1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande ni Rais Mpya wa Ufaransa

7 Mei 2012

Wapiga kura nchini Ufaransa wamemchagua Francois Hollande kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Ushindi wake dhidi ya Nicolas Sarkozy ni pigo kubwa kwa sera za kubana matumizi kama suluhisho la mgogoro wa fedha barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/14r1T
Rais Mpya wa Ufaransa, Francois Hollande
Rais Mpya wa Ufaransa, Francois HollandePicha: dapd

''Wafaransa, leo tarehe sita Mei, wameamua kuleta mageuzi, kwa kunichagua kuwa rais wa Jamhuri''

Hayo ni maneno ya  rais mteule wa Ufaransa Francois Hollande, alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake waliojawa na furaha usiku wa kuamkia leo, baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais ambao jana ulikuwa katika duru ya pili. Hollande ambaye ni kiongozi wa chama cha kisoshalisti amepata asilimia 51.7 ya kura, dhidi ya asilimia 48.3 za rais anayeondoka, Mhafidhina Nicolas Sarkozy.

Rais Nicolas Sarkozy amekubali kushindwa
Rais Nicolas Sarkozy amekubali kushindwaPicha: Reuters

Vingozi wa Kimataifa wamkaribisha Hollande

Hollande ambaye katika kampeni yake alitoa ahadi ya kuujadili upya mpango wa kubana matumizi barani Ulaya, amesema ushindi wake umeonyesha kuwa mpango huo sio kitu kisichoepukika.

''Najua pia kuwa Ulaya inatuangalia. Matokeo haya yalipotangazwa, nina uhakika, kuna nchi ambazo zimefarijika na kupata matumaini, kwamba hatimaye, hatua za kubana matumizi siyo kitu kisichoepukika''. Alisema Hollande.

Viongozi wa nchi muhimu duniani wamempigia simu Hollande kumpongeza na kumpa ahadi ya ushirikiano. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa Nicolas Sarkozy amempongeza Hollande na kumualika kuitembelea Ujerumani mapema iwezekanavyo. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye pia alimuunga mkono Sarkozy mwanzoni mwa kampeni, amesema atashirikiana na Hollande kuboresha uhusiano kati ya Uingereza na Ufaransa.

Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) spricht am Montag (16.04.2012) beim Empfang zum dritten Jugendintegrationsgipfel im Bundeskanzleramt in Berlin zu den Teilnehmern. Der Jugendintegrationsgipfel dient als Ideenschmiede, wie die Integration weiter voran gebracht werden kann. Foto: Kay Nietfeld dpa
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amempongeza Francois HollandePicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa rais wa Marekani Barack Obama, Jay Carney, amesema Obama ameahidi kufanya kazi pamoja na Francois Hollande, kukabiliana na changamoto nyingi katika sekta za uchumi na usalama.

Nchi za Amerika ya Kusini, zikiongozwa na Brazil yenye uchumi mkubwa zaidi, pia zimempongeza kiongozi mpya wa Ufaransa.

Mpango wa nidhamu ya bajeti mashakani

Francois Hollande alisema kitu cha kwanza atakachokifanya kama rais ni kuwaandikia barua viongozi wenzake wa Ulaya, akiwatolea mwito wa kujadili upya mkataba wa nidhamu katika bajeti. Yeye anataka mkataba huo ushirikishe mpango wenye kugharimiwa na serikali utakaosaidia kuchochea ukuaji wa uchumi, akisema mgogoro wa madeni utakuwa mbaya zaidi iwapo uchumi hautaanza kukua tena.

Ingawa baadhi ya masoko yamekuwa na wasi wasi juu ya urais wa Francois Hollande, profesa wa masuala ya fedha katika chuo kikuu cha Notre Dame huko Ufaransa, Jeffrey Bergstrand, amesema Hollande atataka kuongezwa kwa matumizi barani Ulaya kama njia ya kuuchangamsha uchumi.

Wakati huo huo, rais anayeondoka Nicolas Sarkozy amekubali kushindwa, na kumtakia kazi njema mrithi wake. Amesema anawajibikwa kwa kushindwa huko, akisema alishikilia kikamilifu maadili, lakini akashindwa kuwashawishi wafaransa wengi kuyakumbatia maadili hayo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AP/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu