1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hofu zimetanda kuelekea maandamano makubwa Misri

12 Desemba 2012

Watu 9 wamejeruhiwa katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo katika wakati ambapo wapinzani na wafuasi wa rais Mursi wanapanga kuundamana, ukipinga au mkono kura ya maoni ya katiba iliyopangwa kuitishwa jumamosi.

https://p.dw.com/p/16zil
Machafuko karibu na kasri la rais mjini CairoPicha: Reuters

Watu tisa wamejeruhiwa pale watu waliokuwa na silaha walipowafyetulia risasi waandamanaji katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo katika wakati ambapo wapinzani na wafuasi wa rais Mursi wanapanga kuundamana, upande mmoja ukipinga na mwengine kuunga mkono kura ya maoni juu ya katiba iliyopangwa kuitishwa jumamosi ijayo.

Wafuasi wa muungano wa vyama na makundi ya kiislam likiwemo lile la Udugu wa kiislam:Uhuru na Haki la rais Mohammed Mursi wanakutana Nasr City umbali wa kilomita 2 kutoka kasri la rais saa sita mchana-Chama cha Al Nour cha nadharia ya salafi kimeamua kutoshiriki katika maandamano hayo.

Upande wa upinzani ukiongozwa na vuguvugu la ukombozi wa taifa na kuongozwa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel,Mohamed Al Baradei,wanapanga kuandamana kuanzia saa nane mchana katika uwanja wa Tahrir,kitovu cha malalamiko yaliyopelekea kutimuliwa madarakani rais wa zamani Hosni Mubarak.

Vuguvugu la ukombozi wa taifa linaloyaleta pamoja makundi yanayofuata nadharia za kiliberali na mrengo wa shoto linapinga kura ya maoni ya katiba iliyopangwa kuitishwa jumamosi ijayo.Wanahisi mswaada wa katiba unafungua njia ya kuenezwa dini nchini humo na haudhamini uhuru wa raia.Upande wa upinzani unahisi mswaada huo wa katiba hauwazingatii wananchi wote milioni 83 wa Misri,ambao asili mia kumi kati yao ni wakristo.

Abdul Bar Zahran,muasisi wa chama kinachopigania Misri huru,mojawapo ya makundi makubwa ya upinzani anasema:"Tunahofia haki za kimsingi za rais hazitaheshimiwa na hazitadhaminiwa na katiba,ndio maana tunaitisha maandamano kote nchini na katika viwanja vyote vya Misri."

Maandamano ya leo yanazusha hofu yasije yakasababisha machafuko mengine baada ya watu sabaa kupoteza maisha yao wiki iliyopita,katika machafuko kati ya wafuasi na wanzani wa rais Mursi.

Hofu hizo zimepata nguvu baada ya kundi la watu waliofunika nyuso zao kufyetua risasi na mabomu ya mikono dhidi ya waandamanani wa upande wa upinzani waliokusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo.Tisa wanasemekana wamejeruhiwa.

Jana rais Mursi amelikabidhi jeshi madaraka ya kulinda usalama hadi matokeo ya kura ya maoni ya katiba yatakapotangazwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu