1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Holbrooke nchini India

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP16 Februari 2009

Holbrooke yuko katika sehemu ya mwisho ya ziara yake iliyompelekea Pakistan na Afghanistan.

https://p.dw.com/p/GvT2
Mjumbe maalum wa Marekani nchini Afghanistan na Pakistan Richard HolbrookePicha: picture-alliance/ dpa

Mjumbe maalum wa Marekani nchini Pakistan na Afghanistan Richard Holbrooke amekutana na maafisa wa ngazi ya juu wa India, kujadili Afghanistan na pia mvutano kati ya India na Pakistan kufuatia mashambulio ya kigaidi ya november 26 mjini Mumbai. Holbrooke aliwasili nchini India hapo jana,akitokea Afghanistan ambako alielezea juu ya sera za Marekani kuhusu vita dhidi ya ugaidi.


Bw Holbrooke yuko katika mji mkuu wa India, New Delhi kwa sehemu ya mwisho yaa ziara yake iliyompelekea Pakistan na Afghanistan. Mjumbe huyo maalum wa Marekani ni afisa wa kwanza wa ngazi ya juu nchini Marekani kuitembea India tangu rais Barrack Obama aingie madarakani mwezi uliopita.Akiwa nchini Afghanistan alielezea wazi msimamo wa Marekani.

Kwa mujibu wa maafisa wa India mashambulio ya November mwaka jana mjini Mumbai yalipewa uzito katika mashauri kati ya bw Holbrooke na waziri wa mambo ya nje wa India Pranab Mukherjee. India imekuwa ikidai watu fulani nchini Pakistan walihusika katika mashambulio hayo yaliyosababisha vifo vya watu 170 na hata kuikabidhi Pakistan ushahidi wake .


Alhamisi iliyopita Pakistan ilikiri kuwa baadhi ya mashambulio hayo yalipangwa katika ardhi yake na kusema kesi ya uhalifu imefunguliwa dhidi ya washukiwa, ambao wengi wao sasa wanazuiliwa na Polisi.


Hapo kabla, Holbrooke alikutana na katibu katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya India Shivshankar Menon na mshauri wa kitaifa wa usalama nchini humo MK Naryanan. Maafisa wa India walitoa wito kwa Marekani kuishinikiza Pakistan kuhakikisha inawachukulia hatua za kisheria washukiwa wa mashambulio ya Mumbai.


Ziara hiyo ya Bw Holbrooke nchini India inafanyika katika wakati mmoja na taarifa za gazeti moja nchini Marekani kuwa maafisa wa upelelezi nchini Marekani waliisadia India na Pakistan kubadilishana maafisa wakuu waowa upepelezi baada ya mashambulio hayo katika mji wa Mumbai.


Mjumbe huyo maalum nchini Afghanistan na Pakistan pia alijadiliana na maafisa wa India kuhusu hali ya mambo nchini Afghanistan na kushamiri kwa harakati za waasi wa Taliban. India ni mhusika katika unenzi mpya wa Afghanistan na imeahidi kutoa dolla billioni 1.2 .