changamoto ya timu 2 zilizopanda msimu huu daraja ya kwanza mjini Cologne,jumamosi, Hofefenheim iliikandika FC Cologne mabao 3:1 na kwavile Bayer Leverkusen ilipoteza pointi 3 kwa Armenia Bielefeld ilipochapwa 2-1, Hoffemnhiem sasa inaongoza Bundesliga pekee ikiwa imefungua mwanya wa pointi 3 kati yake na Bayer Leverkusen na Bayern Munich zenye pointi 28 kila moja kwa 31 za Hoffenhiem.Na hivi ndivyo kocha wa Hoffenheim Ralf rangnick alivoueleza mpambano na mahasimu wao wakubwa FC Cologne:

."Takriban dakika 90 nzima tulitamba na tukapata nafasi za kutia mabao na tulijua kuzitumia."

Changamoto ya pili iliokodolewa macho mno mwishoni mwa wiki ilikua ile kati ya mahasimu wawili wa Ujerumani ya kaskazini-Hamburg na Bremen:Hamburg ikicheza nyumbani mwishoe ilitamba kwa mabao 2:1 ingawa Bremen ndio iliotawala uwanja kwa muda mrefu bila ya kutia mabao ya kutosha.

Kocha wa Bremen , Thomas Schaarf ingawa hakupendezwa na ushindi wa hamburg,alitambua kosa la timu yake lilikuwa wapi-hawakutia mabao:" Tulifanya mengi barabara,lakini tulisahau tu kutia magoli licha ya nafasi nyingi tulizopata."

Nae kocha wa Hamburg kutoka Holland akiridhika na pointi nyengine 3 zilizoiweka hamburg nafasi ya 5 ya ngazi ya Ligi alisema:

"Bremen ilitamba zaidi lakini hawakupata mwanya wa kutia mabao.Ukitia bao kama alilotia Ohlich,basi ushindi unastahiki."

Ama katika La Liga-ligi ya Spian, FC barcelona inayocheza na mkamerun Samuel Eto-o, kwa msangao wa mashabiki wao walizimwa sare ya bao 1-1 na Getafe tena nyumbani hapo jana ,hata hivyo, Barcelona wamebakia kileleni mwa ligi ya Spain.

Barcelona iko pointi 3 usoni.Manu del Moral aliwasangaza Barcelona kwa bao lake la haraka ,lakini mwishoe, Barcelona ikiwaambia kutangulia si kufika-Seydou Keita aliwaokoa Barcelona kwa bao lake la kusawazisha.Kusema kweli, Barcelona ilimkosa uwanjani Lionel Messi,chipukizi wao stadi kutoka Argentina.Real Madrid, mabingwa walio pointi 3 nyuma ya Barcelona walishinda kwa taabau Huelva inayoburura mkia wa Ligi.Villareal waliozabwa mabao 3-0 jumamosi na Valladolid wameangukia nafasi ya 3 nyuma ya Real Madrid.

AC Milan imeachwa sasa nyuma na viongozi wa Ligi ya Itali Inter Milan walipomudu suluhu tu ya 2:2 jana na Rorino.Wabrazil Pato na Ronalidinho ambae sasa ndie mtiaji mabao mnegi wa Milan akiwa ameshapichika mabao 6 walinasa tena wavu kwa AC Milan.

Tugkigeukia dimba huko Afrika mashariki na kat: Kombe la Challenge Cup kwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati lakaribia kuanza hapo Desemba 16 na timu mbali mbali za Taifa zajinoa .Mara hii timu mbili zilizo nje ya kanda ya CECAFA zimealikwa ingawa hazitaondoka na kombe-Zambia na Saudi Arabia:Timu ya Taifa ya Zanzibar au "Zanzibar Heroes" inatazamiwa kuja tena Ujerumani mkesha wa mwaka mpya.Itashiriki katika kombe la Challenge na timu B.

Wanariadha wa mwaka 2008 wamechaguliwa jana huko Monte Carlo na wote ni wafalme na malkia wa michezo ya mwaka huu ya olimpik ya Beijing:

Upande wa wanawake, taji la mwanariadha wa mwaka amevikwa mrukaji kwa upongoo-Pole Vault- mrusi Yelena Isinbayeva na upande wa wanaume, si mwengine bali mfalme wa mbio fupi mjamiaca Usain Bolt-bingwa wa olimpik na wa rekodi ya dunia.

Bolt mwenye umri wa miaka 22,alikuwa binadamu wa kwanza kunyakua medali 3 za dhahabu za mbio za masafa mafupi-sprints katika kila finali ya michezo ya Beijing hapo august,mwaka huu.Alikimbia muda wa sek.9.60 kwa mita 100.Muda wa sek. 19.30 kwa mita 200 na sek. 37.10 kwa mbio za kupokezana -relay za mita 100X4.Mapema mwaka huu mjamaica huyo alinyanyua rekodi ya dunia ya mita 100 na kuiweka sek.9.72.

Isinbayeva amevaa taji hilo la "Malkia wa riadha " kwa mara ya tatu baada ya kutwaa taji hilo 2004 na tena 2005. Isinbayeva alinyakua medali yake ya pili ya dhahabu ya olimpik katika michezo ya mwaka huu ya Beijing baada ya kuruka juu kwa upongoo mita 5.05.